Music | Lifestyle+Fashion | Antivirus | Love+Relationships | Business+Politics | Sport | TUMA Registrations

You are here:   HomeBusiness+PoliticsPetroli, dizeli bei juu tena
| + -

Petroli, dizeli bei juu tena

Sunday, 14 August 2011 17:50 Deiwaka World News - Political Issues
Print PDF

Petroli, dizeli bei juu tena

Ni mshtuko lakini huo ndiyo ukweli kwamba kesho Mamlaka ya Huduma ya Nishati na Maji (Ewura) itatangaza bei mpya za mafuta ya petrol na dizeli ambazo zitakuwa na nyongeza.

Hii itakuwa kama mchezo wa kuigiza, kwani haijapita wiki tangu ulipozuka mgogoro mkubwa kati ya wafanyabiashara waliowekeza kwenye nishati ya mafuta dhidi ya Ewura.

Ewura ilitangaza bei za mafuta yenye kikomo cha shilingi 2060 petroli, hivyo kuibua mgogoro mkubwa na wafanyabiashara hao waliodai kwamba kiwango hicho kingewapa hasara kulinganisha na bei waliyonunulia.


Kampuni zilizogoma kutoa huduma, zilipewa kitisho cha kunyang’anywa leseni na Ewura, huku Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja akifanya kazi kubwa kuwatuliza wabunge waliokasirishwa na wafanyabiashara waliogoma kuuza mafuta, huku wangine wakipendekeza JWTZ liingilie kati.

Makampuni yote yalikubali kutii agizo la serikali, isipokuwa BP ambayo imefungiwa kuuza mafuta nchini kwa muda wa miezi mitatu, huku watendaji wake wakuu wakifikishwa mahakamani na Ewura.

Wakati wananchi wakiamini kuna unafuu kwa bei hizo kushuka, zipo taarifa kwamba kesho bei ya petroli na dizeli itarudi juu.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Ewura, Titus Kaguo alizungumza jana kwenye kipindi cha Kipimajoto, ITV kuwa kesho mamlaka hiyo itatangaza bei mpya.

“Pengine Jumatatu (kesho) tutatoa bei mpya lakini tulitaka kuwaambia Watanzania kwamba bei zilizokuwepo zilikuwa zinaonesha dalili ya kushuka na hivyo bei huwa zinabadilika badilika, wasije wakashangaa ikionekana Jumatatu bei zikawa na mabadiliko,” alisema Kaguo.

Hata hivyo, ishara kuwa bei itakuwa juu ilitokana na kauli ya Kaguo kwamba thamani ya shilingi imeshuka ukilinganisha na sarafu za kigeni.

“Tunakwenda na hali halisi ya soko kwa kuangalia kiwango cha kubadilisha fedha kinavyokwenda. Thamani ya shilingi yetu imeshuka, kwa hiyo Watanzania waipokee bei kama ilivyo, wasiseme tumenyoosha mikono kwa wafanyabiashara endapo wataona bei imepanda kidogo,” alisema.

Hata hivyo, Kaguo hakuweka wazi mafuta hayo yatapanda bei kwa kiasi gani.