Mwisho wa Gaddafi wawadia
Tripoli, Libya
Utawala wa Rais wa Libya, Muammar Gaddafi umekwisha, jitihada za waasi kumng’oa madarakani ni wazi zimetimia.
Waasi nchini Libya, jana walifanikiwa kuushikilia Mji Mkuu, Tripoli, kisha waliwakamata watoto wawili wa kiume wa Gaddafi na kuwaweka mahabusu.
Mtoto ‘roho’ ya Gaddafi, Saif al-Islam pamoja na kaka yake, Mohamed walikamatwa na waasi usiku wa Jumapili iliyopita. Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imeshatoa hati ya kukamatwa kwa Islam na baba yake ili wakasomewe mashtaka.
Mpaka Uwazi linakwenda mtamboni jana, waasi walikuwa wameshakaribia Ikulu ya Libya, ingawa taarifa zinadai kwamba Gaddafi alishakimbilia Venezuela, huku maofisa wa juu wa serikali yake wakiwa hawajulikani walipo.
WAASI HAWAJUI GADDAFI ALIPO
Leo asubuhi, baada ya waasi kufika Tripoli, walipita wakishangilia ushindi huku wakihoji, “Kanali Gaddafi yuko wapi?â€
Wakati waasi wakishangilia ushindi, kiongozi huyo wa Libya ambaye ametawala nchi hiyo kwa miaka 42, alishatoa kauli kuwa hataondoka.
Aliwataka Walibya wote kujitokeza kupigana kwenye vita hiyo.
"Nipo Tripoli," alikiambia Kituo cha Televisheni cha Libya (Libyan TV) kwa njia ya simu. "Tokeni nje, mpambane, mimi nipo na ninyi mpaka mwisho.â€
GADDAFI ROHO YA PAKA
Pamoja na hali kuonekana kwamba ni lazima ang’oke kwa hatua ambayo waasi wamefikia, taarifa zinasema kuwa mpaka bado Gaddafi na wafuasi wake wanaendelea kushikilia sehemu ndogo ya mji wa Tripoli.