Music | Lifestyle+Fashion | Antivirus | Love+Relationships | Business+Politics | Sport | TUMA Registrations

You are here:   HomeMusicSugu aeleza atakavyoipeleka Anti Virus Ikulu
| + -

Sugu aeleza atakavyoipeleka Anti Virus Ikulu

Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi "Sugu" amesema kuwa ataipeleka mix-tape ya Anti Virus Ikulu baada ya kuzinduliwa.


Sugu alisema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete anastahili kupewa mix-tape hiyo ili ajue hali halisi ya kilio cha wanamuziki wa kizazi kipya.

Alisema, ndani ya Anti Virus, wanamuziki wa kizazi kipya wameeleza matatizo yanayowakabili na kuwataja waziwazi wezi wa kazi za muziki.

Nilishaahidi, na sasa nasisitiza tena. Lazima nimpelekee Rais Kikwete Anti Virus, alisema Sugu na kuongeza: Suala hapa ni siku ya kumkabidhi. Kila kitu kimeshapangwa, kwa hiyo ni utekelezaji ndiyo umebaki.

Uamuzi hapa ni kumkabidhi Anti Virus baada ya uzinduzi. Pengine JK anaweza kuwa ameshaona hizi taarifa kwenye vyombo vya habari na anangoja kwa hamu, kwa hiyo tunamtaka awe na subira, angoje uzinduzi ndiyo nitampelekea mwenyewe.

Kuhusu dhamira ya kumpelekea JK Anti Virus, Sugu alisema: Unajua Rais Kikwete amekuwa na nia njema ya kuusaidia muziki wa kizazi kipya lakini dhamira yake imekuwa ikipindishwa na watu wachache, yeye anasaidia halafu kikundi cha watu kinapora, matokeo yake wanamuziki hawanufaiki.