Waasi wampa JK siku 100
Shari kamili ni ujumbe mkali kutoka kwa waasi uliotumwa kwa viongozi wa nchi, wakiwataka kuachia madaraka ndani ya siku 100, vinginevyo watawaondoa kwa nguvu.

Habari za ndani zinasema kuwa ujumbe huo hatari, umetumwa kupitia waraka pepe na SMS kwenda kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete, wakimpa siku 100 awe ameachia madaraka, vinginevyo wahusika watatumia nguvu.
Ujumbe huo, umeelekezwa pia kwa Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha amesema kuwa serikali inafanya uchunguzi kuweza kuwabaini wahusika na kuwataka wananchi watoe ushirikiano.
Imeelezwa kuwa waraka huo umetumwa na kiongozi wa kikundi cha watu 2,858 ambacho kimejitambulisha kwamba kinatokana na muungano wa askari waajiriwa kutoka majeshi mawili nchini.
Katika madai yao ya msingi, kikundi hicho kinadai kuwa viongozi waliopo madarakani wameshindwa kazi ya kuongoza nchi, hivyo wamewapa siku 100 waondoke, vinginevyo watatumia nguvu kuwaondoa.
“Jeshi la polisi limeanza kufanya uchunguzi kubaini watu hao na wakipatikana tuanze kuwahoji ili hatua zichukuliwe,” alisema Nahodha.
Nakala ya waraka huo wa vitisho ulitumwa pia kwa Jeshi la Polisi Tanzania, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Idara ya Usalama wa Taifa Makao Makuu, Wizara ya Mambo ya Nje, Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na ubalozi wa Marekani Tanzania.
Nakala nyingine zimetumwa kwa Kamanda Mkuu wa Al Shabaab, ubalozi wa Uingereza Tanzania, Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), mashirika yasiyo ya kiserikali ya ndani na nje ya Tanzania pamoja na vyombo vya habari.