Music | Lifestyle+Fashion | Antivirus | Love+Relationships | Business+Politics | Sport | TUMA Registrations

You are here:   HomeBusiness+PoliticsJairo, Ngeleja, Luhanjo waingia kitanzini
| + -

Jairo, Ngeleja, Luhanjo waingia kitanzini

Sunday, 20 November 2011 18:16 Deiwaka World News - Political Issues
Print PDF

Jairo, Ngeleja, Luhanjo waingia kitanzini

Serikali inapitia kipindi kigumu kutokana na kitimtimu cha Wizara ya Nishati na Madini, kilichoanzia kama skendo ya rushwa kwenye Bunge la Bajeti la mwaka 2011-2012, ikimgonga aliyekuwa katibu mkuu wa wizara hiyo, David Jairo.


Kutokana na jitihada za Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), Ludovick Utouh kumsafisha Jairo na skendo ya kukusanya shilingi bilioni moja ili kuwahonga wabunge waweze kupitisha bajeti ya wizara yake, jana (Jumamosi) yaliibuka makubwa zaidi.


Kamati Teule ya Bunge, chini ya Mwenyekiti Ramo Makani, ilisoma ripoti yake na kueleza kubaini ufisadi wa fedha za serikali, hivyo kutoa mapendekezo kwamba Jairo, Luhanjo, Utouh na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja wachukuliwe hatua zinazofaa.


Ilibainishwa ndani ya ripoti kuwa kuna skendo ya kughushi fedha iliyofanywa na Jairo kwa kuandika kiasi kikubwa kuliko malipo yaliyofanyika, jambo ambalo ni kosa la jinai.

Baada ya ripoti hiyo, wabunge walikuja juu kwa kutaka wahusika wafukuzwe na wafikishwe mahakamani na kubainisha kwamba uozo huo ni sehemu ya ufisadi wa mabilioni ya shilingi yanayokwapuliwa kila kukicha serikalini.

Katika ripoti ya Kamati Teule ya Bunge, Jairo alikutwa na hatia ya kukusanya fedha kinyume cha utaratibu pamoja na udanganyifu wa malipo.

Skendo hiyo iliibuliwa na Mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shelukindo aliyesoma bungeni barua ya Jairo kwenda kwa wakuu wa idara zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini, akielekeza kila moja itoe mchango wa shilingi milioni 50 ili kurahisisha kupita kwa bajeti ya wizara hiyo.

Ikaelezwa kuwa idara 20 zilichangia, hivyo kufanya zipatikane jumla ya shilingi bilioni moja ambazo inadaiwa lilikuwa ni fungu la kutoa rushwa kwa wabunge ili wapitishe bajeti ya wizara hiyo.

Baada ya madongo mengi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Mathias Chikawe alisema, serikali imepokea mapendekezo yote ya Kamati Teule ya Bunge pamoja na hoja za wabunge na majibu yatatolewa kwenye mkutano wa sita wa Bunge.