JK: Malipo ya wabunge naidhinisha mimi
Rais Jakaya Kikwete, amesema kuwa maslahi ya wabunge anapitisha yeye kwa mujibu wa sheria ya bunge.

JK, ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook kuwa maslahi yote ya wabunge huidhinishwa kisheria katika ofisi ya rais.
Alisema, sheria inayotumika kupitisha maslahi hayo ya wabunge ni ile Sheria ya Utawala wa Bunge iliyotungwa mwaka 2008.
“Maslahi yote ya wabunge huidhinishwa na rais kwa mujibu wa Sheria ya Utawala wa Bunge ya mwaka 2008 ambayo ndiyo inayotumika wakati huu,” alisema JK.
Kauli hiyo ya JK inafuatia malalamiko ya wanaharakati kuhusu nyongeza ya maslahi ya wabunge, iliyoanza kikao kilichopita.
Inaelezwa kuwa Mkutano wa Tano wa Bunge, wabunge waliongezewa maslahi, jambo ambalo limelalamikiwa na wale ambao walikuwa wanapingana na mtindo wa kuwapa posho lukuki wabunge.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, amelalamikia nyongeza hiyo kwa maelezo kuwa ni kuzidi kuwapa mizigo walipa kodi.