Kili Stars yatupwa nje Chalenji
Timu ya Soka ya Taifa, Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, imetupwam nje kwenye michuano ya Chalenji katika mchezo uliochukua dakika 120 leo, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Stars, imefungishwa virago na Timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ katika mchezo wa nusu fainali baada ya kutandikwa jumla ya mabao 3-1.
Kwa matokeo hayo, sasa Stars itawania taji la mshindi wa tatu, itakapomenyana na Sudan Jumamosi.
Katika mchezo wa leo, Stars ilianza vizuri, ikipoteza nafasi nyingi kabla ya kuandika bao la kuongoza kupitia kwa mchezaji mwenye mbio, Mrisho Ngassa.
The Cranes, walisawazisha kipindi cha pili na kufanya dakika 90, zimalizike huku ubao wa matokeo ukisomeka 1-1.
Dakika 30 za nyongeza, The Cranes walipata mabao mengine mawili, huku moja likiwa la penalti.
Wachezaji wa Stars, watajilaumu leo kutokana na kupoteza nafasi nyingi za wazi ambazo zingeweza kuifanya itoke kifua mbele.
The Cranes, sasa itapambana na Rwanda ‘Amavubi’ kwenye mchezo wa fainali.