Chelsea yaipiga Bayern, yanyakua ubingwa Ulaya
Klabu ya Chelsea, leo imefanya kile ambacho hakikutarajiwa na wengi kwa kuifunga FC Bayern Munich na kuchukua ubingwa wa Ulaya.
Mikwaju ya penalti ndiyo iliamua mshindi wa leo baada ya kumaliza dakika 120 matokeo yakiwa 1-1.


Chelsea imetawazwa bingwa mpya wa Ulaya baada ya kuishinda Bayern kwa mikwaju ya penalti 4-3.
Straika wa Chelsea, aliye raia wa Ivory Coast, Didier Drogba amekuwa shujaa wa klabu hiyo, baada ya kufunga mkwaju wa mwisho ulioipa ubingwa.
Mbali na hilo, Drogba pia aliisawazishia Chelsea bao dakika ya 88, baada ya kuwa imetangulia kufungwa mnamo dakika ya 84.
Drogba pia, aliisaidia Chelsea pale alipomkwatua staa wa Bayern, Frank Ribery aliyekuwa anakwenda kufunga.
Katika tukio hilo, Drogba alipewa kadi ya njano lakini nyota mwingine wa Bayern, Arjen Roben alikosa penalti ambayo iliamuliwa na refa baada ya Ribery kukwatuliwa ndani ya eneo la 18.
Baada ya kukwatuliwa, Ribery hakurudi tena uwanjani, hivyo kiasi fulani kupunguza mashambulizi langani kwa Chelsea.