Music | Lifestyle+Fashion | Antivirus | Love+Relationships | Business+Politics | Sport | TUMA Registrations

You are here:   HomeBusiness+PoliticsHuyu ndiye Ekerege wa TBS aliyetimuliwa
| + -

Huyu ndiye Ekerege wa TBS aliyetimuliwa

Sunday, 20 May 2012 21:21 Deiwaka World News - Political Issues
Print PDF

Huyu ndiye Ekerege wa TBS aliyetimuliwa

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, ameshamsimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango nchini (TBS), Charles Ekerege.

Kigoda ambaye ni waziri mpya, alichukua uamuzi huo ambao ulimgharimu mtangulizi wake, Dk. Cyril Chami.

Chami, alituhumiwa na wabunge kwamba anamlinda Ekerege kwamba licha ya madudu mengi aliyoyafanya, bado hajashurutishwa kusimamishwa kazi.

Skendo ya Chami pamoja na mawaziri wengine, akiwemo Ezekiel Maige (aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii), Mustafa Mkulo (Fedha) na wengine, ndiyo kichocheo cha Rais Jakaya Kikwete, kufanya mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri hivi karibuni. Mabadiliko hayo yaliwapumzisha mawaziri sita, akiwemo Chami, Mkulo, Maige, William Ngeleja (aliyekuwa Nishati na Madini) na wengine.

GOGORO LA EKEREGE LILIPOANZA

Awali, wabunge walikerwa na kauli za mawaziri kuhusu Ekerege.

Mbunge wa Mwibara, Alphaxard Lugora, aliomba mwongozo wa Spika kutokana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami na Naibu wake, Lazaro Nyalandu kutofautiana juu ya uchunguzi dhidi ya bosi wa TBS.

Wakati Nyalandu anajibu swali, alisema uchunguzi wa CAG umekamilika na ameshawasilisha ripoti serikalini, bosi wake, Dk. Chami alisema, uchunguzi huo haujakamilika na unaendelea kufanywa na CAG.

Ekerege anatuhumiwa na kamati za kudumu za bunge, Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na ile ya Hesabu za Serikali (PAC).

Tuhuma hizo ni kwamba aliweka kampuni hewa za kukagua magari nje ya nchi na hivyo kuingizia hasara serikalini ya shilingi bilioni 30 ambazo ziliainishwa kwenye ripoti ya CAG ya hesabu za mwaka jana na ripoti hiyo kusomwa mwaka huu.

Baada ya Lugora kumaliza kuomba mwongozo, alisimama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi aliyesema ni kweli majibu ya mawaziri hayo hayafanani na Serikali imeliona hilo, na Ofisi ya Waziri Mkuu itakusanya ushahidi wote juu ya jambo hilo na itatoa taarifa bungeni.

Lakini Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM) alihoji kwa nini Serikali inashindwa kutoa majibu ya uhakika juu ya suala hilo wakati wabunge wanachotaka kufahamu ni kauli ipi yenye ukweli.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) alisema kamati yake anayoiongoza ya Mashirika ya Umma iliunda kamati ndogo kushughulikia tuhuma zinazomkabili Ekerege na kwamba wakati huo wa kipindi cha bunge, walikuwa wameshawasilisha taarifa kwa spika ambaye alipaswa kuipeka Ofisi ya Waziri Mkuu ili walete taarifa ya utekelezaji bungeni.

Kwa upande wake, Naibu Spika Job Ndugai alikiri kuwa jambo hilo ni la muda mrefu na umefika wakati liishie kwa kupatiwa ufumbuzi kwani linawapaka matope wabunge bila sababu za msingi.