Music | Lifestyle+Fashion | Antivirus | Love+Relationships | Business+Politics | Sport | TUMA Registrations

You are here:   HomeSportSherehe za ubingwa Simba kufuru tupu Dar
| + -

Sherehe za ubingwa Simba kufuru tupu Dar

Monday, 28 May 2012 12:43 Deiwaka World News - Sports News
Print PDF

Sherehe za ubingwa Simba kufuru tupu Dar

Simba SC, ililiteka Jiji la Dar es Salaam ambalo lilivaa sura nyekundu kwa muda, jana Jumapili.

Wachezaji na mashabiki wa klabu hiyo walikuwa wakikatiza mitaa mbalimbali ya jiji hilo wakisherehekea ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2011/2012.

Msafara mkubwa wa magari, pikipiki na watembea kwa miguu, ulipita kwa shangwe katika barabara kubwa na mwisho ukaelekea kwenye Ukumbi wa Dar Live, Mbagala, Zakhem kwa ajili ya kuhitimisha sherehe hizo.

Kazi ilianzia makao makuu ya klabu hiyo, Msimbazi, Kariakoo saa sita mchana, ambako maelfu ya wananchi walifurika wakiwa na magari, pikipiki na wengine wakitembea kwa miguu huku wengi wao wakiwa na flana na bendera za Simba.

Msafara ulitoka Msimbazi kupitia Barabara ya Morogoro kuelekea Ubungo, lakini ulipofika maeneo ya Jangwani, kiungo Uhuru Selemani, alipandwa na ‘mizuka’ na kushuka ndani ya gari kubwa la wazi walilokuwemo wachezaji na kuanza kucheza na mashabiki kabla ya kupanda tena garini.

Wachezaji wa Simba walionekana ni wenye furaha kubwa walipokuwa wakikatiza mitaa mbalimbali na walifungua shampeini kadhaa kuonyesha furaha yao.

Kila msafara ulipopita, mashabiki wengi walikuwa pembeni ya barabara wakipunga mikono na bendera juu kwa furaha kubwa.

Ulipofika Ubungo, msafara ulipita Barabara ya Mandera kisha ukatokezea Tazara, ukakatia BMT maeneo ya Sabasaba na kuingia Dar Live majira ya saa 11 jioni.

Hata hivyo, msafara ulipokuwa maeneo ya Ubungo External, mvua ilianza kunyesha lakini wachezaji waliendelea kushangilia na kuruka juu.

Ndani ya Dar Live mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali, alipokuwa akiingia ndani, mashabiki walianza kumshangilia na kupiga naye picha.

Katibu mkuu wa zamani wa klabu hiyo, Mwina Kaduguda, alipewa jukumu la kutoa historia fupi ya Simba, kuna muda alitaka kukatisha lakini mashabiki wakamsisitiza aendelee.

Katika hotuba yake hiyo, Kaduguda alisema ana mpango wa kutengeneza kitabu cha historia ya Simba ambapo asilimia mbili ya mapato ataipeleka katika klabu hiyo.

Naye makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Godfrey Nyange ‘Kaburu’, aliwaahidi wanachama wa klabu hiyo kwamba atafanya shughuli kubwa ya arobaini ya kiungo Patrick Mafisango, aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Mei 17, mwaka huu kwa ajali ya gari jijini Dar es Salaam.

Mgeni rasmi wa sherehe hizo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo ambaye ni Mbunge wa Mvomelo, Amos Makala, aliwapongeza wachezaji na viongozi wa timu hiyo kwa ubingwa walioupata.

“Ninachowaomba ni kutobweteka na ubingwa huu ili muweze kufanya vizuri zaidi,” alisema Makala ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Watunza Fedha Simba huku akisisitza kuwa yeye ndiye aliyemshawishi Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga, aachie ngazi ili kuinusuru klabu hiyo.

“Nawataka pia viongozi wa Simba mjenge uwanja wa kisasa zaidi ya ule wa Azam (Chamazi), sisi kama serikali tutatoa sapoti kubwa,” alisema Makala ambaye pia aliwavalisha medali wachezaji wa Simba.

Tuzo moja ilitolewa kwa ajili ya marehemu Patrick Mafisango ambayo ilipokelewa na nahodha wa Simba, Juma Kaseja lakini wakati wa tukio hilo wachezaji pamoja na baadhi ya mashabiki waliangua kilio.

Baada ya tukio hilo, uongozi wa ukumbi wa kisasa wa Dar Live ulitoa zawadi ya shilingi milioni tatu kwa Simba kutokana na kutwaa ubingwa huo.