Music | Lifestyle+Fashion | Antivirus | Love+Relationships | Business+Politics | Sport | TUMA Registrations

You are here:   HomeLove+RelationshipsUsistaduu, ubrazameni na mapenzi ya kichina
| + -

Usistaduu, ubrazameni na mapenzi ya kichina

Sunday, 03 June 2012 21:03 Deiwaka World News - Love+Relationships
Print PDF

Usistaduu, ubrazameni na mapenzi ya kichina

Mapenzi yamekuwa magumu. Ni mzigo mzito kuubeba. Yanendelea kujeruhi wengi, bado ni mateso kwa wengine. Sasa hivi, asilimia kubwa ya watu, inaamini kwamba kupata mwenzi sahihi wa maisha ni ndoto za alinacha. Ni kamari, ni bahati nasibu.

Maendeleo yamekuja na mambo leo. Kile kinachoonekana ni uzungu, kimeathiri kwa kiasi kikubwa ustaarabu wetu. Mila na desturi zetu, vimepokwa na utandawazi uliotujia. Hii inamaanisha kwamba uhusiano wa kimapenzi wa sasa, hauendani na sura ya utamaduni wetu.

Vijijini kuna unafuu japo na kwenyewe fujo zimeshaingia na mambo yameshabadilika. Mijini ndiyo matatizo yenyewe. Ulimwengu wa digitali na fursa za mitandao zinatutia wazimu. Tunataka kuiga mitindo ya maisha ya wenzetu, matokeo yake tunageuka watumwa wa mapenzi.

Hayakuletwa mapenzi ili yawaumize watu, yapo kwa ajili ya kutoa faraja ndani ya jamii. Yalivyo ni kwamba baada ya misukosuko ya kimaisha, vurugu mechi za kusaka riziki na mihangaiko mingine ya kimaisha, angalau unaweza kusahau yote unaporejea kwa mwenzi wako.

Hata hivyo, mapenzi hugeuka matatizo pale ambapo kazini umeondoka pakiwa moto, unarudi nyumbani nako pia unakuta moto. Unakosa sehemu ya kwenda kujishikiza. Faraja inaota mbawa. Hapa ndipo tafsiri ya mapenzi inapokosa mashiko. Jitazame, muangalie na mwenzako!

Japo ni ukweli usiopingika kuwa mapenzi siku zote hayapo tambarare hata kwa wenza waliostaarabika, ila katika kundi la mabrazameni na masistaduu ni mtihani. Kuna usemi kwamba glasi hugongana kabatini, nakubaliana nao lakini kwa makundi hayo ni pasua kichwa.

Mabrazameni na masistaduu ni zao la mapenzi ya kichina, yaani uhusiano bandia. Inawezekana akiwa kwako akajilegeza kama amefika, kumbe anao wengine wengi. Hili ni janga zito kwa maisha ya sasa. Uaminifu haupo, uzinzi na usaliti vimekuwa fasheni ya kutukuzwa.

Wengine siyo masistaduu wala mabrazameni, wapo kawaida au pengine wana muonekano wa heshima mno. Hata hivyo, ukichimbua hulka zao ndiyo utachoka. Ni wakali wa kuwapanga foleni, akitoka kwa huyu anakwenda kwa yule. Mapenzi yametawaliwa na rangi ya Shetani.

Wapo wanaobadili wapenzi kwa sababu za tamaa, lipo kundi linaloamini miili yao ni mtaji wa kupata fedha, wengine shida za maisha, zikasababisha uamuzi huo wa kujidhalilisha, wapo ambao ni tabia. Bila kugusa huku na huko hatosheki. Makundi yote hayo yamezingirwa na Ibilisi.

Mume wa mtu, anapewa sifa ya ‘uchapaji’ wa vidosho. Kwamba anajua kuwapanga kila kona. Nyumba za kulala wageni, anaingia kama nyumbani kwake. Yaani wanamjua, ni mteja wao hodari. Akifika, wanampeleka kwenye chumba anachokipenda.

Wapo wanaopiga simu, yaani namba za nyumba za kulala wageni zimejaa kwenye simu yake. Akijibiwa kwamba Sinza Kumekucha hakuna vyumba, anapiga Vatican, nako akikosa anajaribu Mori. Inahitaji sala na dua kuishi na mtu wa aina hiyo. Kuna mawili, kama hatakupa maradhi, omba usijue tabia yake, atakuua kwa presha.

Mke wa mtu mkali wa mafiga matatu mpaka matano. Anaita vidumu. Anaingia hoteli na gesti bila woga. Wapo wanaodiriki kuwaingiza wanaume ndani ya nyumba zao, wakati waume zao wakiwa hawapo. Balaa likamkuta yule mwanamke wa Kenya, akagandiana na mwanaume aliyemuingiza chumbani kwake, juu ya kitanda anacholala na mumewe.

Wengine ni ujasiri wa asili, wapo wanaofanya hivyo kwa sababu wanaona fasheni. Katika kundi hili wanaorukaruka, wakijiona ni fasheni ndiyo shabaha yangu kubwa. Itapendeza zaidi mapenzi yakikaa kwenye mstari wake ulionyooka. Maana halisi isipindishwe.

Kama ambavyo Jennifer Lopez, anavyobadili wanaume Marekani, eti na hapa Bongo, Wema Sepetu naye hajambo. Nimeshazungumza mara nyingi na Miss Tanzania huyo wa mwaka 2006-07, hata siku moja hajawahi kuonesha kujuta kwa safari yake ya kubadili wanaume ovyo.

Naseeb Abdul ‘Diamond’, Jumanne Kihangala ‘Mr. Chuz’ na wengine mfano wao, kama Sean Combs ‘P. Diddy’, Christiano Ronaldo na wengineo. Ni mwendo wa kimagharibi. Hakuna mapenzi, ila kupozana haja. Wakitamaniana, wanamalizana leoleo tu. Ameimba Ali Kiba kwenye wimbo Single Boy.

KIINI CHA MAPENZI YA KICHINA

Kuna ulimbukeni uliwaingia watu. Ghafla, kuna tabaka fulani (wakiwemo hawa mastaa wetu), wakaanza kuona mapenzi kama mchezo. Yaani, mtu anaweza kuhusika kimapenzi na mwenzake hata kama hawapendani. Angalia skandali za Wema, Diamond, Jokate Mwegelo, Irene Uwoya na wengineo.

Ni mtindo wa kuyabeba mapenzi kama mchezo wa kujifurahisha. Masistaduu na mabrazameni, hawayabebi kwa uzito wake unaostahili. Wewe msomaji wangu, unayeamini maadili na unathamini moyo wako, utakosea kupita kiasi endapo utaacha njia inayopendeza na kushika mtindo huu wa kimapenzi.

Jaribu kutafakari: Leo inazungumzwa kwamba Diamond anatoka kimapenzi na Aunt Ezekiel. Hapohapo, tambua kuwa Wema alikuwa mchumba wa staa huyo wa Bongo Fleva. Ongeza lingine kuwa Jokate naye kapita kwa kijana huyohuyo. Halafu nakupa siri moja kuwa wote hao ni washiriki wa Miss Tanzania mwaka 2006.

Inamaanisha kuwa walikaa kambi moja lakini wamediriki kuchangia mwanaume mmoja. Wema na Aunt ni marafiki, kwa hiyo hawana wivu. Hata kama ulikuwepo ila sasa umwekwisha. Na hii ndiyo tafsiri ya mapenzi ya Kichina. Mwendo wa kuzungukana, leo kwako, kesho kwa mwingine.

Akina Wema, Jokate na Diamond, kwao inakuwa rahisi kujulikana kutokana na umaarufu wao. Waandishi wa habari wanawafuatilia kila kona, hivyo wanaripotiwa na jamii inajua nyendo zao. Kundi hilo ndilo linatajwa kwamba wahusika wake hawajatulia.

Hata hivyo, upo ukweli uliotimia kuwa mitaani kwa jamii ya watu wa kawaida, wapo wachafu kuliko. Mwanamke mmoja anaweza kuwapanga wanaume watano kwa siku. Akitoka huyu anakwenda kwa mwingine. Anabadili nyumba za kulala wageni.

Huyu, hajitambulishi kama changudoa. Atasimama pembeni na kwamba yeye ni mtu mwenye heshima zake. Akiwaona machangudoa usiku wa manane wakiwa wamejipanga mawindoni na mavazi yao ya nusu uchi, atawalaani. Ni msemo wa nyani haoni makalioni kwake!

Huko nyuma nilishawahi kueleza mfano wa wanandoa kusaliti. Nikabainisha kwamba baadhi ya wanaume hufanya makosa pale wanapowakataza wanawake wao kufanya kazi. Eti wanataka wakae tu nyumbani. Hapa ndiyo kuna jambo, kwani mtu anapokaa bila kazi, hukaribisha hisia za karibu.

Hii ikanifanya nijenge hoja kutokana na muongozo wa kisaikolojia kwamba akina mama wa nyumbani, ni kundi hatari mno kusaliti ndoa. Mara nyingi wanakuwa hawapo bize, kwa hiyo hisia za kimapenzi zinakuwa karibu na matokeo yake hujikuta wakifanya zinaa na watu wa kushangaza.

Hujawahi kusikia mke wa mtu katembea na ‘houseboy’ wake? Vipi mwanamke kufanya zinaa na mdogo wa mume wake? Je, muuza bucha kujilia vyake nyakati za mchana kwa ofa za robo ya nyama anayomuongezea mke wa mtu aliyekwenda kununua kilo mbili? Hayo yapo kwenye mazingira yetu ya kila siku.

Kila siku wauza magenge na maduka, wanaingilia ndoa za watu. Nafasi hizo wanazipata kwa sababu ya kutokuwepo ubize kwa wanawake hao. Asili yetu tunapenda utani, hivyo wakitaniana mara mbili, mwanamke anahama kihisia. Keshokutwa asubuhi mume akiondoka, huyu anakimbilia gengeni.

Huu ni mfano katikati ya mada yetu. Mtu wa aina hii akiwaona machangudoa barabarani, atawalaani kupita kiasi. Hata hivyo, mtindo wa maisha yake hauna tofauti na changudoa kutokana na ukweli kwamba mtu mwenye staha na heshima, hawezi kujilimbikizia vidumu. Mume usiku, mchana muuza bucha au houseboy, haijakaa vizuri.

Hapa nifafanue kuwa yule ambaye anajiona yupo kwenye uhusiano salama, basi aendelee hapohapo kwa sababu ndipo kwenye bahati yake. Kwa wale wenye maumivu pale walipo, basi wajiangalie mara mbilimbili. Maisha yanaendelea. Maisha bora yanajengwa na mtu mwenye akili iliyotulia.

Huwezi kuwa na matatizo, akili haitulii kwa sababu ya misukosuko ya kimapenzi, ukadhani kwamba utajenga maisha imara. Hapo utakuwa unajidanganya. Tibu kwanza janga lako la mapenzi ili maisha yako yanyooke. Ikiwezekana, jipe muda wa kukaa ‘singo’. Inawezekana.

Beba zingatio kuwa lipo kundi la watu wanaowachezea wenzi wao lakini maisha yao ya kimapenzi bado ni imara. Japo anayetendwa ni maumivu kwake, ila mtendaji ni sawa tu. Haumii, anamnyanyapaa mwenzi wake na anaendelea kupendwa. Ni bahati tu.

Wewe unasaga miguu na kuumiza kichwa. Kila siku unajitahidi kumtafuta mwenzi bora wa maisha yako lakini hujampata. Badala ya furaha, unavuna machungu mtindo mmoja. Usijione una bahati mbaya, badala yake endelea kuitazama mbele kwa matumaini.

Huyo huelewani naye kwa sababu siyo wa bahati yako. Wako yupo na bahati mbaya hujamfikia. Jambo la kufanya si papara, kuwa mtulivu, utampata kwa urahisi. Ukijifanya bingwa wa kuwapanga na kuwapangua, hutafanikiwa, matokeo yake utampita na mwenzi bora wa maisha yako bila kujua.

Penda kutazama mifano kwa walio karibu yako. Je, wanaishi vipi na wenzi wao? Kama nao picha haziendi, tambua kwamba wanalazimishana. Watu wanaopenda, haiwezekani kila siku wakawa wanasumbuliwa na migogoro. Kuna mawili, moja litakuwa sahihi.

Mosi; wote hawapendani ila walijikuta wapo pamoja kwa mvuto wa tamaa za mwili, nao wakajidanganya ni mapenzi, hivyo wakawa pamoja. Pili; kama mosi haikuwa sahihi, basi itakuwa mmoja anapenda, mwingine analeta utani, hivyo kufanya misuguano isiyoisha.

Itaendelea wiki ijayo.