Sugu alivyofunika Dar Live
Gwiji wa Hip Hop, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Jumapili iliyopita aliweka kando uheshimiwa wake na kuthibitisha kwamba yeye ndiye baba wa muziki wa kizazi kipya nchini.
Sugu aliye Mbunge wa Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alipanda kwenye jukwaa linalopanda na kuteremka la Ukumbi wa Dar Live, Mbagala Zakhem, Dar es Salaam na kupiga shoo kali kwa zaidi ya saa moja.
Alithibitisha viwango vyake katika sauti na pumzi kwa kupiga ngoma mfululizo, hivyo kupagawisha maelfu ya watu waliohudhuria onesho hilo.















Tofauti na wanamuziki wengi nchini ambao wakipanda jukwaani, huimba juu ya wimbo (playback), Sugu yeye alikamua live juu ya beat.
Mashabiki muda wote waliimba naye, walimshangilia, hivyo kufikisha meseji kwamba Sugu ni mwana Hip Hop anayependwa zaidi, nyimbo zake zinabamba japo zimeadimika redioni.
Meseji nyingine iliyopatikana kwenye shoo hiyo ni kuwa nyimbo za Sugu hazichuji na kwa namna zilivyoonesha zinawabamba mashabiki, ni wazi zitachezeka hata miaka mia moja ijayo.
FEDHA ZAKE APELEKA MFUKO WA ELIMU
Mbele ya hadhira, Sugu alitimiza azma yake ya kukabidhi mapato yake ya shoo hiyo kwenye mfuko wa elimu aliouanzisha kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wasio na uwezo wa kulipa ada katika Jimbo la Mbeya Mjini.
Sugu, alimkabidhi katibu wa mfuko huo shilingi milioni mbili, huku mashuhuda wa onesho hilo wakishuhudia na kushangilia vilivyo.
Alisema, katika shoo hiyo iliyopewa jina la Usiku wa Sugu, alilipwa shilingi milioni tatu, alichokifanya alitoa shilingi milioni moja kuwawezesha wasanii wenzake wa crew ya Vinega ambao alishirikiana nao katika mradi wa Anti Virus na shilingi milioni mbili zote zikaingia kwenye mfuko wa elimu.
“Shilingi milioni moja, nimewapa machizi (Vinega) na milioni mbili zinakwenda mfuko wa elimu jimboni,” alisema Sugu huku akishangiliwa.
VINEGA, PROF. JAY NA JUMA NATURE
Mbali na Sugu, wakali wa mradi wa Anti Virus, Vinega kama Daniel Kamili ‘Dani Msimamo’, Fred Mariki ‘Mkoloni’, Suma G na Mapacha walipagawisha kwa zamu hadhira iliyokuwepo.
Kabla ya Vinega, wakongwe wa Hip Hop, Joseph Haule ‘Prof. Jay’ na Juma Kassim Kiroboto ‘Sir Nature’, walithibitisha nao kwamba wao ni keki jukwaani, kwani walipiga shoo kali na kushangiliwa kwa kiwango cha juu.
Click here for TUMA Registrations.