Bob Makani aagwa, kuzikwa Jumatano
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, jana aliungana na Watanzania wengine kuuaga mwili wa aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Kwanza wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mohamed Bob Makani katika Viwanja wa Karimjee jijini Dar es Salaam aliyefariki usiku wa kuamkia juzi katika Hospitali ya Agha Khan.

Viongozi wengine wa Serikali waliokuwepo ni Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad. Pia alikuwepo mama Anna Mkapa na mama Salma Kikwete.
Viongozi wa kitaifa wa Chadema, akiwemo Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Willibroad Slaa, Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Zitto Kabwe na wengineo, walihudhuria tukio hilo.
Mzee Makani, anatarajiwa kuzikwa kesho (Jumatano) mkoani Shinyanga katika mazishi ambayo pia yatahudhuriwa na baadhi ya viongozi wa kitaifa.
Mungu ailaze pema roho ya marehemu mzee Makani.