Pinda azungumzia kutekwa kwa Dk. Ulimboka
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema, kuna utata mkubwa kuhusu tukio la kutekwa na kujeruhiwa kwa kiongozi wa mgomo wa madaktari, Dk. Stephen Ulimboka, hivyo ameagiza uchunguzi ufanywe haraka sana.
Pinda amesema bungeni mjini Dodoma kuwa, Serikali imeshtushwa na tukio hilo kwa kuwa imekuwa ikishirikiana na Dk. Ulimboka katika mchakato wa kumaliza mgogoro kati yake na madaktari.

“Ndugu Ulimboka tumekuwa naye muda wote…kama ni Serikali mnafanya ili iweje…namtakia kila la heri apone haraka” amesema Pinda mjini Dodoma wakati akijibu maswali ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu.
Kwa mujibu wa Mbowe, Dk. Ulimboka, alitekwa, akateswa, kang’olewa meno na kucha. Ulimboka (35) anayeongoza mgomo wa madaktari nchini, alivamiwa na watu wasiojulikana, kutekwa na kujeruhiwa kwa kipigo usiku wa kuamkia jana.
Dk Ulimboka ambaye anaongoza mgomo huo ingawa yeye si mwajiriwa wa Serikali, alifikishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbuli, Dar es Salaam jana asubuhi baada ya kuokotwa eneo la Mabwepande wilayani Kinondoni akiwa amejeruhiwa Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Namala Mkopi, alidai Dk Ulimboka alitekwa juzi usiku na watu wasiojulikana na kupigwa na kung’olewa kucha na meno na hali yake ni mahututi.
Alidai Dk Ulimboka alizungumza kwa taabu alipofikishwa hospitalini ambapo alidai juzi jioni alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kama Abduel anayedaiwa kutoka Ikulu na alitaka kuzungumza naye kuhusu maendeleo ya madai ya madaktari.
“Alikubali kuonana na mtu huyo ambaye pia alikuwa akizungumza naye mara kwa mara na alikubaliana na wenzake asiende kuonana naye mwenyewe, aliongozana na rafiki yake Dk Deo hadi eneo walilopatana ambalo ni Kinondoni barabara ya Tunisia,” alisimulia Dk Mkopi.
Alidai Dk Ulimboka alisimulia kuwa akiwa katika eneo hilo pamoja na Abduel na Dk Deo, walitokea watu watatu; wawili wakiwa na silaha aina ya bastola na mmoja bunduki.
Kwa mujibu wa madai ya Dk Ulimboka, watu hao walianzisha vurugu na kuwataka wengine waondoke na kumchukua peke yake na kumuingiza kwenye gari nyeusi yenye namba zisizosajiliwa na kutokomea naye.
Kwa mujibu wa madai hayo, Dk Deo aliamua kuwasiliana na wenzake ambao walimtafuta kwenye vituo vyote vya Polisi bila mafanikio na kuishia kuandika maelezo ya tukio hilo katika Kituo Kikuu cha Polisi.
Dk Deo pia aliwasiliana na wanaharakati akiwemo Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC) Hellen Kijo-Bisimba.
Anadai alipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa ni msamaria kwamba amemuokota Dk Ulimboka akiwa hoi eneo la Mabwepande.
Inadaiwa Dk Deo aliwachukua wanaharakati hao hadi Kituo cha Polisi Bunju alikopelekwa Dk Ulimboka na kumchukua na kumkimbiza Muhimbili.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema, Dk Ulimboka alikuwa na rafiki yake aitwaye Dk. Deogratius Michael na watu wengine katika Klabu ya Leaders Kinondoni ambapo ghafla saa 5:30 usiku, walitokea watu watano wasiofahamika wakavamia klabu hiyo na kuwatishia na kuwataka walale chini.
“Dk Ulimboka na wateja wengine walilala chini kwa kuhofia madhara kwa kuwa watu hao walikuwa na kitu wanachohisi ni silaha na hatimaye watu hao walimchukua Dk Ulimboka na kusema kwamba walikuwa wakimhitaji yeye na kumuingiza katika gari aina ya Suzuki Escudo nyeusi ambayo haikuwa na namba za usajili,” alidai Kova.
Alidai wakati wakiwa njiani, watu hao walianza kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili wake na bila kusema wanataka nini kutoka kwake na walipofika maeneo ya Mwenge, walimvisha fulana nyeusi usoni na hakujua tena wanaelekea wapi huku wakiendelea kumpiga na mmoja wa watu hao akasema watamuua.
Kamanda Kova alidai ilipofika asubuhi, Dk Ulimboka alijikuta yupo msitu wa Mambwepande na alijivuta hadi barabarani na alikutwa na msamaria akiwa amefungwa kamba miguuni na mikononi.
Kwa mujibu wa Kamanda Kova, Dk Ulimboka alieleza kuwa gari yake aliiacha maeneo ya Leaders Club na watu hao waliuchukua ufunguo wake, nyaraka zake pamoja na fedha ambazo hakumbuki ni kiasi gani.
Kamanda Kova alisema ameunda jopo la wapelelezi wa fani mbalimbali chini ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na mlalamikaji mwenyewe na mashahidi walioona tukio hilo, ili uchunguzi wa shauri hilo ufanyike na kuwaomba raia wema kutoa ushirikiano ili matukio ya aina hiyo yasijirudie.
“Naamini kwamba watu wengi watakuwa wameguswa na tukio hili ila nawasihi watuache polisi tufanye upelelezi na waachane na minong’ono kwa kuwa sisi hatukuwa na ugomvi wowote na Dk Ulimboka wala madaktari… upelelezi utafanyika kwa makini na taarifa rasmi zitatolewa baadaye.” alisema.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi amesema Serikali haihusiki na imeshtushwa, imesikitishwa na inalaani kitendo cha kutekwa na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Ulimboka.