Music | Lifestyle+Fashion | Antivirus | Love+Relationships | Business+Politics | Sport | TUMA Registrations

You are here:   HomeSport
| + -

Sports News

Tuesday, 19 March 2013 06:31 Al News - Sports News
Print PDF

Sakata la TFF VS Fifa, wadau waipa dole serikali

Kufuatia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoa taarifa kuwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limetoa tishio la kuifungia Tanzania, kumekuwa na maoni tofauti kutoka kwa wadau ambapo asilimia kubwa wameshusha lawama zao kwa TFF.

Wakitoa maoni kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, wadau mbalimbali walisema kuwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga ndiye anayestahili lawama. Sehemu ya maoni hayo ilisomeka hivi:

Grayson John: “Tenga huo ni mpango wako na wenzio, Waziri Makalla nakuaminia, bora tufungiwe.” Amin Mandemla: “Watu wanaleta siasa kwenye mpira matokeo yake ndiyo haya, tuachieni huu msituharibie mbona michezo ipo mingi? Tenga yuko sahihi, wanasiasa wanataka kuwepo katika kila kitu.”

Petro Mponda: “Ni bora tufungiwe tu maana viongozi wa serikali wanatamani madaraka mpaka TFF.” John Stephen: “Majungu na uchawi, TFF wachawi wakubwa, serikali inawasaidia mambo kibao, leo wanatuletea uchaguzi wa kihuni kama watoto wadogo, wanaelekezwa wanalalama wanaingiliwa.”

 
Tuesday, 19 March 2013 04:40 Al News - Sports News
Print PDF

Wanachama Simba wamng’oa Rage

Wanachama wa Klabu ya Simba ya Dar es Salaam, leo wamefanya uamuzi mgumu kwa kumuondoa madarakani mwenyekiti wa sasa Ismail Aden Rage.

Simba, walikutana leo na kufanya mkutano wa dharura kwenye Hoteli ya Star Light, Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

Kabla ya kutoa uamuzi huo, wanachama walitoa maoni yao ambapo wengi waliushutumu uongozi wa Rage kwamba ni mbovu na hauisaidii timu.

Baada ya maoni hayo, kila mmoja akitoa dukuduku, wanachama hao kwa pamoja walikubaliana kuupumzisha uongozi wa Rage kwa maslahi ya klabu.

Uamuzi huo, ulienda sambamba na wanachama hao kukabidhi uongozi wa klabu hiyo kwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Rahma Al-Kharus ‘Malkia wa Nyuki’.

Vilevile, wanachama hao walimrudisha kundini, kiongozi aliyejiuzulu wadhifa wake, Zachary Hans Pope.

Wanachama hao wamesema wanatarajia kuitisha mkutano mkuu na kuwachagua viongozi wapya baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara inayoendelea ili kuepusha kuivuruga timu.

Pop ambaye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili, alijiuzulu hivi karibuni kwa maelezo kwamba haridhishwi na hali ya mambo ndani ya klabu.

Pamoja na Pop, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, naye alibwaga manyanga.

 
Monday, 18 March 2013 15:48 Al News - Sports News
Print PDF

Hiki ndiyo First 11 ya Azam iliyoiua BYC II jana

Klabu ya Azam FC, jana ilipiga hatua moja mbele kwenye Kombe la Shirikisho la Soka Barani Afrika (Caf) kwa kuichapa Klabu ya BYC II ya Liberia.

Azam, ilishinda 2-1 kwenye mchezo huo, uliofanyika kwenye Uwanja wa ATS, Monrovia, Liberia.

Kwa ushindi huo, sasa Azam imejiweka kwenye hatua nzuri zaidi ya kufuzu mzunguko wa tatu wa mashindano hayo.

Timu hizo, zitarudiana wiki mbili zijazo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Matokeo yoyote yale ambayo BYC itayapata ambayo yatakuwa chini ya ushindi wa mabao 2-0, yataibeba Azam kwenda mzunguko unaofuata.

Azam inahitaji sare ya aina yoyote na hata ikifungwa bao 1-0, bado itafuzu kutokana na faida ya mabao mawili ya ugenini ambayo jana iliyapata.

Hivyo basi, BYC inahitaji ushindi wa mabao 2-0 ili iweze kufuzu.

FIRST 11 YA AZAM ILIKUWA HIVI

1.Mwadini Ali

2.Himidi Mao

3.Waziri Salum

4.David Mwantika

5.Jockins Atudo

6.Michael Bolou

7.Kipre Tchetche

8.Ibrahim Mwaipopo

9.John Bocco

10.Humphrey Mieno

11.Mcha Khamisi

 
Wednesday, 06 March 2013 07:12 Al News - Sports News
Print PDF

Jini Kabula adata, ajiita Mrs. Yanga

Staa wa maigizo Bongo, Miriam Jolwa ‘Jini Kabula’ ni wazi amedata kwa mapenzi aliyonayo juu ya Klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Tanzania.

Kabula, kupitia akaunti yake ya mtandao wa watumia simu aina ya Blackberry, BBM, amejiandika kwa jina la Miriam Jolwa Mrs. Yanga.

Katikati ya majina Miriam Jolwa na Mrs. Yanga, Kablula ameweka alama ya kopa ambayo humaanisha upendo wa ndani ya moyo.

Mbali na hilo, uchunguzi unaonesha kwamba Kabula amekuwa akijitokeza mara kwa mara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kila Yanga inapocheza hususan kwenye mechi kubwakubwa.

Mrembo huyo, aliyejipatia umaarufu kupitia igizo la Jumba la Dhahabu, kila anapoingia uwanjani, huvaa uhalisia wa kuishabikia Yanga kwa kuvaa nguo zenye rangi ya njano na kijani.

Hivi karibuni, ilidaiwa Kabula anatoka kimapenzi na straika wa Yanga, Jerry Tegete, ingawa mwenyewe alikanusha kupitia akaunti yake ya BBM.

 
Tuesday, 05 March 2013 06:24 Al News - Sports News
Print PDF

Twitte aanza kuigharimu Yanga

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limefanya maamuzi magumu kwa klabu za Simba na Yanga, kwa kuzikata fedha za mapato yao, kisa kikiwa ni madeni ya wachezaji wao Mbuyu Twite (Yanga) na Paschal Ochieng (Simba).

TFF imeamua kuikata Simba kufuatia kuvunja mkataba na Ochieng na kumuacha solemba bila kumlipa, wakati Yanga inakatwa baada ya Twite kushindwa kurudisha fedha za usajili wake Msimbazi.

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema tayari wameshaanza kuzikata klabu hizo ikiwa ni kutekeleza hukumu iliyotolewa na Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji iliyo chini ya Alex Mgongolwa.

Angetile alisema tayari shirikisho limeshaanza kuzikata klabu hizo asilimia 38 ya mapato ya michezo ya Ligi Kuu Bara ambapo Yanga tayari imeshakatwa mara tatu kufidia dola 32,000 (Sh milioni 51.8) ambazo Twite anadaiwa na Simba.

“Tumeamua kufanya hivi kwa sababu klabu hizi zilishapewa kazi ya kumaliza masuala ya wachezaji hawa, lakini zikashindwa kutekeleza hilo, sasa tumeona sisi tuzikate katika fedha za mapato yao ya ligi.

“Kiasi tunachokata ni asilimia 38 katika kila mapato ya mechi zao za ligi, awali Yanga waligomea na kususia fedha lakini baada ya muda wakakubali na mpaka sasa tumeshawakata mara tatu na mchezo wa mwisho ni ule waliocheza na Kagera Sugar, hizi fedha tukishazikata tunaziwasilisha kwa wahusika,” alisema Osiah.

Akizungumzia upande wa Ochieng, Osiah alisema kuwa bado hawajaanza kuwakata, lakini wataanza kufanya hivyo kwenye michezo ijayo.

 

 
Monday, 04 March 2013 06:36 Al News - Sports News
Print PDF

TFF yamwangukia Waziri Mukangara

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema ipo haja kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kufikiria upya uamuzi wake wa kutengua usajili wa Katiba ya TFF ya mwaka 2012 na kutaka itumike ya mwaka 2006, kwani hautekelezeki.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mchana, mara baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema ni muhimu jambo hilo likaangaliwa upya kwa sababu athari zake ni mbaya, na pengine Dk. Mukangara hakushauriwa vizuri kabla ya kufanya uamuzi huo.

“Kamati ya Utendaji ya TFF haitaki kubishana na Mheshimiwa Waziri hata kidogo, ila tunaamini wakati anatamka haya hakufahamu madhara yake, athari zake na ugumu wa utekelezaji wake. Kwa waliomshauri hili, wamemshauri vibaya,” amesema Rais Tenga.

Amesema rai ya TFF kwa Waziri ni kuwaita ili wamweleze ni kitu gani wafanye kunusuru mpira wa miguu wa Tanzania, kwani wanaamini jambo hili litakwisha baada ya kumwelimisha hasa kutokana na ukweli kuwa kabla ya kufanya uamuzi huo hakuwasikiliza.

Katika mkutano huo, Rais Tenga alianza kwa kusema kuwa TFF inaiheshimu sana Serikali, hivyo inaheshimu maagizo yaliyotolewa na Waziri, lakini akaongeza kuwa TFF ina wajibu wa kutoa ufafanuzi juu ya maagizo hayo.

Amesema lengo la kuelezea historia ya TFF ilikotoka ni kubaini migongano ya maagizo hayo na taratibu za TFF ambazo kwa bahati mbaya zinasigana na maagizo hayo.

Rais Tenga amesema TFF ni chombo cha wanachama, ambapo wanachama wake ni vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu, na ina taratibu za kufanya uamuzi kwa mujibu wa Katiba yake na za wanachama wake ambazo zimeidhinishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema si TFF pekee, bali vyama vya nchi zote ambavyo vimeunganishwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), zinaheshimu na kufuata maagizo na miongozi ya shirikisho hilo la kimataifa la mpira wa miguu.

Rais Tenga amesema TFF haitakiwi kuingiliwa katika uongozi na uendeshaji wake, kwani jambo hilo likitokea rungu la FIFA litaiangukia TFF, na madhara yake ni makubwa. Miongozo ya FIFA inasisitiza uhuru wa wanachama wake katika uendeshaji shughuli za mpira wa miguu, na iko kwenye Katiba ya TFF.

“Sheria za nchi ndizo zilizozaa Katiba ya TFF. TFF ni chama kamili kinatakiwa kufanya uamuzi wake ili mradi uzingatie madhumuni ya kuanzishwa kwake. Leo TFF ikiacha mpira wa miguu na kuanza kujishughulisha na gofu, hapo Msajili ana haki ya kuingilia,” amesema Rais Tenga.

Kuhusu maagizo ya Waziri, Rais Tenga amesema kifungu cha 11 cha Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kinazungumzia usajili wa chama, na si marekebisho ya katiba, ingawa kanuni zinahusu marekebisho ambapo ameongeza kuwa uamuzi wa marekebisho ni wa Mkutano Mkuu na si Msajili.

“Ukienda kuomba viza, fomu unapewa na yule anayekupa viza. TFF tulipowasilisha marekebisho ya Katiba hatukupewa fomu. Msajili akasema sawa. Jambo la kujaza fomu si la TFF, ndiyo maana tunasema ipo haja ya jambo hili kufikiriwa upya.

“Usajili tayari umepita, kwamba Msajili hakutoa fomu, mwathirika anakuwaje TFF? Tunaona ni muhimu jambo hili likaangaliwa upya,” amesema Rais Tenga na kuongeza kuwa utaratibu wa kusajili Katiba ya 2006 ambayo ndiyo Waziri ameagiza itumike ulikuwa huo huo uliosajili Katiba ya 2012.

Akizungumzia historia ya TFF kutoka mikononi mwa BMT, Rais Tenga amesema ni zao za Katiba ya 2004 ambayo ilifanyiwa marekebisho ukumbini na kugongwa mhuri na Msajili hapo hapo na kuingia kwenye uchaguzi. Katiba hiyo ndiyo iliyoiondoa BMT kuisimamia TFF.

“Huko ndiko tulikotoka, si kwa kulazimishwa, bali kwa kupewa Katiba ya 2004. Katiba ina utaratibu mzima wa kufanya uamuzi. Maelekezo ya Waziri yamesahau huko tulikotoka siku nyingi. Uhalali wa marekebisho unatokana na ridhaa ya Mkutano Mkuu. Hiyo ni kwa mujibu wa Katiba yenyewe, hakuna nafasi ya BMT,” amesema.

Amesema katika maagizo ya Waziri, ameitaka TFF kufuata Katiba ya 2006 na kanuni za BMT, lakini Katiba hiyo hiyo ya 2006 haina nafasi ya BMT, na hata kama TFF ingetaka kutekeleza hilo haliwezekani.

“Kwa maagizo haya inaonekana Waziri kashauriwa vibaya. Tunajua hakuwepo katika nafasi hiyo (2004) wakati wa makubaliano kati ya Serikali na FIFA kuacha mpira wa miguu ujiendeshe wenyewe,” amesema Rais Tenga.

Pia amezungumzia umuhimu wa Katiba toleo la 2012, kwani kuna marekebisho mengi yalifanyika mwaka 2007, 2008, 2009 na 2011 ambapo ukiyafuta maana yake unakiweka pembeni Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), Bodi ya Wadhamini, wanachama wapya (mikoa), Bodi ya Ligi, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi, Leseni za Klabu na Kanuni za Fedha.

“Kwa uamuzi huu yote yaliyofanyika hayana maana. Waziri sidhani kama alikuwa anafahamu athari za maagizo yake. Kama angelijua asingefanya uamuzi huo. Si rahisi kurudi katika Katiba ya 2006. Hao wajumbe wa Katiba ya 2006 unawapata wapi? Maana yake hata vyama wanachama ni batili kwa vile vimerekebisha Katiba zao 2009 na 2010,” amesema Rais Tenga.

Amesema kwa Serikali kufuta, maana yake ni kutengua uamuzi wa TFF ambapo madhara yake ni nchi kufungiwa, ambapo timu za Taifa hazitacheza mpira, klabu hazitashiriki michuano ya kimataifa na wadhamini nao watakaa pembeni kwa vile hawawezi kudhamini timu ambazo hazishindani kimataifa.

“Dhana kwamba tukae tu tusicheze nje, ni dhana ya watu walio nje ya mpira wa miguu. Dhamira yetu ni kuhakikisha hatufungiwi. Waziri ametuagiza tupeleke barua FIFA kuwa ametengua marekebisho ya katiba. Hatupeleki hivyo, kwani hiyo ni Government interference, watatufungia.

“Nia yetu bado ni Waziri kutupa nafasi ya kutusikiliza,” amesema Rais Tenga na kuongeza kuwa kuhusu uchaguzi kwa vile FIFA wanakuja ombi la TFF kwa Waziri ni kuacha kwanza mchakato uendelee hadi ufike mwisho.

“FIFA wanakuja, tuwasubiri. Nilidhani utaratibu huo utaheshimika. Kama mtu wa mpira haitaki FIFA anataka nini? Ahadi yetu ni kuhakikisha watu wanapewa haki. Hiyo ndiyo ahadi yetu na tumeisimamia, na ndiyo maana FIFA wanakuja,” amesema.

Akijibu swali kuhusu waraka, Rais Tenga amesema marekebisho ya Katiba hayakufanywa kwa siri, ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu kufanya marekebisho hayo kwa njia ya waraka ilipatikana ambapo 70 waliunga mkono na 33 walikataa.

 
Monday, 04 March 2013 06:21 Al News - Sports News
Print PDF

Simba yapigwa 4, Azam yashinda 5

Hali ni mbaya ndani ya Klabu ya Simba ‘Wekundu wa Msimbazi’, baada ya leo kuchabangwa mabao 4-0 na timu ya Recreativo do Libolo FC ya Angola.

Kwa matokeo hayo, sasa Simba imeyaaga mashindano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika kwa jumla ya matokeo ya mabao 5-0.

Ikumbukwe kuwa Simba ilifungwa bao 1-0, wakati zilipokutana Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam takriban wiki mbili zilizopita.

Wakati Simba imelia, Azam FC yenyewe imefuzu hatua ya pili kwa kuiadhibu Klabu ya El Nasir ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 5-0.

Azam ilikuwa na kazi rahisi, kwani iliingia uwanjani ikiwa na ushindi wa mabao 3-1 ambao iliupata katika mechi ya kwanza iliyochezwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.

Kwa matokeo hayo sasa, Azam imeifungwa El Nasir kwa jumla ya mabao 8-1.

 
Sunday, 03 March 2013 07:42 Al News - Sports News
Print PDF

 

Wambura: Tenga ni tatizo TFF

Aliyekuwa mgombea wa nafasi ya makamu wa rais katika Uchaguzi Mkuu wa Shirikikisho la Soka Tanzania (TFF), Richard Wambura amemtaka Rais wa shirikisho hilo, Leodgar Tenga kuomba radhi kwa mabadiliko ya katiba aliyoyafanya, kwani tatizo kubwa ni yeye.

Wambura alisema, Tenga anatakiwa kuwaomba radhi Watanzania kufuatia kufanya mabadiliko ya katiba ya shirikisho hilo pasipo kufuata katiba.

Alisema, migogoro inayotokea sasa chanzo kikubwa ni Tenga ambaye ameshindwa kusimamia matumizi sahihi ya katiba na kumtaka kuwajibika kwa matatizo yoyote yatakayoweza kuikumba Tanzania endapo itaadhibiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

“Tenga aandike barua Fifa itakayolenga kuwataarifu kwamba hakuna migogoro kwani kuwaita Fifa kuja kuamua mgogoro wa Tanzania ni aibu kwa taifa.

“Haiwezekani Tanzania tukashindwa kusimamia uchaguzi wetu wenyewe huu ni uzembe wa watu wachache, sasa ni wakati kwa TFF kuridhia kutekeleza uamuzi wa serikali bila kigugumizi na baadaye itaje upya tarehe ya uchaguzi na wagombea wote walioenguliwa warudishwe,” alisema.

 

 
Sunday, 03 March 2013 07:21 Al News - Sports News
Print PDF

Azam: Tutashambulia mwanzo mwisho Sudan

Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall (pichani), ameweka wazi mpango wake wa kuhakikisha anaitoa El Nasir ya Sudan na kusema wanakwenda nchini humo kutafuta ushindi wa bao 1-0 wala siyo kuzuia katika mechi hiyo ya pili ya Kombe la Shirikisho itakayochezwa wikiendi hii.

Mpango huo wa Stewart unakuja kufuatia kikosi chake kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya El Nasir katika mchezo wa kwanza uliopigwa wiki mbili zilizopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini, ambapo sasa kikosi hicho kinatarajia kuondoka kesho asubuhi kwa Shirika la Ndege la Kenya kuwafuata Wasudani hao.

Stewart amesema katika mchezo wa marudiano dhidi ya Wasudani hao, kamwe hawatakwenda kujihami na kusema amefurahi kuona mshambuliaji wake, John Bocco, akirudi rasmi ambapo anategemea atakisaidia kikosi hicho katika kuongoza mashambulizi.

Wakati huohuo, Kocha Msaidizi wa Azam, Kali Ongala, amesema baada ya maandalizi mazuri, kikosi kinachoelekea Sudan kitakuwa na jumla ya wachezaji 20.

Kikosi hicho kitaondoka kesho kuelekea Sudan Kusini kikiwa na wachezaji 20 lakini viungo Uhuru Suleiman na Abdulhalim Humud wakiachwa katika msafara huo kutokana na kukabiliwa na matatizo binafsi ya kifamilia.

 
Sunday, 03 March 2013 07:17 Al News - Sports News
Print PDF

Simba waahidiwa donge nono wakiifunga Libolo

Timu ya Simba imetangaza majina 18 ya wachezaji waliotarajiwa kwenda nchini Angola, leo asubuhi kwa ajili ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Recreativo do Libolo, utakaochezwa keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Calulo.

Tayari uongozi wa klabu hiyo umetoa ahadi ya Sh milioni 10 kwa wachezaji hao iwapo watashinda na kuitoa Libolo katika michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga, amethibitisha.

Katika safari hiyo pia Simba itaongozana na benchi la ufundi pamoja na viongozi ambao jumla yao watakuwa saba.

Wachezaji hao ni: Juma Kaseja, Abel Dhaira, Shomari Kapombe, Komambil Keita, Said Nassor ‘Chollo’, Juma Nyosso na Amri Kiemba.

Wengine ni Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi ‘Boban, Mrisho Ngassa, Abdallah Juma, Felix Sunzu, Abdallah Seseme, Haruna Chanongo, Amir Maftah, Kigi Makassy na Salim Kinje.

 

Page 2 of 26

<< Start < Prev 1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 Next > End >>