Music | Lifestyle+Fashion | Antivirus | Love+Relationships | Business+Politics | Sport | TUMA Registrations

You are here:   HomeSport
| + -

Sports News

Wednesday, 24 April 2013 19:39 Al News - Sports News
Print PDF

Barthez njiapanda Taifa Stars

KOCHA Mkuu Taifa Stars, Kim Poulsen ametangaza kikosi cha pili cha timu ya taifa, Taifa Stars, ambacho atakitumia kuangalia wachezaji anaoweza kuwaita kwenye kikosi cha kwanza huku jina la kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’ likiwemo na mchezaji kutoka England.

Akizungumza kabla ya kutaja kikosi hicho jana, Kim alisema hiyo ni sehemu ya Mpango wa Maendeleo wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) uliozinduliwa Aprili 4, 2013.

Amesema timu hiyo inajumuisha wachezaji ambao wamepita umri wa kuchezea timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, lakini hawajapata nafasi ya kucheza Taifa Stars.

“Leo (jana) ninatangaza timu ya pili ya Stars ambayo inaundwa na wachezaji wengi vijana wa umri chini ya miaka 20 na wachache ambao hawajapata nafasi ya kuichezea ile ya kikosi cha kwanza.

“Tofauti na vijana hao, pia nimeita wakongwe kama Barthez, Barnabas (Vicent) na David Mwantika kwa ajili ya kuwaangalia uwezo wao zaidi na kama nikiona wanafaa nitawapandisha kwenye timu ya kwanza,” alisema Kim.

Wachezaji walioitwa wataingia kambini Mei 2 hadi 6, mwaka huu. Walioitwa ni; Aishi Manula (Azam), Hussein Shariff (Mtibwa Sugar) ambao ni makipa. Mabeki ni Kessy Hassan (Mtibwa Sugar), Kennan Ngoma (Barnsley FC, Uingereza), Himid Mao (Azam), Ismail Gambo (Azam), David Mwantika (Azam), Miraji Adam (Simba), Mohamed Hussein (Kagera Sugar), Waziri Salum (Azam), Samih Nuhu (Azam) na Emily Mgeta (Simba).

Viungo ni; Haruna Chanongo, William Lucian, Jonas Mkude, Edward Christopher, Abdallah Seseme, Ramadhan Singano (wote Simba), Mudathiri Yahya (Azam), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Jimmy Shoji (JKT Ruvu), Farid Mussa (Azam) na Vicent Barnabas (Mtibwa Sugar).

Washambuliaji ni; Hussein Javu (Mtibwa Sugar), Jerome Lambele (Ashanti United), Zahoro Pazi (JKT Ruvu), Twaha Hussein (Coastal Union), Abdallah Karihe (Azam) na Juma Luizio (Mtibwa Sugar) na Barthez.

 
Thursday, 18 April 2013 06:38 Al News - Sports News
Print PDF

Niyonzima atoa masharti kabla ya kusaini Yanga

Baada ya kukubali kusaini mkataba na Klabu ya Yanga, kiungo mchezeshaji Haruna Niyonzima sasa ametoa masharti mazito kwa viongozi wa timu hiyo ili amwage wino.

Hivi karibuni Niyonzima alisema kuwa yupo tayari kuongeza mkataba wake Yanga unaotarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu. Mpaka sasa yupo kwenye mazungumzo na viongozi wa timu hiyo.

Niyonzima, raia wa Rwanda, amesema kuwa, amewapa viongozi wa timu hiyo masharti ili aendelee kuichezea klabu hiyo na kama wasipoyatekeleza hawezi kuongeza mkataba.

Hata hivyo, kiungo huyo aliyetawala safu ya kiungo ya Yanga, amekataa kuyataja masharti hayo, akidai atakuwa tayari kulizungumzia suala hilo baada ya ligi kumalizika.

“Nipo kwenye mazungumzo na viongozi wa Yanga juu ya mkataba mpya. Bado sijasaini. Nimetoa masharti kwa viongozi hao ili nibaki. Nataka waboreshe baadhi ya mahitaji yangu yaliyoandikwa kwenye mkataba,” alisema Niyonzima.

 
Tuesday, 09 April 2013 06:14 Al News - Sports News
Print PDF

Super Sport kuing’arisha tena Ligi Kuu Bara

Kituo cha televisheni cha SuperSport cha Afrika Kusini kitaonesha moja kwa moja mechi sita za Ligi Kuu ya Vodacom katika Super Week kati ya Aprili 11 na Mei 18 mwaka huu.

Mechi hizo ni kati Azam na African Lyon itakayochezwa Aprili 11 mwaka huu badala ya Aprili 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam. Yanga na Oljoro JKT ambayo sasa itachezwa Aprili 13 mwaka huu badala ya Aprili 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Azam na Simba itakayochezwa Aprili 14 mwaka huu badala ya Aprili 13 mwaka huu Uwanja wa Taifa, na mechi kati ya Coastal Union na JKT Ruvu itakayochezwa Aprili 16 mwaka huu badala ya Aprili 10 mwaka huu.

Mechi nyingine ya Super Week itakayochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga ni kati ya Mgambo Shooting na Yanga itakayofanyika Aprili 17 mwaka huu badala ya Aprili 13 mwaka huu.

Pia mechi nyingine itakayooneshwa live na SuperSport ni kati ya Yanga na Simba itakayofanyika Mei 18 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kutokana na mechi za Super Week, mechi kati ya Mtibwa Sugar na Oljoro JKT iliyokuwa ichezwe Aprili 13 mwaka huu sasa itachezwa Aprili 17 mwaka huu Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.

 
Tuesday, 02 April 2013 21:29 Al News - Sports News
Print PDF

Uchawi wa Tiger Woods katika gofu watajwa

Stadi wa mchezo wa gofu duniani, Tiger Woods, amepigwa dongo kwamba uchawi wake upo kwenye mapenzi.

Woods ambaye hivi karibuni, alifanya mambo makubwa na kumpiku Rory Mcllroy, hivyo kukamata nafasi ya kwanza kwa ubora wa wacheza gofu duniani, amepondwa kwamba anapokuwa na migogoro ya kimapenzi anakuwa si mchezaji mzuri.

Chanzo cha habari, kililiambia gazeti moja la England: “Yupo kwenye maelewano mazuri sana na mpenzi wake mpya, Lindsey Vonn. Huyo ndiye amempa nguvu ya kufanya vizuri. Amemsaidia kutuliza kichwa, akili ikakaa sawa na alifanya vizuri.

“Alipogombana na mke wake, Elin Nordegren, wakapeana talaka baada ya Woods kupata kashfa ya usaliti wa ndoa, kila kitu kilionekana kama kimefika ukingoni upande wake. Alipoteza michezo, kichwa kilivurugika, hakuonesha ushindani wowote, mwisho akaporomoka.”

Kwa msisitizo, chanzo hicho kiliongeza: “Kabla ya michuano ya Arnold Palmer Invitational kuanza Machi mwaka huu, alitumia muda mwingi kukaa na Lindsey, kujiweka sawa kisaikolojia. Kama siyo mpenzi wake, angeharibu kwa mara nyingine.”

Kwa upande mwingine, wapo watu wanaoamini kuwa pamoja na maajabu ambayo Woods aliyaonesha kwenye michuano ya Arnold Palmer Invitational, ataporomoka kwa mara nyingine kwa sababu hakitapita kipindi kirefu kabla hajagombana na Lindsey.

Hata hivyo, Lindsey anamtetea Woods: “Tulishazungumza mengi, amekuwa muwazi kwangu kwa kila kitu. Sitarajii kama atarudia, watu wananishangaa mimi kuwa na Woods, wanaamini atanisaliti, siyo kweli. Woods ni binadamu.”

Woods, aliamua kujituliza kwa Lindsey, baada ya jitihada zake za kutaka kurudiana na Elin kugonga mwamba.

 
Tuesday, 02 April 2013 21:15 Al News - Sports News
Print PDF

Mwinyi Kazimoto achenguka na stori ya soka, bangi kuhusu Bob Marley

Kiungo wa Simba, Mwinyi Kazimoto, Jumamosi iliyopita, alionesha kuchenguka na simulizi ya bangi inayomhusu mfalme wa muziki wa Reggae duniani, Robert Nesta ‘Bob’ Marley.

Katika mtandao wa Twitter, mmoja watumiaji aliandika kuwa Bob Marley, alizikwa pamoja na mche wa bangi, kitu ambacho kilimfanya Kazimoto aijibu tweet hiyo kwa mshangao.

Kazimoto, akionesha wazi kuchenguka na stori hiyo ya mche wa bangi, aliandika: “Aah kweli!” akijibu tweet ya mtumiaji mwenye akaunti @UberFacts ambaye aliorodhesha vitu mbalimbali ambavyo Bob Marley alizikwa navyo.

Kwa mujibu wa tafsiri ya kile kilichoandikwa na @UberFacts, Bob Marley katika maisha yake, alionesha mapenzi makubwa kwa vitu kadhaa, hivyo ili kuvienzi, marafiki na familia yake, waliridhia azikwe navyo.

Mbali na bangi, vitu vingine ambavyo @UberFacts alieleza kuwa Bob Marley alizikwa navyo ni Biblia, mpira wa miguu na gitaa.

 
Wednesday, 27 March 2013 07:55 Al News - Sports News
Print PDF

Abramovich adaiwa kusababisha kifo cha mpinzani wake

Mmiliki wa Klabu ya Chelsea ya England, Roman Abramovich, ametupiwa skendo kwamba yeye ndiye sababu ya kifo cha mpinzani wake, Boris Berezovsky, aliyefikwa na mauti akiwa na umri wa miaka 67.

Berezovsky, aliyekutwa amefariki dunia, nyumbani kwake mjini Ascot, Berkshire, magharibi mwa Jiji la London, England, Jumamosi iliyopita, kifo chake kimezua utata mkubwa.

Tajiri huyo wa Kirusi, aliyekuwa akiishi uhamishoni England, moja ya sababu ya kifo chake imetajwa pengine amewekewa sumu lakini kubwa zaidi ni madai kwamba trilionea huyo kwa chenji ya madafu, alianza kupata wakati mgumu tangu alipopoteza mabilioni ya pauni, aliposhindwa kesi mahakamani na Abramovich.

Berezovsky, alimburuza Abramovich mahakamani, akimtaka amlipe fidia ya pauni bilioni 3 (shilingi trilioni 7.4), akidai alimdhulumu katika mgawo wa fedha kwa uwiano wa hisa, baada ya kuiuza kampuni ya mafuta ya Urusi, Sibneft.

Madai ya msingi kama yalivyowasilishwa mahakamani na Berezovsky, yalisema: “Abramovich kwa kutambua haki na wingi wa hisa za Berezovsky, hakutenda haki na kumpa gawio dogo baada ya Abramovich kuiza Kampuni ya Sibneft.”

Hata hivyo, baada ya kusikiliza kesi hiyo, Abramovich alimbwaga Berezovsky, hivyo Jaji wa Mahakama ya Biashara, Uingereza, Dame Elizabeth Gloster ‘Lady Popplewell’, aliagiza Berezovsky amlipe Abramovich gharama zote za uendeshaji wa kesi.

Berezovsky, alikubali kumlipa Abramovich fidia ya pauni milioni 35 (shilingi bilioni 86) ingawa taarifa ilitolewa baadaye kuwa alitakiwa kulipa pauni milioni 100 (shilingi 246).

Tangu kushindwa kesi hiyo mwaka jana, Berezovsky alianza kunyong’onyea, muda mwingi akiwa na msongo wa mawazo kabla ya Jumamosi iliyopita kukutwa amefariki dunia nyumbani kwake.

“Kama siyo sumu basi pigo alilopata kutoka kwa Abramovich ndiyo limesababisha. Sibneft ilipouzwa aliathirika sana kwa mgawo aliopata kutokana na hisa nyingi alizokuwa nazo, aliposhindwa kesi, alizidi kunyong’onyea.

“Kwa pamoja, Abramovich na Rais wa Urusi, Vladimir Putin wameharakisha kifo cha Berezovsky kwa sababu aliondoka Urusi na kuishi uhamishoni England kwa sababu ya tofauti zake na Putin.

“Alipoteza mali na fedha nyingi alipohamia England, Abramovich akazidi kumuumiza alipoiuza Sibneft na fidia ya kesi aliyotakiwa kumlipa,” kilisema chanzo.

Msemaji wa kampuni ya Berezovsky, Bell Pottinger, alisema: “Mwili wa marehemu uligunduliwa na bodigadi wake. Hakuna taarifa zaidi ya hizo mpaka wakati huu.”

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, Berezovsky mpaka anakumbwa na mauti, alikuwa na utajiri wenye thamani ya pauni bilioni 5 (shilingi trilioni 12) na inaelezwa angekuwa mbali ya hapo kama asingekutana na misukosuko na serikali yake ya Urusi pamoja na mgogoro dhidi ya Abramovich.

 
Monday, 25 March 2013 05:06 Al News - Sports News
Print PDF

Taifa Stars yaiduwaza Morocco, yaichapa 3-1

Leo ilikuwa raha kwa kila Mtanzania pale Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ilipowachabanga Simba wa Milima ya Atlas, Timu ya Taifa ya Morocco mabao 3-1.

Straika bei mbaya wa Tanzania, anayeichezea Klabu ya TP Mazembe ya DRC, aliwafundisha adabu Morocco, kwani aliweza kutupia mabao mawili kimiani.

Tanzania ilinogeshwa na zawadi kutoka DRC, kwani janki mwingine anayeichezea TP Mazembe, Thomas Ulimwengu, alifanya kweli pale alipotupia bao la tatu.

Kwa hali halisi, Stars leo imeonyesha maajabu na kuwaduwaza Waarabu wa Morocco, kwa kuchapo hicho kitamu cha mabao 3-1 ndani ya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Awali Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilipanga mchezo huo uanze saa tisa kamili ili kuwawezesha wachezaji wa Stars wafanye vizuri kutokana na wao kulizoea zaidi jua na joto kali, ambapo ilihisiwa kwamba kwa staili hiyo, itakuwa rahisi kuwaweza Waarabu.

Iliaminika kuwa Morocco wao wamezoea kuchezea katika mazingira yasiyo na jua, hivyo jua la Dar es Salaam la saa 9 alasiri, lingeisaudia Stars.

Hata hivyo, mabadiliko ya hali ya hewa yaliyoikumba Dar leo, mvua ikianza kunyesha kuanzia asubuhi, ilizua hofu kwamba itakuwa vigumu kwa Stars kuwaadhibu Morocco lakini mpaka kipyenga cha mwisho kinapulizwa, Waarabu walikuwa wameshatota 3-1.

Mabao yote yalifungwa kipindi cha pili, huku lile la Morocco la kufutia machozi, likitumbukizwa mnamo dakika ya 90 ya mchezo.

 
Friday, 22 March 2013 06:25 Al News - Sports News
Print PDF

Morocco kuwasili kesho kuivaa Stars

Timu ya Taifa ya Morocco (Lions of the Atlas) inatarajiwa kuwasili nchini kesho (Ijumaa) kwa ndege ya Emirates tayari kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, itakayochezwa Jumapili katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Msafara wa timu hiyo yenye watu 58 wakiwemo maofisa 19 na waandishi wa habari 12, utawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 8.55 mchana na utafikia hoteli ya Kilimanjaro Hyatt Regency.

Siku hiyo, Morocco inatarajiwa kufanya mazoezi jioni kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, na Jumamosi itafanya mazoezi yake ya mwisho kwenye Uwanja wa Taifa kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa saa 9 kamili alasiri.

Wachezaji walioko kwenye kikosi hicho chini ya Kocha Rachid Taoussi ni Nadir Lamyaghri, Anas Zniti, Yassine Bounou, Younnes Bellakhadar, Abdellatif Noussair, Abderrahim Achchakir, Zoheir Feddal, Younnes Hammal, Zakarya Bergdich na Abdeljalil Jbira.

Wengine ni Issam El Adou, Kamel Chafni, Salaheddine Saidi, Mohamed Ali Bamaamar, Abdelaziz Barrada, Salaheddine Aqqal, Abdessamad El Moubarky, Nordin Amrabat, Chahir Belghazouani, Abdelilah Hafidi, Youssef Kaddioui, Brahim El Bahri, Hamza Abourazzouk na Youssef El Arabi.

Wakati huo huo, tiketi kwa ajili ya mechi hiyo zitaanza kuuzwa kesho katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Uwanja wa Taifa na Dar Live Mbagala.

Milango siku ya mechi kwa ajili ya watazamaji itafunguliwa saa 6 kamili mchana.

 

 
Tuesday, 19 March 2013 07:32 Al News - Sports News
Print PDF

Ngassa aiaga rasmi Simba

Kiungo mshmbuliaji wa Simba SC, Mrisho Ngassa, ameiaga rasmi timu hiyo.

Nyota huyo alijiunga na timu hiyo kwa mkopo katika usajili mkubwa uliopita kabla ya kuanza kwa msimu huu.

Ngassa amesema, hafikirii kuongeza mkataba mwingine mpya wa kuichezea timu hiyo inayoshikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na pointi 34.

Ngassa alisema amefikia uamuzi huo kutokana na viongozi wa timu hiyo kujiuzulu huku kukiwa na malumbano mbalimbali kwenye klabu hiyo.

Alisema mkataba wake unatarajiwa kumalizika Mei 30, mwaka huu, mara baada ya kumalizika kwa msimu wa ligi kuu, Mei 18.

“Kiukweli kabisa sifikirii na sina mpango wa kuongeza mkataba mwingine wa kuichezea Simba msimu ujao.

“Huo ndiyo ukweli wenyewe, kama viongozi wanalumbana na wanajiuzulu iweje mimi ning’ang’anie kubaki kuichezea Simba?

“Mkataba wangu unatarajiwa kumalizika Mei 30, mwaka huu ikiwa na maana baada ya msimu huu wa ligi kumalizika nitakuwa huru kwenda kusajiliwa timu yoyote, ni vyema wakajua hilo,” alisema Ngassa.

Kiungo huyo wakati anatoka uwanjani kwenye mechi ya jana dhidi ya Coastal Union, alionyesha mapenzi ya wazi kwa mashabiki wa Yanga baada ya kuwapigia makofi huku akiwapungia mikono.

Wakati gazeti hili linakwenda mtamboni, lilipata taarifa kuwa winga huyo tayari amemalizana na Yanga na wamemkabidhi gari aina ya Nissan X-Trail lenye thamani ya shilingi milioni 25, aliloondoka nalo Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam muda mchache baada ya mechi hiyo kumalizika.

Wakati anaondoka uwanjani hapo, mashabiki wa Simba walimzomea kwa kuamini tayari ameshakuwa mchezaji wa Yanga.

 

 
Tuesday, 19 March 2013 07:05 Al News - Sports News
Print PDF

Tevez achungulia jela

Straika wa Manchester City, Carlos Tevez anachungulia kifungo jela, kinachongojewa ni mahakama kusema kama Muargetina huyo ana hatia au la!

Tevez, 28, alikamatwa wiki iliyopita akiendesha gari, wakati yupo kwenye adhabu inayomkataza kufanya hivyo katika kipindi cha miezi sita.

Huku akifahamu kwamba alipewa adhabu na mahakama ya kutoendesha gari kwa miezi sita Januari mwaka huu, Tevez alikamatwa barabarani mjini Alderley Edge, Cheshire, Ijumaa jioni.

Msemaji wa polisi kwenye Mji wa Cheshire, alisema: “Mnamo saa 11:13 (saa za Uingereza), Ijuma iliyopita, tulimkamata mwanaume mwenye umri wa miaka 28.”

Baadaye ilibainishwa kuwa mwanaume huyo ni Tevez na kwamba endapo atakutwa na hatia, mahakama haitakuwa na uamuzi mwingine zaidi ya kumfunga jela.

“Kwa sheria za hapa, mahakama itakapogundua Tevez amekiuka adhabu yake inayomkataza kutoendesha gari kwa miezi sita, itabidi afungwe jela,” kilisema chanzo cha habari, ingawa hakikufafanua kwamba anaweza kufungwa kwa kipindi gani kutokana na kosa hilo.

 

Page 1 of 26

<< Start < Prev 1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 Next > End >>