Siasa na ukosefu wa wawakilishi makini ni chanzo cha machafuko Mtwara
Nimeshawahi kuandika makala huko nyuma, nikitanabahisha kwamba siasa zinaipeleka nchi pabaya. Tupo kwenye kipindi kigumu sana. Hatuoni misimamo ya kitaifa, kila jambo lazima ligawe wapinzani na serikali.
Nilishangazwa sana na jinsi ambavyo baadhi ya wapinzani walivyokuwa wanaunga mkono vurugu za kidini. Bila kutafuna maneno, ukweli uliopo sasa ni kwamba wapinzani wanalazimisha mitaji ya kisiasa kwenye machafuko.


Hata kama ni kweli Waislam wana madai ya msingi, kivipi usiwaunge mkono wakati mwafaka, ukangoja kipindi ambacho Makanisa yanachomwa moto ndipo utoe tamko la kuhalalisha harakati za akina Issa Ponda?
Ni wazi kwamba tamko hilo lilimaanisha Waislam waendelee na kile walichokuwa wanakifanya. Kauli hizo, zilitaka Wakristo nao waamke kujibu mashambulizi, baada ya hapo taifa liyumbishwe na vita ya kiimani.
Ni kweli kwamba serikali imeshindwa kufanyia kazi madai ya Waislam lakini anayekwamisha hayo siyo Makanisa. Wanasiasa wanajua athari, ila kwa sababu malengo yao ni mtaji wa kisiasa, wakaunga mkono ili vurugu ziendelee.
Gesi Mtwara ni sakata lenye umaarufu mkubwa nchini kwa sasa. Unapolitazama kwa kina, unaweza kuona makosa ya serikali, vilevile udhaifu wa kukosekana wawakilishi makini, mwisho siasa zimesababisha vurugu.
Haiwezekani mkoa ukawa na wabunge pamoja na maadiwani, hata siku moja hawajawahi kuwa na kauli nzito za kuishinikiza serikali dhidi ya madai ya gesi, matokeo yake wanaibuka wananchi, wanaandama, machafuko yanaibuka, vifo vinatokea..
Ile wananchi kuandamana wenyewe, maana yake kuna mambo mawili, moja linaweza kuwa sahihi. Mosi, wawakilishi na wananchi wana mitazamo tofauti, pili, wawakilishi wamelala, sasa wananchi wameamua wenyewe kusimama mstari wa mbele kudai kile wanachoamini ni haki yao.
Kama wawakilishi wanakubaliana na serikali, maana yake kuna tafsiri mbili, moja ndiyo ukweli. Mosi, wawakilishi wameshindwa kufanya kazi ya kuwaelimisha wananchi, pili, wawakilishi wamekubaliana na serikali kinyume na matakwa ya wananchi.
Kabla ya wananchi kuandamana, hatukuwahi hata mara moja kuona wabunge au misimamo ya madiwani katika Halmashauri za Mtwara, wakisimamisha mishipa kupinga gesi kusafirishwa kutoka mkoa huo.
Maana yake wananchi Mtwara wameamua kujisemea wenyewe, wamewaweka kando wawakilishi wao. Wamewaona maadui, kwa hiyo wakaamua kuwachomea moto nyumba zao. Ni aibu, mkuu mkoa, wabunge, wangejiuzulu ingefaa zaidi.
Vurugu za Mtwara, zitoe elimu kuwa Katiba Mpya inafaa kutamka kwamba wabunge hawapaswi kuwa mawaziri. Akina George Mkuchika na Hawa Ghasia inaonekana wanashindwa kufanya kazi ya uwakilishi ipasavyo, badala yake wanawajibika kwa serikali. Kosa kubwa.
Siasa; vyama vinaamini kuwa migogoro ya wananchi kama ilivyo Mtwara kwa sasa, kwao ni mtaji. Badala ya kujishughulisha kutoa elimu na kuwasaidia namna bora ya kudai haki bila machafuko, wao wanaunga mkono bila hata kuwapa tahadhari ya vurugu zao.
Serikali; bila shaka imeshajifunza wananchi wa Mtwara wanahitaji nini. Hivyo basi, inafaa kutumia busara za kidiplomasia kulimaliza hili jambo na amani irudi kwenye mkondo wake. Serikali inaposhindwa kuelewana na raia wake, hutoa picha kwamba inaongoza kiimla. Kwa Tanzania bado hatujafika huko.
Makala haya ni maoni ya mwandishi, siyo msimamo wa DeiwakaWorld.