Music | Lifestyle+Fashion | Antivirus | Love+Relationships | Business+Politics | Sport | TUMA Registrations

You are here:   HomeBusiness+Politics
| + -

Political Issues

Wednesday, 08 May 2013 03:41 Al News - Political Issues
Print PDF

Ukweli kamili kuhusu bomu lililotupwa kanisani Arusha

Kama tulikuwa tunasubiri dalili kubwa zaidi zijitokeze ndipo tutambue kwamba hali ya nchi inatisha, tukio la bomu kutupwa kanisani, likasababisha vifo na majeruhi, lipimwe kama ishara ya juu kabisa.

Pamoja na kila kinachosemwa kuzunguka tukio hilo, ukweli ni kwamba serikali ina kazi kubwa ya kufanya kutuliza mdudu hatari wa ubaguzi ambaye anaelekea kufanikiwa kuwagawa Watanzania kutokana na matukio ya aina hiyo.

Kudhihirisha hali ilivyo mbaya, maneno ya chuki ya kidini yalitawala jijini Arusha na katika mitandao ya kijamii kuzunguka nchi nzima, baadhi ya wakosoaji wakiwashutumu watu wa dini fulani kuhusika.

NI UGAIDI TU

Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasit, Arusha, lililipuliwa na bomu la mkono, Jumapili iliyopita, saa 4:30 asubuhi.

Iliripotiwa juzi (Jumapili) kuwa mmoja wa watuhumiwa wa tukio hilo, anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, mtu huyo alikamatwa muda mfupi baada ya msako dhidi ya washukiwa kuanza.

Kuhusu chanzo au sababu ya wahusika kufanya ulipuaji huo, bado ni siri nzito lakini Watanzania wameshauriwa kuwa watulivu, kwani hilo ni moja ya matukio ya kigaidi ambayo yanapenyezwa nchini kwa sasa.

“Sisi Watanzania tunajuana, hakuna Muislamu anayeweza kufanya shambulio dhidi ya Wakristo, kadhalika hakuna Mkristo anayeweza kufanya shambulio dhidi ya Waislamu, walipuaji ni magaidi, wakamatwe na washtakiwe kama magaidi.

“Haya maneno ya kusema watu wa dini moja wamewashambulia wa dini nyingine ni uchochezi mbaya na maneno ya aina hiyo yakiendelea yatatugawa Watanzania,” alisema Aminieli Moba, juzi, akiwa eneo la tukio, muda mfupi baada ya mlipuko.

Maneno ya Moba, hayapishani na ya Tito Hebrew, aliyeandika kwenye ukurasa wake wa Facebook: “Jamani hakuna udini, kuna chokochoko nyingi zinaibuliwa hapa. Watu walishataka kutugombanisha kwa njia za kisiasa wakashindwa.

“Kuna kipindi walijitahidi kutugombanisha kwa misingi ya ukabila ikawa ngumu, sasa hivi wanaamua kutumia njia za udini. Watanzania tunatakiwa tuutegue huu mtego, vinginevyo tutaingia kwenye vita ya sisi kwa sisi.”

TUKIO LENYEWE

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, akiwemo mtoto mdogo (wote tunawahifadhi), mwanaume aliyevalia koti kubwa lenye kofia, akiwa amejifunika usoni, alitokea upande wa kushoto wa kanisa hilo kwa mbele na kutupa bomu hilo.

“Nilikuwa nimesimama ghorofani, nikamwona mtu akiwa na koti la mvua akisogea mbele ya kanisa na kurusha kitu kilichotoa mlio mkubwa na baadaye watu walianza kulia kwa sauti ndiyo nikajua lilikuwa ni bomu,” alisema shuhuda mmoja.

Shuhuda mwingine alisema: “Yule mlipuaji alikuwa na mwenzake na walifika pale kanisani wakiwa na gari. Baada ya kurusha bomu, alirudi kwenye gari kisha wakakimbia.”

Hata hivyo, shuhuda huyo ambaye ni mtoto mdogo, hakuweza kufafanua gari hilo ni aina gani wala namba zake za usajili.

VIFO

Kwa mujibu taarifa za vifo mpaka sasa, watu watatu wamesharipotiwa kufariki dunia kutokana na tukio hilo.

Watu 70 walijeruhiwa katika shambulio hilo na wote walifikishwa kwenye Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru.

Waliojeruhiwa katika tukio hilo, wengi wao walionekana wakivuja damu nyingi, zilizolowanisha kabisa nguo zao.

Wengi wa waliojeruhiwa, walikatika viungo na wengine wamechanwachanwa, hivyo kuacha taharuki isiyomithilika.

MWAKILISHI WA PAPA CHUPUCHUPU

Mwakilishi wa Papa Francis I hapa nchini, Balozi Francisco Padilla, alinusurika kifo katika shambulio hilo.

Balozi Padilla aliyekuwa mgeni rasmi wa uzinduzi wa kanisa hilo, alikoswa na bomu, kwani lililipuliwa wakati akikamilisha ratiba za kubariki kanisa kabla ya kukata utepe, kuashiria mwanzo wa utoaji wa huduma za kikanisa.

Kanisa hilo ni jipya na ujenzi wake ulikamilika hivi karibuni, hivyo kugeuka gumzo kutokana, likitajwa kuwa moja ya makanisa yaliyojengwa kisasa kabisa ukanda wa Afrika Mashariki.

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu, pamoja na  mapadri zaidi ya 200, walihudhuria hafla hiyo ya uzinduzi wa kanisa hilo lakini wote wamenusurika.

NI MAAFA KATIKATI YA SHEREHE

Msemaji wa Kanisa Katoliki Parokia ya Olasit, Father Festus Mwangwangi, alisema kuwa sherehe za uzinduzi zilianza vizuri lakini mambo yaliharibika baadaye.

Alisema, kabla ya tukio hilo waumini wa kanisa hilo walianza maandamano kuanzia Kanisa Katoliki la Burka ambalo ni kanisa mama, wakiongozwa na Askofu Lebulu, na ilipofika saa 3.30 asubuhi, walifika katika kanisa hilo la Mtakatifu Joseph.

“Maandamano yalipokamilika, balozi wa Vatican (mwakilishi wa Papa), aliwasili katika msafara wake na mwenyeji wake ambaye ni Askofu Lebulu, kisha akamtembeza kulikagua kanisa hilo.

“Baada ya kulikagua kanisa, lilifuata tendo la kubariki maji ambayo yangechanganywa na chumvi kisha kutumika kulibariki kanisa lakini tukiwa kwenye hatua ya kubariki maji ndipo mlipuko mkubwa ulisikika,” alisema Father Mwangwangi.

UVUMI KUHUSU SIASA

Kwa upande mwingine, yapo madai yaliyopo mkoani Arusha kwamba bomu hilo pengine ni njama za wanasiasa.

Inadaiwa kuwa kuelekea uzinduzi wa kanisa hilo, kuna mmoja wa mawaziri wakuu wastaafu, alitajwa sana kuwa angekuwa mgeni rasmi.

“Pengine watu wabaya dhidi ya huyo mheshimiwa, waliamini huo uvumi, sasa wakaona hiyo ndiyo sehemu ya kutekeleza njama zao,” alisema mkazi mmoja wa Arusha, Philipo Abdiel.

LEMA AKOSOLEWA

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, alifika eneo la tukio muda mfupi baada ya bomu kulipuka na kutoa matamshi makali dhidi ya serikali na udini.

Hata hivyo, wananchi wa Arusha waliozungumza na ripota wetu, walisema kuwa wanamheshimu sana Lema na wanampenda kama mbunge wao lakini anakosea kuweka siasa katika tukio zito kama hilo la ugaidi.

“Kuna mambo akichanganya na siasa itakuwa sawa lakini siyo hili. Lema anatakiwa kushirikiana na serikali katika vita dhidi ya ugaidi ambao unapenyezwa nchini,” alisema Rosemina Kiwia, mkazi wa Ngarenaro, Arusha.

POLISI WANENA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema: “Uchunguzi makini utafanyika. Hapa tutawaleta wataalamu wa mabomu na baada ya uchunguzi ndipo tutatoa taarifa rasmi ya jeshi la polisi.”

MKUU WA MKOA

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, aliwataka wananchi kuwa watulivu wakati vyombo vya dola vikiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

“Polisi kutoka makao makuu ya jeshi pamoja na wataalamu wa mabomu kutoka makao makuu wanatarajiwa kufika katika eneo la tukio ili kuongeza nguvu,” alisema Mulongo.

KAULI KALI YA WAZIRI NCHIMBI

Jana, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema kuwa watu wanaoeneza chuki za kidini hawatavumiliwa, watachukuliwa hatua kali sana.

“Tunaendelea na uchunguzi wetu lakini kuanzia sasa, serikali haitawavumilia watu wanaoeneza chuki za kidini, tutawachukulia hatua kali ili iwe fundisho,” alisema Nchimbi.

JK ASITISHA SAFARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete, alikuwa kwenye ndege safarini kwenda Kuwait, wakati shambulio hilo la bomu lilipofanyika na lakini alipofika na kujulishwa kilichotokea, alisitisha ziara yake na kurudi nchini.

Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, alisema kuwa baada ya kupata taarifa hiyo, aliwasiliana na viongozi mbalimbali nchini kwa ajili ya kupata picha halisi ya tukio.

“Sasa hivi (jana mchana), yupo njiani, atafika Dar es Salaam halafu kesho (leo) asubuhi atakwenda Arusha,” alisema Rweyemamu.

WALIOKAMATWA

Mpaka sasa, watu wanane walishakamatwa, mmojawapo akiwa mtuhumiwa nambari moja, anayefahamika kwa jina la Victor Ambrose, 20.

Inaelezwa kuwa Ambrose, aliwataja wenzake watatu ambao nao walikamatwa.

Vilevile, raia wanne wa Saudi Arabia, walikamatwasiku ya tukio wakiwa safarini kuelekea Kenya, wakipitia mpaka wa Namanga.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ametoa taarifa bungeni leo kuwa raia wa Saudi Arabia, waliokamatwa ni kwa ajili ya upelelezi kama kweli wanaweza kuwa wanahusika au la!

“Mpaka kesho, itakuwa imeshajulikana kama kweli wale wanahusika au la,” alisema Pinda.

 

 
Friday, 03 May 2013 05:28 Al News - Political Issues
Print PDF

Nani fisadi yupi siyo, Usalama wa Taifa wakiamka nchi itanyooka

Idara ya Usalama wa Taifa ni nyeti. Hali ya ufisadi ilivyofikia sasa hivi, haiwezi kumalizwa na wanasiasa peke yao. Programu ya dharura inapaswa kuchukua nafasi na watekelezaji wake wanatakiwa wawe wazalendo kweli. Wenye tamaa wakae mbali, maana ndiyo wametufikisha hapa.

Pamoja na uwepo wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Usalama wa Taifa wanaweza kuwa msingi wa vita dhidi ya ufisadi. Kama wamelala katika eneo hili, wanapaswa kuamshwa, watambue kwamba maisha ya Watanzania yanahitaji nguvu na maarifa yao.

Watumishi wengi wa umma wanaishi maisha ya bandia. Wanafanya mambo makubwa tofauti kabisa na mishahara pamoja na marupurupu yao. Wanajenga majengo ya kutisha na kuendesha magari ya kufuru. Ajabu ni kwamba watu hao hawaguswi. Usalama wa Taifa mpo wapi?

Kama aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, aliandamwa kwa kununua nyumba ya shilingi milioni 650, ni kwa nini maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, hawafuatiliwi na hawachunguzwi? Kwa maana wanayoyafanya ni mazito.

Akaunti yake ina mabilioni ya shilingi, amezipataje? Amejenga nyumba yenye thamani ya shilingi bilioni tatu, amepata wapi fedha za kufanya hivyo? Anamiliki magari ya kifahari, ukijumlisha idadi yake na kuyapigia hesabu, yanaweza kugharimu zaidi ya shilingi bilioni moja.

Anatembea na wapambe siyo chini ya 10, anakutana nao kwenye hoteli zenye hadhi ya nyota tano, anawanunulia chakula, wanakula mpaka wanasaza, anawanywesha pombe hadi wanalewa tilalila. Kwa siku moja anaweza kutumia shilingi 2,000,000, kwa siku 10, milioni 20 zinakatika.

Mshahara wake na marupurupu vimekaaje? Maana pamoja na matumizi hayo, anawalipia kodi za nyumba wapambe ambao kazi yao kubwa ni kumtafutia tu wanawake. Hawana kazi, kwa hiyo anawapa mpaka fedha za matumizi ya kuendesha familia zao na starehe ndogondogo.

Hao wanawake, wenye bahati wanajengewa nyumba, wapo wanaonunuliwa zikiwa zimekamilika. Wengine wanapangiwa, vilevile kuna wanaoishia kupewa fedha. Kuhonga magari ndiyo usiseme, utadhani anayatengeneza yeye. Turudi kwenye swali la msingi, anapata wapi pesa?

Ofisa wa TRA, hata akiwa kamishna hana ubavu wa kufanya vurugu hizo. Lazima tu atakuwa anaiba. Wizi wenyewe ni uhuni wa ulipaji kodi. Wanakula na wakwepaji, na kwa sababu fedha zinakuwa za haramu, haoni hata woga wa kuzichezea, ndiyo maana anazitumia kama fimbo.

Tunawaona, wakali wa vita za kugombea wanawake. Wanashindana kuhonga vitu vya thamani ili kupata mapenzi (ngono). Siku zote mwizi akili yake huwa inalala, ukomo wa mawazo yake huishia katika kuiba na kutumia. Anaiba nyingi, anafanyaje sasa? Hii ndiyo sababu ya kufanya vurugu nyingi mitaani.

Nidhamu ya utumishi wa umma ni jambo ambalo linapaswa kusukwa upya. Wengi wanajiangalia wao peke yao. Usalama wa Taifa wakiamua, wanaweza kuchunguza aina ya watu ambao wanafaa kuwatumikia wananchi. Wezi, wenye tamaa, watapanya pesa hawatakiwi.

Inashindikana nini kwa Usalama wa Taifa kuchunguza mishahara ya watumishi wa umma lafu wakaoanisha na matumizi yao, kujua nani fisadi yupi siyo? Ni hesabu ndogo, tena ni kazi ambayo haihitaji hata siku 30. Wakifuatiliwa, ndani ya wiki moja watakuwa wameshabainika.

Inawezekana Usalama wa Taifa wanafuatilia mambo mengi kwa ajili ya kuhakikisha nchi ipo salama, hili la ufisadi katika kipengele cha mapato ya watumishi wa umma dhidi ya matumizi, wanawaachia Takukuru. Hapo ndipo wanapofanya makosa makubwa.

Takukuru wanafanya kazi kwa mtindo wa mazoea. Pale walipo, hawashughuliki na mtu mpaka wapewe taarifa kwamba mhusika amepokea au yupo kwenye harakati za kula/kutoa rushwa. Akifuatiliwa bila taarifa, hiyo ni janja ya maofisa fulani na wakishapozwa hunyamazwa kimya.

Tunataka watu wanaothubutu. Wale watakaosimama leo na kusema ufisadi ufike mwisho. Wenye uchungu na jasho la walalahoi. Walio na nia thabiti ya kumkomboa Mtanzania na hili janga la ugumu wa maisha. Usalala wa Taifa amkeni leo, tuanze mapambano ya mapato dhidi ya matumizi kwa watumishi wa umma, tutawanasa mafisadi wengi sana.

 
Tuesday, 23 April 2013 14:37 Al News - Political Issues
Print PDF

Komedi bungeni; bunge nyumba ya mipasho, ubabe

Je, ni sahihi kutumia mabilioni ya shilingi kufanya uchaguzi halafu wanaochaguliwa badala ya kufanya kazi ya nchi, wanakwenda kutukanana, kuoneshana ubabe, kushabikia vyama vyao? Kuna haja ya kufanya tathmini upya.

Je, fedha zinazotumika kuendesha bunge, zinazolipa mishahara wabunge na posho, kazi yake ndiyo hii ya kupigana mipasho na kukifanya chombo hicho muhimu cha kutunga sheria, kiwe mahsusi kwa ajili ya kuoneshana ubabe na ufundi wa kuzungumza maneno machafu ya mtaani?

Utovu wa nidhamu bungeni unazidi kushamiri. Taswira ya sasa, inasherehesha ukweli kwamba bunge limepungukiwa maadili. Na kwa vile wanaounda chombo hicho ni watu, wao ndiyo watovu wa maadili. Bunge makini linajengwa na wabunge makini na kinyume chake.

Yaani, bunge la sasa na matukio ya ‘komedi’ ambayo yanaendelea ni matokeo ya kuwa na wabunge wa aina hiyo. Na hayo ndiyo mazao ambayo tuliyapanda wakati wa uchaguzi. Ni utovu wa busara kutarajia kuvuna mpunga kwenye shamba ambalo wewe mwenyewe ulipanda matembele.

Ni ukweli kuwa yapo makosa ya wapigakura katika kile walichokipanda, yaani wakati wa kampeni hawakufanya kazi nzuri ya kuchagua mbegu bora, wao waliona bora mbegu. Hili linaweza kuwa fundisho kubwa sana katika uchaguzi wowote ujao. Tutajicheka mno tukirejea kasoro hizi.

Hata hivyo, kwa namna pana kabisa, wabunge wenyewe wanajidhalilisha. Kama hawana habari, basi ukweli ni kwamba mitaani kwetu wanawapuuza kwelikweli. Picha ambayo wanawatafsiri, hawawachukulii kama wawakilishi wa kweli, bali makada wa vyama vyao, walioamua kwenda kutetea maslahi yatokanayo na sera za vyama vyao.

Je, bungeni tumewapeleka wabunge kwenda kutetea maslahi ya vyama au kujenga taifa imara lenye maendeleo? Kwa mwendo wa sasa, ni vigumu sana kuona mijadala makini ikichukua nafasi kwa sababu fujo zinatawala. Jazba na hisia za kibinadamu zinawatawala na kuvuruda weledi.

Mbunge anaposimama na kusema “Sizungumzi na mbwa, nazungumza na mwenye mbwa”, huyo anakuwa ametoka nje ya maadili. Mwingine anapotukana kabisa, inasikitisha sana. Naomba niandike kwa msisitizo kuwa aibu iwe kwake Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba na tusi aliloliporomosha bungeni.

Serukamba alitukana lakini ni wengi tu ambao walizungumza lugha zisizo na staha. Imekuwa aibu kiasi ambacho, kuna tamko linatolewa kwamba wazazi wanawazuia watoto wao kutazama bunge kwa sababu wanaweza kujifunza lugha zisizofaa. Sijawahi kuona aibu nzito kama hii!

Kwa tafsiri ni kwamba bunge linaonekana ni X, kwa hiyo watu wenye umri chini ya miaka 18, hawatakiwi kabisa kutazama. Sidhani kama kuna fedheha nzito kuliko hii. Hatupaswi kuacha hili liendelee. Kwa maneno na vitendo, tunapaswa kuweka wazi hisia zetu kwa namna ambavyo tunachushwa na komedi za ndani ya bunge.

Unaangalia kikao cha bunge, Televisheni ya Taifa, inakwepesha kamera na baadaye kukatisha kurusha matangazo ili vioja vya ndani ya bunge visionekane. Nashindwa kusadiki kile nilichokuwa nakiamini sana huko nyuma kwamba wabunge ni watu daraja la juu kabisa ambao sauti zao ni ukombozi wa mwananchi.

Kwa maneno ni sawa lakini hali halisi kwa sasa ni tofauti. Tangu Bunge la Bajeti la mwaka wa fedha 2013-2014 lianze, kila siku malumbano. Spika wa Bunge, Anne Makinda anakemea leo, kesho mheshimiwa mwingine anarudia madudu yaleyale yaliyokatazwa. Huu ni zaidi ya utoto.

Mbunge hajaruhusiwa kuzungumza, akiwa ameketi anapaza sauti kupinga hoja ya mwenzake anayezungumza. Bunge linageuzwa soko, mazungumzo yanafanyika bila utaratibu, kila mteja na muuzaji wake, wanaelewana kivyao. Mtu anaitwa baba, tena kiongozi wa wananchi, mwakilishi lakini anafanya mambo ambayo wanafunzi wa shule za msingi wana afadhali.

Upande wa pili, kiongozi wa vikao anapozidiwa na hisia za kibinadamu ni hatari sana. Kila siku narudia kile kipande ambacho Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliamuru Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu aondolewe nje ya ukumbi Aprili 17, mwaka huu, napata shida mno.

Pengine Lissu ni mtukutu lakini siku ile alikosea nini? Aliomba mwongozo kama kanuni zinavyomtaka. Ndugai akachukizwa na hilo, akadai anasimamasimama sana. Mbona ilikuwa rahisi tu kumzimia ‘maikrofoni’ au kumwambia akae na kuzuia mwongozo mpaka aliyekuwa anazungumza amalize?

Hisia zilitawala na kupoka hekima na weledi, ubabe ukatawala ndiyo maana wabunge wengine wa Chadema, walisimama kuwazuia askari wasimtoe Lissu nje ya ukumbi. Je, hivyo ndivyo tunapaswa kwenda? Kuna makosa makubwa ya wabunge na baadhi ya viongozi wa vikao.

 
Thursday, 18 April 2013 06:14 Al News - Political Issues
Print PDF

Fast Jet: Hata mtu wa chini kabisa sasa anaweza kupanda ndege

Unaweza kutafuta kitu ambacho kinaweza kukufanya usisafiri na Fast Jet kwa sasa lakini ikashindikana. Hii ndiyo kampuni inayotoa huduma bora zaidi na nafuu za usafiri wa anga nchini.

Haina muda mrefu sana tangu ilipojikita kwenye ardhi ya Tanzania lakini ndani ya kipindi hicho kifupi, imeweza kuondoa ile dhana kuwa usafiri wa ndege ni kwa ajili ya watu wenye vipato vya juu.

Aprili 10, mwaka huu, mwanadishi wa makala haya, alisafiri na Fast Jet kati ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Zanzibar na kuzungumza na abiria 27 na kila mmoja alitoa maoni chanya, kuhusu mapinduzi makubwa yaliyofanywa katika Nyanja ya usafiri wa anga na kampuni hiyo ya ndege.

“Niliwahi kusafiri kwa ndege karibu miaka 17 iliyopita. Baada ya hapo sikuwahi kupanda ndege kabisa kwa maana niliona ni gharama kubwa ambazo sikuweza kuzimudu,” alisema Neyman Ndelijwa, 46, mkazi wa Arusha.

Neyman ambaye alikuwa kwenye ndege akitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia), akielekea Dar es Salaam, alimweleza mwandishi wa makala haya: “Sasa naweza kupanda ndege, Fast Jet wamerahisha sana maisha ya usafiri.

“Ukiangalia bei ambayo nimelipa, haitofautiani sana na gharama za kawaida za usafiri wa mabasi. Naamini kwamba hivi sasa kila anayesafiri kwa basi, anaweza kupanda ndege na ikawa nafuu zaidi kupitia Fast Jet.”

Anachokizungumza Neyman ni kweli kabisa, kwani mapinduzi ya sasa ya Fast Jet, yanafanya usafiri wa ndege kuwa gharama nafuu mno kupita hata basi.

Mathalan; kwa usafiri wa basi kwenda Mwanza, nauli ni kati ya shilingi 45,000 mpaka 60,000. Fast Jet yenyewe inatoza nauli ya chini kabisa shilingi 43,000, yaani usafiri shilingi 32,000 na kodi shilingi 11,000, jumla shilingi 43,000.

Vilevile unapopanda Fast Jet, haikulazimu kuingia gharama za ziada kwa ajili ya matumizi ya njiani. Kati ya dakika 45 na 60, unakuwa umeshafika unapokwenda.

Unaposafiri na basi, mbali na kutumia saa nyingi njiani, vilevile itakulazimu kununua chakula kuanzia asubuhi, mchana na wakati mwingine jioni, kwani unakuwa bado hujafika. Kwa kifupi, Fast Jet ni mkombozi wa kila Mtanzania.

Hakuna sababu ya kutumia saa nyingi njiani au wakati mwingine kupitisha zaidi ya siku ukisafiri, eti kwa kukimbia gharama za kusafiri kwa ndege, wakati Fast Jet inakusafirisha kwa bei nafuu kuliko hata ile ambayo ungelipa kwa basi.

Musika Nyangabo, 41, aliyekuwa anatokea JNIA kwenda Kia, alisema: “Fast Jet ni nafuu sana. Mimi na mtoto wangu tumeweza kusafiri kwenda na kurudi, Kilimanjaro – Dar kwa shilingi 282,000. Unadhani kama ingekuwa ni kwenye makampuni mengine hali ingekuwaje? Nafurahia bei na huduma za Fast Jet.”

NI HUDUMA KAMA ULAYA

“Ni mara yangu ya kwanza kuja Tanzania, Watanzania wana kila sababu ya kujivunia Fast Jet kwa sababu ni kampuni bora sana ya ndege,” alisema Okite Obakponovwe, 37, raia wa Nigeria ambaye alizungumza na mwandishi wa makala haya, akiwa angani kutoka Kia kwenda Julius Nyerere International Airport, Dar es Salaam.

Mnigeria huyo, aliyekuwa Kilimanjaro kwa ajili ya kutalii Mlima Kilimanjaro, aliongeza: “Fast Jet ni sawa na Kampuni ya Easy Jet ya Uingereza. Kila huduma inayotolewa na Fast Jet, inaendana na Easy Jet, kwa kifupi Tanzania imepata bahati kuliko nchi nyingine yeyote Afrika.

Obakponovwe ambaye alikuwa ameongozana na mkewe, Irene Okite, aliongeza: “Gharama ni nafuu sana. Hata kule Uingereza Easy Jet ni nafuu. Mimi na mke wangu, tumefurahia huduma za Fast Jet, tumeweza kusafiri vizuri na ndege zake zina uhakika wa safari na kufika salama kwa asilimia 100.”

Abiria wengine waliozungumza na mwandishi wa makala haya ni Faraja Temu, aliyewasili Uwanja wa Ndege wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Karume, Zanzibar akitokea Kilimanjaro, yeye alisema: “Nafurahia huduma, Fast Jet imerahisha maisha yetu ya usafiri hata kwetu sisi wanafunzi.”

NDEGE ZA AIRBUS BORA SANA

Mhudumu wa ndege, Jasmine Kaungu, alisema: “Nilishafanya kazi kwenye makampuni tofauti ya ndege hapa nchini, ila najisikia fahari kufanya kazi na Fast Jet. Abiria wanasafiri kwa uhakika sana kutokana na ndege zetu aina ya Airbus ambazo ni bora sana.”

Mmoja wa wasimamizi wa huduma kwa wateja, Omar Chinguile, alisema: “Kikubwa kwetu ni umakini. Menejimenti yetu ipo makini kuhakikisha wateja wanapata huduma bora sana. Ripoti yoyote inayoonesha uzembe, husababisha mfanyakazi apoteze ajira.”

BOOKING YA MAPEMA NI MUHIMU

Mkuu wa Oparesheni wa Fast Jet, Kia, Robert Kessy alisema: “Nashauri abiria wawe wanajitahidi kufanya booking mapema ili wapate bei ya chini kabisa ambayo ni shilingi 43,000. Wanapochelewa ndiyo hukutana na bei za juu. Kwa kawaida bei zetu zinaanzia shilingi 43,000 mpaka shilingi 300,000.”

CAPTION:

1. Abiria wakipanda ndege ya Fast Jet, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, wakielekea Kilimanjaro, Aprili 10, mwaka huu.

2. Abiria wakiwa ndani ya moja ya ndege za Fast Jet, iliyokuwa inatokea Dar es Salaam kwenda Kilimanjaro.

3. Okite Obakponovwe, raia wa Nigeria, akiwa ndani ya ndege ya Fast Jet, yeye alieleza kwamba huduma za Fast Jet ni bora sawa na zile za Easy Jet ya Uingereza.

4. Mkuu wa huduma za ndani ya ndege katika moja ya ndege za Fast Jet, Omar Chinguile (kushoto), akizungumza na mwanadishi wa habari na mmiliki wa Blogu ya Full Shangwe, John Bukuku, wakati wakiwa safarini kutoka Kilimanjaro kwenda Zanzibar, Aprili 10, mwaka huu.

5. Marubani wa Fast Jest, John Lewis (Kushoto) na Alex Taylor (katikati), wakiwa na mhudumu wa ndege, Jasmine Kaungu, muda mfupi kabla ya kuanza safari ya kutoka Kilimanjaro kwenda Zanzibar, Aprili 10, mwaka huu.

 
Thursday, 11 April 2013 11:04 Al News - Political Issues
Print PDF

Tunamchekea gavana Bot halafu tunalia kupanda kwa nauli

Mfumuko wa bei ni janga kubwa. Tafsiri yake tu inatosha kuonesha namna ambavyo hatupaswi kuuchekea. Kama taifa, tunateseka leo kwa sababu ya kushindwa kuudhibiti. Wananchi wa chini wanaangamia.

Maana yake ni kupanda kwa gharama za maisha. Bei za vitu na huduma muhimu za kijamii zinakuwa juu. Wakati mwingine ni matokeo ya kushuka thamani ya sarafu. Ulegevu wa benki kuu au udhaifu wa wizara ya fedha na uchumi katika usimamizi wa utekelezwaji wa bajeti, kwa tafsiri iliyooka, ndiyo kitovu cha tatizo.

Wiki iliyopita, Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), ilitangaza bei mpya ya nauli. Michango ya wengi, inaonesha kuwa ongezeko la gharama za usafiri siyo mwafaka, kwani ni nyundo nyingine kwa wananchi wa tabaka la chini.

Sumatra imetangaza kuwa sasa nauli zitapanda kwa asilimia 24.46 (kadiria asilimia 24.5), kwa hiyo mwananchi aliyekuwa anapanda daladala kwa shilingi 300, sasa atalipa shilingi 375 (kadiria 400). Msafiri wa kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine, aliyelipa shilingi 40,000, sasa atatakiwa alipe shilingi 50,000.

Ni mpanga bei anayepitiwa na msemo “mwenye shibe hamkumbuki aliye na njaa” ndiye peke yake anayeweza kuona bei hizi ni rahisi. Watanzania wanateseka, kuendelea kuwapandishia gharama za maisha ni kuzidi kuwaumiza na kuwakatisha tamaa.

Mfumuko wa bei ukiendelea kuitesa nchi, ajabu ni kwamba Gavana wa Bot, Benno Ndullu bado yupo palepale. Ufanisi wake hauonekani katika kuhakisha  benki kuu kama roho ya nchi, inafanya kile kinachotakiwa kuhakikisha gharama za vitu muhimu na huduma nyeti, hazipandi.

Taarifa kwamba mfumuko wa bei umefikia asilimia 20, inatoa picha kuwa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2012-2013, imepunguza uwezo wa kununua bidhaa na huduma kwa takribani asilimia 6. Hii ni sawa na shilingi trilioni moja kuyeyuka kabla hata mwaka mpya wa fedha haujafika.

Hali ni mbaya zaidi kwa wananchi, kwani mfumuko wa bei za vyakula umekua kwa kasi kikubwa mno. Ofisi ya Takwimu ilishaonesha kuwa mfumuko wa bei za chakula pekee umepaa kwa wastani wa asilimia 25. Upande huo kukiwa bado majanga, nauli nazo zinaongezeka.

Hata hivyo, ukiangalia kwa undani zaidi, utakuja kugundua kuwa bei za chakula zimekuwa maradufu, ukilinganisha na hali ilivyokuwa miaka miwili iliyopita. Mchele, sukari, nyama, samaki, sembe na ngano, vyote vimepanda kwa kati ya asilimia 30 mpaka 50.

Gesi ipo juu, mafuta ya taa yalishapanda kwa asilimia 71 mpaka 75 tangu miaka miwili iliyopita. Hii inasababisha wengi wakimbilie nishati ya mkaa ambayo ni hatari, ingawa nako huko ni pagumu kwa mwananchi wa kawaida, kwani umepanda kwa asilimia 30.

Mfumuko wa bei unasukuma Watanzania wengi zaidi kwenye dimbwi la umasikini, unapunguza uwezo wa serikali kutoa huduma za kijamii kupitia bajeti na hata kutimiza mipango ya miradi ya maendeleo kama miundombinu ya barabara, umeme, bomba la gesi, madaraja nk. Mkakati mahususi unatakiwa kubadili hali hii.

Kwa namna tunavyokwenda, kama tusipochukua hatua, kuna hatari ya dhahiri kwamba tunaweza kurejea mfumuko wa bei wa mwaka 1992 ambao ni asilimia 22, kadhalika tunaweza kuukaribia ule uliokuwa tishio zaidi, wa mwaka 1994, asilimia 33.

Kwa nini Ndullu anastahili lawama na kuwajibishwa kwa hili? Siku zote kuna njia mbili ambazo husimamiwa na benki kuu katika kudhibiti mfumuko wa bei. Mojawapo ni Monetary Measures, hii hugusa moja kwa moja sera kuhusu uchumi ndani ya benki kuu kwa kuweka riba kubwa dhidi ya mabenki ya kibiashara ili kuifanya serikali (hazina) kuwa na akiba nzuri.

Bot lazima isimamie sera ya riba ili kusababisha kupanda kwa gharama za kukopa dhidi ya mabenki ya kibiashara kutoka benki kuu. Matunda yake ni kupungua kwa mtiririko wa fedha kwa wananchi, hilo likifanikiwa serikali itaweza kupanga bei za bidhaa kulingana na hali za wananchi. Hivi sasa fedha zipo nje, wafanyabiashara wana hela sana, kwa hiyo inakuwa vigumu kuwadhibiti.

Mfumuko wa bei kwa tafsiri nyingine ni matokeo ya wafanyabiashara kuizidi nguvu serikali, kwa hiyo wanajipangia bei bila kupingwa. Ndullu kwa nafasi yake, anatakiwa kuhakikisha sera zinafanya kazi, serikali inakuwa na nguvu siku zote dhidi ya wafanyabiashara. Bot ikiendelea kusinzia, stori zitabaki zilezile.

 
Tuesday, 02 April 2013 21:32 Al News - Political Issues
Print PDF

Ukweli kamili ni huu

Jengo lenye urefu wa ghorofa 16, lililoanguka katikati ya Jiji la Dar es Salaam na kusababisha vifo, ulemavu wa watu pamoja na uharibifu wa mali, lilikuwa lazima lianguke.

Tathmini iliyoratibiwa kisayansi na ripota wa DeiwakaWorld, ikihusisha baadhi ya wataalamu wa majengo, inaonesha kwamba aina ya ujenzi wa jengo hilo, ulikuwa haukidhi hata kwa ghorofa tano.

Machi 29, mwaka huu (Ijumaa iliyopita), jengo hilo, lililopo kwenye makutano ya Barabara ya Morogoro na Mtaa wa Indira Ghandhi, lilianguka na kuibua wasiwasi mkubwa.

Kwa mujibu wa mhandisi wa majengo, Abel Kadali, anayemiliki kampuni yake, akiwa ni msomi mwenye shahada mbili, ujenzi wa jengo hilo, ulizungukwa na utani mwingi.

“Kwanza jengo refu kama lile linapokatika na kubomoka kisha eneo kugeuka kifusi kama hivi, maana yake ujenzi ulikuwa dhaifu kuanzia mwanzo hadi mwisho.

“Kama ujenzi ungekuwa mzuri, hili jengo hata kama lingeanguka, lisingesambaratika kama hivi. Hapa kuna kasoro za kiweledi. Ujenzi wa namna hii, huwa unatufanya tuonekane hatuwezi kazi,” alisema.

KASORO KATIKA SARUJI

Macho ya waandishi wetu yaliona lakini Kadali akafafanua kwamba ni kosa kubwa kujenga ghorofa, halafu ukabana saruji.

“Nikishika tofali, naona ni mchanga mtupu. Kwa kadirio la kitaalamu, inaonekana kila mfuko mmoja  wa saruji, ulitengeneza matofali 90. Maana ni mchanga mtupu.

“Kitaalam, ghorofa kama lile, angalau kadirio zuri la saruji na mchanga, ni matofali 20 kwa mfuko mmoja. Kwa hiyo kosa la kwanza kabisa ninaloweza kuliona hapa ni matumizi ya saruji,” alisema Kadali.

NONDO DHAIFU

Kadali alifafanua kuwa nondo zilizotumika siyo za kujengea ghorofa lenye urefu huo.

“Nikiziangalia hizi nondo, naona kabisa hili jengo lilijengwa chini ya kiwango kuanzia kwenye msingi wake mpaka hapo lilipofikia na kuanguka. Sasa ni kwa nini lisianguke?

“Tunacheza na maisha ya watu. Nondo ni nyembamba sana, nikiziangalia, zinaonesha kuwa pamoja na wembamba wake, hazina ubora,” alisema Kadali.

TATIZO LA MALIGHAFI

Kuhusu ubora wa nondo, Kadali alisema kuwa inashangaza kuona zikikunjwa zinakatika.

“Hili ni tatizo la malighafi, lazima ukaguzi wa kina ufanyike kwenye viwanda vyetu, kuona ubora wa bidhaa zinazotengenezwa.

“Ni kweli nondo ni nyembamba lakini ukweli usipindishwe kuwa hata ubora wenyewe haupo. Ina maana zilitengenezwa kwa malighafi zisizokidhi viwango.

“Viwanda vyetu vinaunda nondo kwa kuyeyusha vyuma chakavu. Ni kosa kubwa. Wakati mwingine inakuwa siyo vyuma peke yake, bali ni mchanganyiko na ‘Alminiamu’,” alisema Kadali na kuongeza:

“Kama nondo inatengenezwa kwa kuchanganya chuma na Alminiamu, unatarajia kweli kupata nondo imara? Ifahamike kwamba kila madini na kazi yake.”

KOSA LA TBS

Kadali alisema kuwa kiwango dhaifu cha nondo na bidhaa mbalimbali nchini, ni matokeo ya Shirika la Viwango Tanzania  (TBS) kutofanya kazi zake ipasavyo.

“Kuruhusu nondo kama zile kuingia sokoni na kuuzwa kwa ajili ya ujenzi, ni tatizo. TBS lazima wasimame imara kuhakikisha wanafanya kazi yao kisheria, hivyo kuokoa maisha ya Watanzania,” alisema Kadali.

KOSA LA NHC

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), nalo limeingia lawamani kwa sababu kisheria, lenyewe lina haki katika umiliki wa jengo hilo lililoanguka.

NHC, linamiliki asilimia 25 ya hisa za jengo hilo, hivyo kitendo cha kuacha ujenzi holela, siyo tu kwamba limeshindwa kutimiza wajibu wake, bali pia linachezea rasilimali za Watanzania.

WALIOKUFA NI 34

Mpaka zoezi la uokoaji linakamilika jana, maiti zilizokuwa zimepatikana ni 34.

Kati ya hao, watu wazima ni 30, watoto wawili na vichwa viwili, huku viwiliwili havikuweza kupatikana.

Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema: “Uokoaji bado unaendelea, vyombo vyote vya dola vipo, pamoja na zana zote.”

WANANE WAKAMATWA

Kova alisema: “Mpaka sasa, polisi kanda maalum imeshawakamata watu wanane kuhusiana na kuanguka kwa ghorofa hilo.

“Waliokamatwa ndiyo waliohusika moja kwa moja, kuanzia michoro mpaka ujenzi. Kwa sasa nisingependa kuwataja majina kwa sababu uchunguzi unaendelea,” alisema Kova.

Kwa upande mwingine, Kova alisema: “Kipindi hiki tunaendelea na uokoaji, hatutarajii kupata majeruhi. Tunachofanya ni kuhakikisha tunapata maiti wote ili waweze kuzikwa kwa heshima zote kama binadamu.”

KUHUSU JENGO PACHA

Habari zinasema kuwa jengo hilo lililoanguka, lilikuwa na pacha wake, jirani kabisa na ilipo Hospitali ya Burhani. Kova amesema kuwa ujenzi wake umesimamishwa mara moja.

“Tuligundua kuwa mmiliki na mjenzi ni yuleyule, kwa hiyo tumechukua hatua za haraka sana kuzuia shughuli zote za ujenzi wa jengo hilo pacha,” alisema Kova.

 
Thursday, 28 March 2013 11:52 Al News - Political Issues
Print PDF

Mbunge wa CUF afariki dunia

Mbunge wa Chambani kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Salum Hemed Khamis, amefariki dunia.

Maradhi yaliyochukua uhai wa Khamis hayajawekwa wazi ila inafahamika kwamba mbunge huyo alianguka ghafla jana akiwa ofisi za Bunge na kukimbizwa Hospitali ya Taifa, Muhimbili kwa matibabu.

Mpaka anafikwa na mauti, Khamis alikuwa Muhimbili akiendelea kupewa matibabu ya kuokoa maisha yake.

Khamis, alikuwa kwenye ofisi hizo kwa ajili ya kushiriki vikao vya kamati za bunge, vinavyoendelea hivi sasa, ikiwa ni maandalizi ya kikao kijacho cha bunge, kinachotarajiwa kuanza Aprili, mwaka huu.

Kuhusu wasifu za marehemu, historia yake pamoja na taratibu za mazishi, tutawaletea kadiri tutakapokuwa tunapata taarifa zaidi.

Mungu ailaze pema roho ya marehemu, Amiin.

Sisi wote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake lazima tutarejea.

 
Thursday, 28 March 2013 08:27 Al News - Political Issues
Print PDF

Ukweli na uongo sakata la Zitto kutaka kuuawa Chadema

Gazeti la Mtanzania, jana liliandika habari kwamba Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, alipangiwa njama za kuuawa.

HABARI YENYEWE IPO HIVI;

Tishio la kuuawa kwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, sasa limechukua sura mpya, baada ya kuibuika kwa madai mapya kuwa Bosi wake, Dk. Willbrod Slaa, alipanga njama za kumuangamiza, MTANZANIA Jumatano linaripoti.

Duru za habari zinaeleza kuwa Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Kiongozi wa Upinzani bungeni, anadaiwa alitaka kuuawa kwa sumu na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Slaa, ambaye alimtumia kada na Mjumbe wa Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA), Ben Saanane, kutekeleza mpango huo.

Habari zinadai kuwa tukio hilo lilipangwa kutekelezwa Mei mwaka jana, katika Hoteli ya Lunch Time, iliyoko Mabibo External, jijini Dar es Salaam.

Kwamba Zitto alilengwa kuuawa kwa kuwekewa sumu kwenye kinywaji chake wakati akiwa kwenye mazungumzo na baadhi ya makada vijana wa chama hicho katika Hoteli ya Lunch Time.

Mmoja wa watu waliokuwa katika tukio hilo amelieleza MTANZANIA Jumatano kuwa Zitto alinusurika baada ya aliyetumwa kumuwekea sumu hiyo kuidondosha na hivyo kuonekana kwa watu waliokuwa eneo hilo.

Anamtaja mtu aliyetumwa kumuua Zitto kuwa ni Ben Saanane, ambaye aliangusha karatasi ya nailoni iliyokuwa na ungaunga unaosadikiwa kuwa sumu na kuonekana kwa watu waliokuwa eneo hilo, akiwemo Zitto mwenyewe pamoja na aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wa Bavicha, Juliana Shonza na Mtela Mwampamba.

Akizungumza na MTANZANIA Jumatano, Shonza alikiri kutokea kwa tukio hilo kwa kueleza kuwa yeye na Mwampamba walihoji kilichokuwa ndani ya nailoni ile, ambacho kilionekana wazi kuwa ni unga unga ni nini, ambapo Saanane alikiri kuwa ilikuwa sumu ambayo alipewa na Dk. Slaa, ili amuwekee Zitto.

Shonza alidai kuwa siku ya tukio, yeye na Zitto walikuwa wamekaa meza moja na Saanane ambaye mkono wake wa kushoto ulikuwa umefungwa bandeji aliyowaeleza kuwa aliifunga kutokana na maumivu ya mkono.

Alisema wakiwa katika maongezi, huku Saanane akionyesha kuzidiwa na kilevi alichokuwa amekunywa, alitoa bahasha ya kaki yenye fedha ili alipie gharama za vinywaji vya wote ambayo ilidondoka na ndani yake ikatoka karatasi ndogo ya nailoni ikiwa na unga mwekundu.

Kwa mujibu wa Shonza, Saanane alipobanwa aeleze unga ule ulikuwa nini, awali alidai ni kilevi aina ya kuberi, huku akiwataka wasiifungue nailoni hiyo, jambo ambalo Mwampamba alilikataa na kulazimisha ifunguliwe pale pale.

“Kwa hasira Ben alitaka arudishiwe ile karatasi, lakini, Mwampamba aliondoka nayo, usiku huo huo Saanane alimtafuta Mwampamba hadi nyumbani kwake akidai apewe mzigo wake.

“Mwampamba alimwambia atampa mzigo wake kwa sharti moja tu la kusema ukweli kuhusu kilichomo ndani ya nailoni hiyo na hapo ndipo Ben alipokiri kuwa alipewa mzigo huo ambao una unga unga wenye sumu na Dk. Slaa, ili amuwekee Zitto kwa sababu amekuwa akimsakama ndani ya vikao vya chama.

“Huo ndiyo ukweli ambao nitausema popote, sasa kama Ben alitudanganya kwa kumsingizia Dk. Slaa hiyo ni juu yao wenyewe,” alisema Shonza.

Shonza alisema hali hiyo iliwaogofya na kuanza kuwa makini katika mapito yao na kuongeza kuwa Zitto bado yuko Chadema kwa sababu ana roho ngumu, mvumilivu na mkomavu wa kisiasa, anayeweza kukabiliana na mambo ya hatari.

Dk. Slaa alipoulizwa na MTANZANIA Jumatano kuhusu madai hayo, alisema hilo ni kosa la jinai, ambalo kama anatuhumiwa kulifanya anapaswa kushtakiwa kwenye vyombo vya dola badala ya tarifa hizo kupelekwa katika vyombo vya habari.

“Usipende kutumiwa na watu, lakini aliyekutuma anajua amekutuma kwa sababu gani. Sasa nitakujibu, hivi suala la kuua si ni jinai? Sasa suala la jinai linapelekwa kwenye vyombo vya dola au kwenye vyombo vya habari? Huyo aliyesema yuko Chadema au yuko wapi? Aliyesema hakwenda polisi? Aliyetaka kuuawa hakwenda pia? Sasa ninyi media mmekuwa nani?

“Wa kumuuliza suala hili ni Saanane mwenyewe au Shonza, wangekuwa na nia njema wangekwenda polisi au Zitto mwenyewe angekwenda polisi kushitaki kwa kutaka kuuawa,” alisema Dk. Slaa.

Naye Saanane ambaye amefanya mahojiano na MTANZANIA Jumatano kuhusiana na mambo mbalimbali mabaya ambayo yamekuwa yakielekezwa kwake, akizungumzia madai hayo alisema madai hayo hayana ukweli wowote, bali yanaibuliwa sasa na mahasimu wake kisiasa kwa lengo la kutaka kumshusha baada ya majaribio mengi dhidi yake kushindwa.

“Kwanza siku ambayo wanasema tulikuwa wote mimi sikuwa huko, nashangaa na haiingii akilini kwamba mimi niende hadi Temeke (kwa Mwampamba) tena usiku wa manane kwa ajili ya kufuata sumu ya kuulia panya.

“Hizi ndizo siasa halisi za maji taka, kuliko nipange njama za kuua mtu kwa malengo ya kisiasa, ni bora niache siasa. Ni mwendawazimu pekee atakayeweza kuamini tetesi hizi za ovyo kabisa zinazofanywa na vijana walioshindwa kujenga hoja za maana kwenye majukwaa,” alisema Saanane.

Aliwaonya watu wanaohasimiana naye kisiasa kuacha kumchafua Dk. Slaa kwa kutumia jina lake katika mambo wanayomtuhumu, kwa kile alichoeleza kuwa ni dhambi kubwa kutunga uongo na kuusambaza ili kutafuta huruma ya umma wa Watanzania.

“Nadhani lengo lao hapa ni kumchafua Dk. Slaa kwa tuhuma hizi za uongo zilizotolewa kwa mara ya kwanza na vijana waliotimuliwa Chadema kwa kukisaliti chama na baadaye kuhongwa na makada na viongozi wa CCM ambao wamejiunga nao sasa.

“Sasa kwa tuhuma hizo, kwa nini wasiripoti polisi, inaingiaje akilini mtu kupanga njama kubwa kiasi hicho halafu ukae kimya tu,” alisema Saanane.

BAADA YA HABARI KUTOKA, ZITTO ALIJIBU HIVI

Katika gazeti la Mtanzania toleo na. 7269 la Jumatano Machi 27, 2013 kuna habari yenye kichwa chenye maneno ‘ SIRI YA KUUAWA ZITTO YAFICHUKA’ na vichwa vidogo ‘yadaiwa ilipangwa anyweshwe sumu hotelini’ dk. Slaa atajwa kumtuma Saanane kummaliza’. Habari hii imeniletea usumbufu mkubwa kwani ndugu, jamaa, marafiki na wapiga kura wangu, wamejazwa na wasiwasi mkubwa sana kwamba ninaweza kuuwawa. Napenda kusema yafuatayo:

Moja, sijawahi katika maisha yangu yote kukutana na mtu anayeitwa Ben Saanane na hivyo hicho kikao ambacho inasemekana nilikuwa naye na akajaribu kunipa sumu hakijawahi kutokea. Imetajwa Hoteli ya Lunch Time ambayo sio tu sijawahi kufika, pia hata siijui ipo wapi. Haijawahi kutokea mimi kufanya kikao cha pamoja na Ben Saanane, Juliana Shonza na Mtela Mwampamba. Hivyo habari iliyoandikwa ni ya kufikirika na hivyo naomba mwandishi ahakikishe kuwa vyanzo vyake vya habari vimempa habari sahihi.

Pili, Siamini kamwe kuwa Katibu Mkuu wa chama changu anaweza kupanga kuniua maana hana sababu ya kufanya hivyo. Napenda kurudia kusema kwamba mimi ninaamini kuwa kila nafsi itaonja mauti. Kila mtu atakufa. Kama nitakufa kwa kuuwawa na mtu mwingine ndio itakuwa nimeandikiwa hivyo na Mungu. Ndio maana hata siku moja silalamiki kuhusu vitisho vya kuuwawa nk. Kama kuna mtu anafikiria kuwa kumuua Zitto ndio furaha ya maisha yake atakuwa anajidanganya tu maana Zitto anaweza kufa kimwili lakini mawazo, fikra na maono ya Zitto yataishi tu. Siogopi kufa maana maisha niliyoyachagua ndio haya ambayo yamejaa vitisho. Muhimu kwangu ni kufanya kazi zangu kwa bidii, uhodari na uaminifu. Siku zote nitasimamia ukweli bila kujali uchungu wa ukweli huo.

Tatu, nawashauri watu ambao wamehama CHADEMA na kuhamia vyama vingine watumie muda wao kujenga vyama vyao badala ya kila siku kuzungumzia masuala ya chama ambacho wao sio wanachama tena. Kama mtu kaamua kuhama CHADEMA anapoteza haki ya kujadili masuala ya CHADEMA maana kama angekuwa anapenda kuyajadili asingehama. Naonya mtu yeyote ambaye anatumia jina langu ili kufanikisha malengo yake ya kisiasa. CHADEMA sio pango la watesaji wala wauaji. Kama kuna mwanachama wa chama kingine cha siasa anayedhani kuna mtu ndani ya CHADEMA anapanga mipango ovu aende kwenye vyombo vya sheria kumshtaki. Matendo ya mtu mmoja yasifanyiwe propaganda kama ni malengo ya taasisi.

Nne, Nawashauri viongozi wa CHADEMA na hasa wanachama tutumie muda wetu kujenga mshikamano ndani ya chama. Fitna, majungu, uongo, uzandiki nk kamwe havijengi chama. Chama chetu lazima kiwe mfano bora wa kuheshimu demokrasia na haki za binaadamu. Wananchi hawawezi kutoa dola kwa chama chenye mifarakano. Tusiruhusu kugawanywa kwa matakwa ya watu wachache. Tusimamie misingi ya kuanzishwa chama chetu.

 

Page 1 of 49

<< Start < Prev 1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 Next > End >>