Kuhusu Tuddd Thomas na Tuzo za Kili
Mashabiki wa mtayarishaji wa muziki (Producer), mwenye uwezo wa kipekee, aliyetayarisha wimbo wa Leka dutigite wa Kigoma All Stars na zingine nyingi, Tudd Thomas, wamekuwa wakiulizana maswali mengi wao kwa wao pasipo kupata majibu.
Safari ya Tudd Thomas katika muziki, ilianzia mkoani Iringa akiwa Iringa Records aliporekodi wimbo wa mwanamuziki Marlaw unaoitwa Bembeleza. Wimbo huo ulipata tuzo ya wimbo bora wa mwaka kutoka Kilimanjaro Tanzania Music Awards mwaka 2008 na pia kumfanya Marlaw apate tuzo ya msanii bora wa kiume kupitia tuzo hizo. Baadae alihamia jijini Dar es Salaam na ndipo alipoonesha uwezo wake zaidi kwa kusuka nyimbo zilizotikisa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Hakuna asiyeufahamu wimbo wa Pii Pii (Missing my baby) wa Marlaw ambao aliutengeneza yeye kupitia Studio ya JML. Wimbo huo ulipata tuzo nyingi ikiwa ni pamoja na tuzo ya Nzumari nchini Kenya mwaka 2009 mbapo uliingia kwenye kipengere cha wimbo bora wa Afrika Mashariki, kumfanya Marlaw aingie kwenye kipengele cha msanii bora wa Afrika Mashariki na kunyakua tuzo hiyo. Baada ya hapo wimbo huo ulipata tuzo ya Kilimanjaro nchini Tanzania kama wimbo bora wa mwaka wa Afro pop mwaka 2010, tuzo ya Chaguo la Teneez Music nchini Kenya kama wimbo ulioongoza kwa kuchukuliwa kwa njia ya mtandao Afrika Mashariki “The most downloaded East African song” mwaka 2010, pamoja na tuzo ya Nigeria Sound City Video Music kama wimbo bora wa Afrika Mashariki mwaka 2010.
Aliendelea kutayarisha nyimbo ambazo zilipata umaarufu mkubwa na kuingia kwenye vipengele mbalimbali vya tuzo za muziki za Kilimanjaro. Mwaka 2012, nyimbo tatu zilizotokana na mikono yake zilipata nafasi ya kushiriki tuzo hizo. Nyimbo hizo ni Liz One wa Izzo Business ambao uliingia kwenye vipengele viwili ambavyo ni wimbo bora wa mwaka na wimbo bora wa Hip hop na pia kusababisha msanii huyo aingie kwenye kipengele cha msanii bora wa Hip hop. Milele daima wa Barnaba na Kizunguzungu wa Rachel, ambapo zote ziliingia kipengele cha wimbo bora wa Zouk/Rhumba pia ni nyimbo alizotengeneza mtayarishaji huyo.
Nyimbo zingine alizotayarisha ambazo zilifanya vizuri kwenye vituo mbalimbali vya redio na TV ni Kisa pombe na Soldier za Mwasiti, Sorry sana, Mbayuwayu na Mtoto wa Afrika za Marlaw pamoja na Natumaini ya Becka aliyowashirikisha Barnaba na Amin. Pia zipo nyingine kama Unikimbie ya Amin, Tushukuru kwa yote ya Ditto, Lonely ya Linah na Magubegube ya Barnaba.
Mtayarishaji huyo ambaye hajawai kuingia kwenye tuzo za Kilimanjaro za muziki wa hapa nchini Tanzania ambazo mwaka huu zimeongezewa kipengele cha Mtayarishaji bora chipukizi ndiye aliyetayarisha wimbo wa Leka dutigite wa Kigoma All Stars kupitia Studio yake ya Ngoma Records. Wimbo huu umeingia kwenye kipengele cha wimbo bora wa mwaka 2013. Pia alishirikiana na mtayarishaji Imma the boy kutengeneza wimbo wa Me ‘n’ U wa Ommy Dimpoz ambao umeingia kwenye kipengele hicho na vipengele vingine ambavyo ni wimbo bora wa Bongo Pop na wimbo bora wa kushirikiana.
Alipoulizwa alisema hapendi kuzungumzia juu ya kutotajwa kama miongoni mwa wanaowania tuzo. Aliendelea kusema kwamba, hata kama baadae ikitokea, kwake ni motisha tu, lakini kikubwa zaidi ni kwamba anahisi analo deni kubwa la kutumia uwezo wake ipasavyo kufanya kazi nzuri zaidi ya hapo ili kuutangaza muziki wa Tanzania kimataifa. Pia alisema ana malengo makubwa aliyojiwekea na ndiyo maana kila kukicha anawaza kutayarisha nyimbo zenye tofauti na zenye radha ya kipekee.
Tudd Thomas anaendelea kukitumia kipaji chake na ujuzi wake ipasavyo na siku chache zilizopita kuna nyimbo zisizopungua tatu zilizoingia sokoni na zinafanya vizuri, ambazo ni kazi za mikono yake. Nyimbo hizo ni Uswazi take away ya Chegge, Nyumbani ya Kigoma All Stars na pia ameshirikiana kwa kiasi kikubwa na mtayarishaji Fundi Samwel kutengeneza wimbo wa Mahakama ya mapenzi wa Linex.
Ruge, Kusaga wakimbilia mahakamani, wamshatki Jide
Staa wa Bongo Fleva, Judith Wambura 'Lady Jaydee', leo alifika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, kufuatia kufunguliwa kesi ya madai katika mahakama hiyo.

Katika hati ya madai hayo, mwanamuziki huyo anashtakiwa na viongozi wa Clouds Media Group ambao ni Ruge Mutahaba na Joseph Kusaga.

Tuhuma za kesi hiyo zinatarajiwa kusomwa mahakamani hapo na Hakimu, Athuman Nyamrani Mei 27 mwaka huu.
Jaydee aliwasili mahakamani hapo akiwa na mumewe, Gadner G. Habash, mishale ya saa 6 mchana na kuongoza moja kwa moja chumba cha makarani wa mahakama hiyo ambao aliwakabidhi hati ya mashitaka hayo.
Awali, ilielezwa kuwa Jide leo angefikishwa Mahakama ya Kinondoni, Dar bila kutajwa aina ya mashitaka yanayomkabili.
Taarifa za mwanadada huyo kufikishwa mahakamani hapo, ziliibuka chinichini kwenye mitandao ya kijamii, mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo baadaye Lady Jaydee alihoji kuwa pengine yeye ndiye anayestahili ‘kukinukisha’ kwa kuwapeleka mahakamani wasanii walio chini ya Tanzania House of Talent (THT), Estalina Sanga ‘Linah’ na Elias Barnaba.

Jide alisema kuwa aliwalipa Lina na Barnaba kianzio cha shoo yake ya Mei 31, mwaka huu kisha kumchomolea dakika za mwisho.

“Hivi mahakamani sitakiwi kwenda mimi ambaye wasanii wao wamechukua advance na kuafiki mbele ya camera na wakanipa, It wasn’t me?” aliandika Lady Jaydee katika mtandao wa Twitter.
KUMBUKUMBU
Kumbukumbu inaonesha, miongoni mwa maneno ambayo yanadaiwa kuwa yaliuchafua uongozi wa Clouds ni yale ambayo Lady Jaydee aliyaandika kupitia blogu yake hivi karibuni, akitoa waraka aliouita wosia kwa Rugen a Kusaga ikitokea yeye akitangulia kufa kabla yao.
Katika wosia huo, Jise alisema kuwa Rugen a Kusaga ni watu wabaya, wanaomuua kimuziki, akatamka kwamba siku akifa redio yao isipige nyimbo zake wala kutoa ripoti yoyote ya msiba, wao wenyewe wasisogee kumzika na watu wakitokea, watakaokuwepo wawapige mawe.
RUGE HAKUKAA KIMYA
Hata hivyo, siku chache baada ya Lady Jaydee kuandika wosia huo mzito, Mkurugenzi wa Vipindi na Utafiti wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba alitumia Kipindi cha Power Breakfast kuzipangua hoja moja baada ya nyingine na mwishoni kumalizia kwa kusema Jide anapaswa kusoma alama za nyakati kwani umri unakwenda na muziki anapaswa kujipanga vizuri ili uweze kujimudu pindi zamu ya kushuka kwenye gemu inapofika.
Kuhusu wito wa mahakamani, Jide ‘ali-tweet’: “Nimepata taarifa zisizo rasmi kuwa nimefunguliwa kesi mahakamani, natumaini sitaitwa kizimbani tar. 31 May ambayo ndiyo siku ya show.”
Baadaye aliongeza: “Ratiba ya usiku wa leo (Ijumaa iliyopita) ni Machozi Band kama kawaida, ila ratiba ya Jumatatu (leo) natakiwa Mahakama ya Kinondoni. Taarifa zaidi zitafuata nikijua kinachoendelea. Ila kwa leo mje tuburudike Nyumbani Lounge mpaka asubuhi.”
Mashambulizi ya Jaydee kwa Ruge, Kusaga yaibua msukosuko
Mwanamuziki mkongwe wa Bongo Fleva, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ ameendelea kuwakaba koo wakurugenzi wa Redio Clouds FM, Joseph Kusaga na Ruge Mutahaba.
Jide, ameibua msukosuko wa aina yake nchini kufuatia tamko lake alilotoa jana, akibainisha kwamba Kusaga na Ruge si watu wema na hata akifa, redio yao isitangaze kifo chake wala kupiga nyimbo zake, vilevile na wao hawatakiwi kuhudhuria.

Hili ndiyo tamko lenyewe…
WOSIA WANGU KAMA IKITOKEA NIMETANGULIA KUFA KABLA YA RUGE AU JOE KUSAGA
Watu wanashtuka mtu akiongelea kifo, Utafikiri hawafahamu fika kuwa kila nafsi itakionja, Kwenye maisha yangu nimepitia mambo mengi, magumu na mepesi na bado naendelea ku-experience mambo magumu zaidi kadri ninavyozidi kuwa mkubwa.
Siku za karibuni nimekuwa nikipigwa vita sana na watu wenye uwezo mkubwa kifedha , ki umri na hata wenye ukubwa wa connection katika hii industry ya muziki. Wanaomiliki chombo cha habari.
Nasimama na kusema kuwa sitokata tamaa, kwani lengo lao kubwa ni kuona na kuhakikisha nimeanguka kabisa na sipo katika ramani ya muziki.

Watu hao ambao vita yao ilikuwa baridi miaka kumi iliopita, sasa inazidi kuwa moto baada ya kutambua kuwa mimi ni mtu mwenye maamuzi yangu na misimamo yangu bila kuburuzwa.
Wanapita kila mahali kuhakikisha kila mrija unaoniingizia chochote unakatika, na hiyo ni kutaka kuuthibitishia umma wa Tanzania kuwa hakuna msanii anaeweza ku survive bila wao. Mimi ni msanii tofauti na hao mnaofikiria.
Nadhani mnafahamu tangu niachane na Tuzo zenu mnazo influence nani apate nani asipate, na tangu niachane na Fiesta nilipolipwa laki 8 mara ya mwisho na kuamua kuunda Band ili nijiajiri na kupata shows zangu mwenyewe, ikafanikiwa sana jambo ambalo limewauma na kuamua kufanya kitu cha kuiangusha Band yangu. Nita survive kwa njia zozote MUNGU alizonipangia.

Wakati bado wote tunapumua na kwakuwa watu hao hawanipendi kabisa, Naamini fika hawataweza kunipenda hata siku nitakapokuwa nimekufa. Na huu ndio wosia wangu kwa watu hao.
Natambua wanaweza kutumia redio yao kutangaza sana kifo changu na kusema marehemu alikuwa mtu mzuri na pengine kupiga nyimbo zangu kuanzia asubuhi mpaka jioni.
Ila naomba nitamke hivi, siku nikifa CLOUDS FM isipige nyimbo zangu, wala isiongelee lolote kuhusiana na kifo changu. Ruge Mutahaba na Joseph Kusaga wasihudhurie msiba wangu, na mkiwaona muwapige mawa enyi mtakaokuwa hai baada yangu.
Kama wamenifitini, na hawajanipenda nikiwa hai hakuna haja ya kujifanya kunipenda nikiwa marehemu. Sina haja wanipende pia kwakuwa mimi sio ndugu yao, Ila ubaya wanaoundeleza mioyoni mwao wanaujua na nina hakika nafsi zao zinawasuta pia.
Niliamua kujiepusha nao miaka mingi na kufanya biashara zangu, nimekaa kimya watu wanafikiri nabebwa lakini sijabebwa chochote sikutaka ugomvi haya mambo yalianza baada ya Album yangu ya pili ya Binti mwaka 2003 nilipojitoa Smooth Vibes chini ya Ruge.
Nilivumilia fitna nikiamini ipo siku yatakwisha lakini naona moto ndio unazidi kuwaka. Na hii ni kwasababu wanaogopa msanii akiwa mkubwa watashindwa kumuamrisha, Hamuwezi kumiliki dunia..
Kama mnasema mlinibeba mbona hamkuwabeba dada zenu wa tumbo moja waimbe ili hela irudi nyumbani??. kama kweli wewe Kusaga unajua kubeba basi beba jiwe liimbe liwe star..
Kwa roho zenu mbaya mnaweza kumbeba mpita njia nyie? Talent haibebwi, hujibeba kama mnabisha si mna watoto wabebeni basi wawe kama kina Diamond ndio nitaamini kweli nyie mnaweza kubeba watu.
Mnawatishia wasanii kuwa yoyote atakaefanya nyimbo na mimi hazitapigwa, vikao vinne mmeshakaa kunijadili. Mnadhani je! nitapungukiwa nini endapo wasanii wengine wakiacha kufanya kazi na mimi?? nyimbo hazitakuwa nzuri.
Basi sawa ngoja tuone MUNGU ni nani, Binadamu nani? Kwahiyo mtaamrisha watu pia wasikae na mimi? Ilikuwa niseme majina matatu huyo mmoja nimemsamehe baada ya kugundua sio hiyari yake ila yuko under influence ya hawa jamaa wawili.
Kila siku mnamsingizia Ruge peke yake Kusaga ni mfitini kuliko hata huyo Ruge, watu hamjui tu.
Mtu hela zote hizo bado shillingi mbili ya Jide inakuuma? Roho gani hiyo??
Naishia hapo na sitabatilisha kauli yangu
Jina la Biggie latumika kunadi mjengo
Mjengo wa kifahari uliopo eneo la Clinton Hill, Brooklyn, New York, Marekani, unauzwa kwa thamani ya dola za 750,000, sawa na shilingi 1.2.
Mchawi wa Freestyle, Christopher Wallace ‘Notorious B.I.G’, aliishi kwenye mjengo huo wakati akiwa mdogo.

Kwa vile B.I.G a.k.a Biggie aliishi hapo enzi hizo, wamiliki wa jengo hilo, wameamua kutumia jina lake kwa ajili ya kulinadi, kwa imani kwamba litapata wateja kwa urahisi.
Matangazo mengi mtandaoni, yanasomeka: “Nyumba aliyoishi Biggie inauzwa.”



Familia ya Biggie ambaye alifariki dunia miaka 16 iliyopita, haijatoa tamko kama inaona sawa au kuchukizwa na matumizi ya jina la mkali huyo wa Hip Hop katika mauzo ya mnada wa jengo hilo.
Lady Jaydee: Mungu si Ruge wala Kusaga
Stadi wa Bongo Fleva, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ ametamka kwamba anaamini hatarudi nyuma na hatatetereka kimuziki kwa sababu anamtumaini Mungu.
Kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii ya Twitter, Jaydee a.k.a Binti Komando, aliandika: ‘Mungu siyo Ruge wa Kusaga kwa hiyo naamini nitashinda.”

Kabla ya hapo, Jaydee ak.a Jide ambaye zamani alipenda ajulikane kama Binti Machozi, aliandika: “Msemo wa Mungu siyo Athumani kila mtu anaujua, ila mimi ninao mpya.”
Baada ya muda mfupi ndipo akaandika: “Msemo wangu naamini Mungu siyo Ruge wala Kusaga, kwa hiyo naamini nitashinda.”

Jide ambaye ni mmoja wa wanamuziki waasisi wa Bongo Fleva, ameamua kujiweka wazi kiharakati, akipingana na unyonyaji wambao unafanywa katika muziki na washikadau.
Jide kama ambavyo kaka zake wa Vinega walivyokuwa wanafanya katika mixtape za Anti Virus, anawashambulia wakurugenzi wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga na Ruge Mutahaba pamoja na kituo chao cha redio cha Clouds FM.
Kweli Bi. Kidude ametutoka
Mwanamuziki mkongwe wa Taarab, Fatuma Binti Baraka Khamis, maarufu kwa jina la Bi Kidude amefariki dunia leo huko Bububu Zanzibar, sehemu alikokuwa anauguzwa.
Taarifa hizo, zinafuatia uvumi wa mara kwa mara kwamba Bi. Kidude hatunaye lakini nyakati zote zilikuwa uzushi ila sasa ni ukweli kwamba mkongwe huyo ametutoka.

Habari zinasema kuwa, mwili wa marehemu Bi. Kidude, utahamishiwa nyumbani kwake Rahaleo na mazishi yanatarajiwa kufanyika kesho.
Sababu ya kifo chake haijawekwa wazi lakini ukweli ni kwamba Bi. Kidude alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya kisukari kwa muda mrefu na tangu mwaka jana, hali yake ilikuwa tete sana.
Vilevile, zipo taarifa kwamba Bi. Kidude alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya uvimbe kwenye kongosho.

Bi Kidude alizaliwa katika kijiji cha Mfagimaringo, alikuwa binti wa mchuuzi wa nazi, hakuna anayejua haswa Bibi huyu alizaliwa tarehe ngapi, wapo wengine wanaoamini kwamba mpaka mauti yamemfika, kulikuwa na uwezekano alishafikisha zaidi ya umri wa miaka 102.
Katika mwaka 1920 tayari alikuwa amekwisha anza kuimba katika vikundi vya sanaa kule kwao, mwaka 1930 alijiunga na Egyptian Musical Club ya Dar es Salaam na kuzunguka miji mingi ya Tanzabua Bara, mwaka 1940 alirudi Zanzibar ambako awali alikuwa amekimbia kwa kuwa aliozwa kwa nguvu na mtu aliyemzidi sana umri.
Bi Kidude pia aliwahi kuimba na Sitti Binti Saadi wakati wa ujana wake na katika maisha yake Bi Kidude amekwisha zunguka mabara yote akiimba katika majukwaa na wanamuziki maarufu ulimwenguni.
Na kuhusu kuzaa, haijawahi kuripotiwa popote kama Bi. Kidude aliwahi kuzaa.
Mungu Amlaze Pema Peponi Bibi yetu. Amen.
Bosi wa East Africa Melody afariki dunia
Mkurugenzi wa Kikundi cha Taarab cha East African Melody, Hadji Mohamed, amefariki dunia asubuhi hii baada ya kuugua kwa muda mfupi katika hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Taarifa zaidi kuhusu kifo hicho, zitakuja baadaye.

Roma siyo mwana Hip Hop, anaimba ngonjera
Rapa Ibrahim Mussa Mshamu ‘Roma Mkatoliki’, amepoteza dira, maringo yanammeza, anagombana mpaka na watu waliomsaidia kufika mahali alipo.
Hazijapita siku nyingi, tangu Roma alipodaiwa ‘kuwadisi’ watangazaji, wakati akiwa jukwaani, akifanya shoo ya kuwasindikiza Kigoma All Stars ‘Leka Dutigite’, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Wiki mbili zilizopita, gazeti ndugu na hili la Ijumaa Wikienda, kupitia safu yake ya Kiti cha Moto, lilichapisha maoni ya wasomaji ambao wengi wao walimkosoa Roma kwa tabia yake ya maringo na kuwadharau watu.


Ni Roma huyohuyo, katika tamasha lililoandaliwa na kampuni moja ya simu za mkononi mapema mwaka huu, Coco Beach, Dar es Salaam, alichelewa kufika eneo la tukio, hivyo kusababisha usumbufu mkubwa.
Mashabiki walirusha chupa na mawe jukwaani, amani ikahatarishwa, chanzo kikiwa ni mtu ambaye amelipwa fedha kwa ajili ya kazi yake, akapangiwa muda lakini kwa makusudi akachelewa.
Mbaya zaidi ni kwamba katika wanamuziki wote walioalikwa kutumbuiza kwenye onesho hilo, ni Roma peke yake aliyechelewa.
Mashabiki wakawa wanauliza alipo Roma kwa sababu walitangaziwa atakuwepo, mwisho wakafanya fujo kwa imani kwamba wametapeliwa. Kumbe rapa mwenyewe ndiye tapeli wa muda.
UNAONA ALIVYO KIMEO?
Kama tabia yake inawachukiza mashabiki kwa kiwango ambacho mpaka wao wenyewe wanatuma maoni kumkosoa kwamba ana maringo, kiburi na dharau, hapo anachezea shilingi kwenye choo cha shimo.
Umaarufu na mafanikio ya Roma, havijafikia hata theluthi moja ya Nice Lucas Mkenda ‘Mr. Nice’ lakini leo hii yupo wapi? Dharau, nyodo, kiburi na maringo, viliwachukiza mashabiki, wakamtema, leo anahangaika.
Kama Nice anatumikia adhabu ya kile alichowafanyia mashabiki miaka ya nyuma, Roma yeye ni nani mpaka yasimkute? Kila mtu huvuna alichopanda. Siku zinavyozidi kwenda, atajikuta hana mpya.
Kivipi anawadisi Watangazaji? Bila watu hao Roma siyo lolote. Ni utovu wa busara, kuingia mgogoro na wanaoufanya muziki wake usikike. Kwa vile hajitambui, kweli ni kimeo!
Kwa matukio mithili ya lile la Coco Beach, sasa siwezi kushangaa ni kwa nini Roma hapati shoo nyingi. Mapromota wanamwogopa, pale alipo anajiona ameshakuwa Shawn Cutter ‘Jay Z’, wakati kiwango chake bado kipo chini sana.
Sasa atakimbilia wapi ikiwa kila upande sasa anaonekana kimeo? Roma anatakiwa kutambua kuwa kipaji ni kipengele kimoja lakini mvuto wa kibiashara anatakiwa aujenge yeye mwenyewe.
WANA HIP HOP HAWAMKUBALI
Mwaka jana, alizua gogoro zito kwa wadau wa Hip Hop, pale alipopewa tuzo mbili za Mwanamuziki Bora wa Hip Hop na Wimbo Bora wa Hip Hop kupitia singo yake ya Mathematics.
Wadau wa Hip Hop, walikosoa kwamba Tuzo za Kili (Kilimanjaro Tanzania Music Awards), zilikosa weledi kwa kumpa tuzo Roma kwa sababu hana vigezo.
Prodyuza mkongwe nchini, Paul Matthysse ‘P. Funk’, alisema: “Yule siyo mwana Hip Hop, ndani ya Roma hakuna Hip Hop, yule ni mpiga kelele tu.”
Hili la Roma kuwa mpiga kelele, limekuwa likisemwa na wengi kwamba hushindwa kuzingatia aina ya nyimbo, badala yake hupayuka kiasi ambacho humfanya msikilizaji asijue anachorap.
HAJUI KUTUNGA
Kingine ambacho Roma anatakiwa kujirekebisha ni kujifunza kutunga, kwani nyimbo zake hazioneshi uwezo wake wa kuandika, bali kile ambacho hufanya huwa ni kugusa vitu mbalimbali.
“Huwa haoneshi uwezo wa kisanii, ndani ya mstari mmoja anaweza kugusua vitu viwili au vitatu bila kutoa picha rahisi kwa msikilizaji. Hii huwafanya wengi ambao wanakuwa hawajui vitu anavyorap, wabaki gizani, huo siyo usanii.
“Utunzi huendana na hoja. Angalia nyimbo za akina Profesa Jay (Joseph Haule) au MwanaFA (Hamis Mwinjuma), wakiimba kitu wanasaidia msikilizaji aelewe vitu kwa uchambuzi wa hoja za kisanii.
“Watu wanaoweza kumshabikia Roma, labda ni wale wapenda kelele ila wanaojua muziki lazima watofautiane naye,” alisema mwana Hip Hop mwenye heshima kubwa nchini kwa sharti la kutotajwa jina.
Mwana Hip Hop huyo akaongeza: “Hip Hop ni hoja, angalia hata mashairi ya Fid Q (Fareed Kubanda). Roma siro rapa, ni mwimba ngonjera. Hata tungo zake zimekaa kingonjerangonjera. Kimahesabu, yeye ndiye rapa Bongo mwenye tungo dhaifu zaidi.”
ANAYO NAFASI YA KUJIREKEBISHA
Mtu anapokosolewa, inabidi kujisahihisha ili kuishi ndani ya mstari unaokubalika. Pamoja na yote ambayo anakosolewa, binafsi naamini anaweza kujirekebisha na kufanya vizuri.
Kama ni maringo, kiburi, jeuri na dharau, basi aache. Kuhusu uzingatiaji wa muda anapopewa kazi ya kutumbuiza, inafaa aheshimu, kwani hiyo ni ajira yake. Namshauri asipotee kwa kuendekeza kuwadisi watangazaji.
Kuhusu tungo, ule ni ushauri tu, bila shaka akiwaona akina Prof. Jay, FA, Fid Q na wengineo, wanaweza kumfunda namna bora ya kuandika mistari iliyoshiba hoja za kisanii ili aachane na mashairi ya ngonjera kama mwana Hip Hop mwenzake alivyomkosoa.
Makala haya ni maoni ya ripota wa DeiwakaWorld, siyo msimamo wa Deiwaka.
Click here for TUMA Registrations.