Abramovich adaiwa kusababisha kifo cha mpinzani wake
Mmiliki wa Klabu ya Chelsea ya England, Roman Abramovich, ametupiwa skendo kwamba yeye ndiye sababu ya kifo cha mpinzani wake, Boris Berezovsky, aliyefikwa na mauti akiwa na umri wa miaka 67.
Berezovsky, aliyekutwa amefariki dunia, nyumbani kwake mjini Ascot, Berkshire, magharibi mwa Jiji la London, England, Jumamosi iliyopita, kifo chake kimezua utata mkubwa.
Tajiri huyo wa Kirusi, aliyekuwa akiishi uhamishoni England, moja ya sababu ya kifo chake imetajwa pengine amewekewa sumu lakini kubwa zaidi ni madai kwamba trilionea huyo kwa chenji ya madafu, alianza kupata wakati mgumu tangu alipopoteza mabilioni ya pauni, aliposhindwa kesi mahakamani na Abramovich.


Berezovsky, alimburuza Abramovich mahakamani, akimtaka amlipe fidia ya pauni bilioni 3 (shilingi trilioni 7.4), akidai alimdhulumu katika mgawo wa fedha kwa uwiano wa hisa, baada ya kuiuza kampuni ya mafuta ya Urusi, Sibneft.
Madai ya msingi kama yalivyowasilishwa mahakamani na Berezovsky, yalisema: “Abramovich kwa kutambua haki na wingi wa hisa za Berezovsky, hakutenda haki na kumpa gawio dogo baada ya Abramovich kuiza Kampuni ya Sibneft.”
Hata hivyo, baada ya kusikiliza kesi hiyo, Abramovich alimbwaga Berezovsky, hivyo Jaji wa Mahakama ya Biashara, Uingereza, Dame Elizabeth Gloster ‘Lady Popplewell’, aliagiza Berezovsky amlipe Abramovich gharama zote za uendeshaji wa kesi.
Berezovsky, alikubali kumlipa Abramovich fidia ya pauni milioni 35 (shilingi bilioni 86) ingawa taarifa ilitolewa baadaye kuwa alitakiwa kulipa pauni milioni 100 (shilingi 246).
Tangu kushindwa kesi hiyo mwaka jana, Berezovsky alianza kunyong’onyea, muda mwingi akiwa na msongo wa mawazo kabla ya Jumamosi iliyopita kukutwa amefariki dunia nyumbani kwake.
“Kama siyo sumu basi pigo alilopata kutoka kwa Abramovich ndiyo limesababisha. Sibneft ilipouzwa aliathirika sana kwa mgawo aliopata kutokana na hisa nyingi alizokuwa nazo, aliposhindwa kesi, alizidi kunyong’onyea.
“Kwa pamoja, Abramovich na Rais wa Urusi, Vladimir Putin wameharakisha kifo cha Berezovsky kwa sababu aliondoka Urusi na kuishi uhamishoni England kwa sababu ya tofauti zake na Putin.
“Alipoteza mali na fedha nyingi alipohamia England, Abramovich akazidi kumuumiza alipoiuza Sibneft na fidia ya kesi aliyotakiwa kumlipa,” kilisema chanzo.
Msemaji wa kampuni ya Berezovsky, Bell Pottinger, alisema: “Mwili wa marehemu uligunduliwa na bodigadi wake. Hakuna taarifa zaidi ya hizo mpaka wakati huu.”
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, Berezovsky mpaka anakumbwa na mauti, alikuwa na utajiri wenye thamani ya pauni bilioni 5 (shilingi trilioni 12) na inaelezwa angekuwa mbali ya hapo kama asingekutana na misukosuko na serikali yake ya Urusi pamoja na mgogoro dhidi ya Abramovich.