Mapenzi bora hupitia katika mzani, jifunze kupima na ‘kubalansi’
Hivi karibuni, niliandika mada “mahaba niue ni matokeo ya kuokosea vipimo vya mapenzi.” Huo ndiyo ukweli na makala haya ni maarifa kwako ili upate namna bora ya kuujua mzani wa mapenzi, kupima na kujua kutengeneza ulinganifu (kubalansi).
Huko nyuma, nimewahi kuandika mada inayosema, “Mapenzi ni matamu lakini siyo rahisi”. Nilieleza kwa upana jinsi ya kukabili. Leo nimekuja na muongozo wa jinsi ya kufanya ili uyaweze mapenzi na kuushinda ugumu uliopo.

Mada hii siyo tu lengo lake ni kukufanya ujue mzani, kuyapima mapenzi na kubalansi, pia itakufanya uyaelewe mapenzi. Si kukimbilia kuacha pale kunapotokea tofauti za hapa na pale na mwenzi wako wa maisha. Uvumilivu unahitajika, amini kwamba utamu wote unaoyazunguka ‘malavidavi’ kuna ugumu mkubwa.
Hapa tunazungumzia elimu zaidi inayoweza kukukomboa wewe kwa kuheshimu hisia za mwenzako na wakati huo huo ukawa unajali za kwako. Kwa pamoja ndipo utaweza kufanikiwa kuwa na moyo tulivu katika nyakati zote.
Ukiheshimu hisia za mwenzi wako na ukawa unajali za kwako, itakusaidia kukufanya uwe na tumaini chanya wakati wote. Wakati wa matatizo, hasa kipindi ambacho hampo kwenye maelewano mazuri, utabaki na imani kwamba yote yatakwisha.
Penda kuamini kuwa “hili nalo litapita” kwamba wakati ambao mwenzi wako amenuna, hataki kuzungumza na wewe, unachopaswa kufanya ni kuheshimu hisia zake na uamini kwamba mwisho atatulia na uhusiano wenu utaendelea kwa maelewano makubwa.
Ukitaka kulazimisha awe mchangamfu kwako kipindi ambacho amenuna, ni sawa na kukaribisha matatizo zaidi. Ni vema kuelewana, watu wengi wanakosea katika uhusiano wao kwa sababu hawatumii busara ili kuwawaelewa wenzi wao pindi wanapoonesha hali tofauti.
Busara iendelee kuchukua nafasi. Maneno “hili nalo litapita” liwe somo kwako. Kwamba leo umerudi nyumbani, umetaka chakula cha faragha, mwenzako amekwambia hajisikii vizuri. Hutakiwi kupandisha mizuka na kusababisha nyumbani pasilalike kwa siku hiyo.
Badala yake unapaswa kuvumilia. Jiulize mmefanya tendo mara ngani katika uhusiano wenu, iweje siku hiyo akwambie hajisikii? Ukilazimisha ni sawa na kumfanyia mwenzako ubakaji. Si ajabu akikuona unakuwa mkali, akakubali kukupa kwa shingo upande lakini si kwa ridhaa yake.
Mapenzi ni matamu lakini siyo rahisi kwa maana, nyakati nyingine utalazimika kuvumilia mambo ambayo pengine yakakuumiza. Mko wawili na kujenga tafsiri ya mwili mmoja. Pengine hata makundi yenu ya damu ni tofauti. Ilivyo maumbile yenu ni hasi na chanya ndiyo na damu zenu zilivyo.
Tofauti hiyo mnaielewa na kuikubali, iweje siku ukirudi nyumbani unamkuta amenuna na hataki kuzungumza na wewe ushindwe kuelewa? Hapo ndipo uvumilivu wako unahitajika. Ni kipindi ambacho busara zako zinapaswa kufanya kazi kwa asilimia 100. Usilazimishe afanye upendavyo wakali mwili wake haupo tayari.
Unaingia faragha na mwenzi wako. Ameshindwa kukuridhisha kabisa. Ni hekima zako kutambua kwamba siku hazilingani. Mbona siku nyingine alikupa mambo mazuri mpaka ukasema ‘poo’? Tatizo ni nini? Pengine nishati za mwili wake kwa siku hiyo hazipo sawasawa na hata yeye mwenyewe hajui.
Ukimkejeli kuwa hajiwezi ni sawa na kumchinjia baharini. Siku zinazokuja atashindwa kabisa. Si kwa sababu uwezo wake ni mdogo, la hasha! Maneno yako ya kejeli na dharau ndiyo yatakayoufanya moyo wake usinyae na kukuogopa ndani kwa ndani. Fikra zake zitashambuliwa na ugonjwa hatari.
Si ugonjwa unaosababishwa na kirusi, hapana. Ni gonjwa la maneno litakaloshambulia ubongo wake. Kila mara kabla ya kuingia mchezo atakuwa na maswali ya kujiuliza. “Sijui leo nitashindwa tena?” “Nikishindwa itakuwaje?” “Atanitukana tena?” “Hivi mimi ni mgonjwa?”
Mwisho wa maswali hayo atahitimisha kauli kwa kusema: “Inawezekana mimi ni mgonjwa kweli ndiyo maana nashindwa kazi.” Amini kuwa kauli hiyo ndiyo ugonjwa hatari ambao utashambulia hisia zake na kuusababisha mwili ushindwe kufanya kazi sawasawa.
Ukitaka kuendelea kufurahia mapenzi ni vizuri umpe moyo mwenzi wako pale inapoonekana ameshindwa kutekeleza kazi ya faragha inavyotakiwa. Kaa naye vizuri na umueleze kwa lugha laini kwamba baadaye au siku inayofuata mtafanya tena kikamilifu na hakutakuwa na kushindwa.
Ikibidi msifie, mwambie kuwa yupo kamili kwa sababu kila siku mnapoingia kazini huwa unatosheka. Mueleze kuwa siku hiyo anasumbuliwa na uchovu au hajisikii vizuri. Maneno hayo utayaona madogo lakini yatamjenga ipasavyo. Yatamrejeshea ari na afya, kwa hiyo siku nyingine hatakuogopa.
Mapenzi ni matamu lakini siyo rahisi. Hii imesababisha watu wengi kushindwa kushirikiana vema na wenzi wao. Jambo dogo la kumuelewesha mwenzake linakuwa tatizo mpaka uhusiano unageuka shubiri. Wawili walioitana majina matamu na yenye kupendeza, wanageuka maadui.
Wanatangaziana sifa mbaya. “Yule muoneni hivyo hivyo kwa nje, hajiwezi kabisa kitandani.” Ni maneno ambayo si mageni. Yanasababishwa na watu kutotambua thamani ya mapenzi, ugumu uliopo ili iwe rahisi kwao kupata alama A kwenye uhusiano wao. Mapenzi ni magumu lakini ni rahisi sana.
Kanuni ni moja tu, kuwa mwelewa. Unaona mwenzi wako anashindwa kukufikisha unapopataka, wewe una jukumu la kumwelewesha. Mfahamishe maeneo ambayo anatakiwa ayafanyie kazi ili ufurahie tendo. Amini kuwa ukifanya hivyo, itakuwa rahisi kwako. Mapenzi ni matamu kama utayajua na kuyaweza.
Kuna maswali ya kujiuliza kuhusu mapenzi. Hayo ndiyo yatakuwezesha kutambua kama unatosha kuendelea na mwenzi wako au kinyume chake. Yatakusaidia kufurahia maisha yako ya kimapenzi.
Itaendelea wiki ijayo.
Mapenzi bora hupitia katika mzani, jifunze kupima na kubalansi - 2
Mapenzi ni matamu lakini siyo rahisi. Mada hiyo niliyoiandika kwenye gazeti hili kwenye matoleo yaliyopita ndiyo imeleta muendelezo huu. Hii ni sehemu ya pili na lengo lake ni kuushinda ugumu uliopo na kuyaweza mapenzi kwa asilimia 100.
Jambo la muhimu ni kwamba usije ukaingia kwenye uhusiano ukidhani kila kitu ni chepesi. Unatakiwa kujipanga, halafu uwe mdadisi kisha upite njia inayostahili.
Ugumu mkubwa ambao upo kwenye mapenzi ni pale mtu anapotaka aoneshwe upendo kulingana na jinsi anavyopenda. Inapotokea anabaini tofauti kati ya anavyopenda na anavyopendwa inakuwa shida kubwa. Hataki kupenda zaidi, eti ataonekana wa bei nafuu.
Kila mtu anataka apendwe zaidi. Kwa nini wewe usiwe wa kwanza kujitoa kumpenda mwenzi wako kuliko yeye anavyokupenda? Ni mtihani mdogo lakini unawashinda wengi na kusababisha mvutano.
Uzoefu unaonesha kuwa watu wengi hawana imani na wenzi wao. Dosari ndogo inaweza kuwafanya wajenge imani kuwa wenzi wao hawawapendi. Kila mmoja analalamika kivyake. “Hanipendi kama mimi ninavyompenda.” Ugumu wa mapenzi huanzia hapo.
Nimeshachambua mengi huko nyuma. Kwa nyongeza, leo nakutaka ujiulize maswali yafuatayo ili uepukane na ugonjwa wa moyo, badala yake, mapenzi kwako yawe kitu rahisi ambacho utakimudu kwa asilimia 100.
*Tazama unavyojisikia pale unapopenda. Je, unapopenda unajisikia vizuri hata kama umpendaye hakupi upendo kama ulionao kwake? Je, kumpenda mtu, ni lazima naye akupende kwa kiwango hicho hicho? Kama ndivyo, ni kwa nini?
*Unajisikia unapendwa hata kama mwenzi wako hayupo? Kama sivyo, ni kwa nini? Je, unajikubali na unaridhika kwa sifa ulizonazo?
*Unafanya vitu kwa ajili ya mpenzi wako? Hata kama hutaki kufanya, je unajitahidi kutekeleza ili kuliweka penzi lenu hai? Unafanya kwa ajili ya mapenzi yake na unahitaji kila unachofanya, naye akufanyie hivyo hivyo?
*Je, umewahi kumueleza mwenzi wako vitu ambavyo ukifanyiwa vinaweza kukufanya ujisikie kupendwa? Amewahi kutekeleza vitu hivyo kwa ajili yako? Kama bado, umewahi kuvumilia na kumfundisha taratibu?
MNAFANANA?
Swali hili lipe uzito. Inawezekana kwenye maswali ya juu ukawa umevuka vizuri. Pamoja na hivyo, haioneshi kama kuna mambo ambayo wewe na mwenzi wako mnafanana. Kama hamuendi sawa, jifunze kumuelewa.
Unaamini katika sanaa, mwenzako anadatishwa na michezo. Unapenda kusoma vitabu na kutoka kwenye matembezi ya hapa na pale, lakini yeye anapenda kusafiri. Hata hivyo, unapaswa kuamini kwamba ndoa ni kujitoa muhanga.
Siyo sawa na kutoa na kuchukua. Inatakiwa uwe mwelewa, katika kuhakikisha mapenzi yenu yanafanikiwa, ni vizuri ukahifadhi mambo yako kisha ukaungana naye kwenye mambo yake. Baadaye utamfanya aungane nawe kwako taratibu.
Hilo litafanikiwa kama utaacha ubinafsi. Tabia ya kutaka upendwe zaidi ni kosa. Katika uhusiano hutakiwi kujifikiria wa kwanza. Wekeza upendo mkubwa, halafu umfanye naye akupende. Si kwa haraka, bali taratibu.
Kama kila unaloamini wewe yeye yupo mbali, jifunze mambo yake kwanza. Muelewe kisha mshirikishe yako. Leo ukimfanya ajue kwamba unapenda kuogelea, keshokutwa mpe lingine na umjulishe kuwa ungependa mwende pamoja.
Itaendelea wiki ijayo.
Mapenzi bora hupitia katika mzani, jifunze kupima na kubalansi - 3
Kipengele cha jinsi unavyofanana na mwenzi wako ndicho kilitufungia sehemu ya nne ya makala haya. Naendelea kusisitiza kuwa haitakiwi kushindana, unapaswa kukubali kuachia vipaumbele vyako ili umpe nafasi mwenzi wako.
Ni mchezo mdogo lakini mgumu, maana yake ni kuyaweza mapenzi. Ni jambo ambalo lipo karibu na kutowezekana kwa mpenzi wa mpira kuacha ‘rimoti’ ya televisheni kwa mwenzi wake ili aangalie tamthiliya. Hata hivyo, endapo mtagombea rimoti, mwisho mtaanza kuchokana mapema.
KUNA MABADILIKO?
Vema kujiuliza swali hilo na matawi yake. Hii itakusaidia kutanzua mambo ambayo yanaweza kusababisha uhusiano wenu ukaenda na maji hapo baadaye.
* Kuna kiasi cha mabadiliko kwa kila mmoja wenu tangu mlipokutana kwa mara ya kwanza?
* Bado unachangia na mwenzi wako kila kitu chenu kama ambavyo mlifanya wakati mnaanza kupendana?
* Kinatokea nini pale kila mmoja hufanya mambo anayojisikia mwenyewe?
* Una muda kiasi gani kutumia na mwenzi wako? Je, unajihisi upo kwenye uhusiano imara na wenye mafanikio? Jiulize, inamaanisha nini kuwa na maslahi tofautin kati yako na mwenzi wako?
* Umewahi kutafakari na kugundua kwamba wewe na mwenzi wako, kila mmoja ni mtu huru lakini mmeamua kuwa pamoja au zipo dalili za kifungo?
* Je, unaamini mapenzi ni kujitoa mhanga? Kama ndivyo ni kwa nini?
JADILI MASWALI HAYO NA MWENZIO
Lazima maswali hayo uyapatie majibu, si kwa wewe peke yako bali kwa kushirikiana na mwenzi wako. Kama kuna sehemu yenye utata basi haraka sana, mnaitolea macho na kuondoa tofauti. Hakikisha kila kitu kinakuwa chanya.
Hata hivyo, pengine kila unapoweka mezani ‘ishu’ ya kujadili inageuka ubishi. Ndani ya ubongo wako, unaamua kuachana na ‘topiki’ hiyo kwa lengo la kuepuka migogoro. Unahisi mbele ya ubishi kuna ugomvi, nawe hupendi kugombana kwani inaweza kuhatarisha mapenzi yenu.
Hata hivyo, kuacha kujadili jambo ambalo linawatofautisha ni hatari zaidi, hivyo ni busara kutafuta meza ya mazungumzo kwa namna yoyote ile. Ni kosa kubwa kuwa na maslahi tofauti kwenye mapenzi. Mnaweza kutofautiana mambo mengine lakini siyo hilo.
Mathalan, wewe unaamini kwamba mpenzi uliyenaye kwake ndiyo umefika, yeye hilo halipo akilini. Unawaza ndoa mwenzako anakutafsiri kama ni wa kuzugia. Uhusiano wa namna hiyo haupo sawa, una matege, haufai kuendelea kujengwa. Unaweza kumrekebisha, kama habadiliki, ni bora ukimbie.
Vema ukajiuliza mwenyewe, ni muda gani utaishi na mtu ambaye hana mpango na wewe. Kila ukianzisha mada ya ndoa anakuwa mkali. Lazima wote muwe na maslahi ya aina moja, nyote mtamani kuoana, hapo mtaweza kufika, vinginevyo utakuwa unajenga, mwenzako anabomoa.
Kama nilivyotaka ujiulize hapo juu, kwamba wewe na mwenzi wako kila mmoja ni mtu huru. Hii inamaanisha kuwa mapenzi siyo kifungo. Unapaswa kumuacha aamue mwenyewe kuhusu hatma ya mapenzi yenu. Ukionekana unambana, anaweza kufanya mambo kukuridhisha lakini kuna siku atakuadhiri.
Baadaye anaweza kuthubutu kukwambia: “Sikutaka kufunga ndoa na wewe, sema tu ulinilazimisha.” Kauli hii ni tusi, endapo utaitafakari kwa mlengo kuwa uliyenaye hana mapenzi ya dhati nawe. Hata kuwa naye ni kama umemlazimisha.
Tafakari kisha upate jibu kwamba mwenzi wako hana hisia na wewe. Huo ndiyo ukweli kwa maana mapenzi ni hisia. Kama mwenzi wako anakupenda, maana yake ana hisia juu yako, baada ya hapo sasa tafsiri kinyume chake. Unaweza kujiona mdogo kama piritoni.
Hutakiwi kufika huko, vema ujiwekee utaratibu wa kutafakari kila hatua ya uhusiano wako. Kuna maswali mengi ambayo nimekutaka ujiulize. Hayo yatakusaidia kukupa picha ya uhusiano wako ulipo na unapoelekea.
Si kukimbiliia kuachana au kuvumilia yasiyovumilika kwa kudhani mwenzi wako atajirekebisha. Bila dira, hutafanikiwa. Vema ujue kuwa hakuna ugumu kwenye mapenzi kama utajifunza na kuyaelewa kikamilifu.