Ruge, Kusaga wakimbilia mahakamani, wamshatki Jide
Staa wa Bongo Fleva, Judith Wambura 'Lady Jaydee', leo alifika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, kufuatia kufunguliwa kesi ya madai katika mahakama hiyo.

Katika hati ya madai hayo, mwanamuziki huyo anashtakiwa na viongozi wa Clouds Media Group ambao ni Ruge Mutahaba na Joseph Kusaga.

Tuhuma za kesi hiyo zinatarajiwa kusomwa mahakamani hapo na Hakimu, Athuman Nyamrani Mei 27 mwaka huu.
Jaydee aliwasili mahakamani hapo akiwa na mumewe, Gadner G. Habash, mishale ya saa 6 mchana na kuongoza moja kwa moja chumba cha makarani wa mahakama hiyo ambao aliwakabidhi hati ya mashitaka hayo.
Awali, ilielezwa kuwa Jide leo angefikishwa Mahakama ya Kinondoni, Dar bila kutajwa aina ya mashitaka yanayomkabili.
Taarifa za mwanadada huyo kufikishwa mahakamani hapo, ziliibuka chinichini kwenye mitandao ya kijamii, mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo baadaye Lady Jaydee alihoji kuwa pengine yeye ndiye anayestahili ‘kukinukisha’ kwa kuwapeleka mahakamani wasanii walio chini ya Tanzania House of Talent (THT), Estalina Sanga ‘Linah’ na Elias Barnaba.

Jide alisema kuwa aliwalipa Lina na Barnaba kianzio cha shoo yake ya Mei 31, mwaka huu kisha kumchomolea dakika za mwisho.

“Hivi mahakamani sitakiwi kwenda mimi ambaye wasanii wao wamechukua advance na kuafiki mbele ya camera na wakanipa, It wasn’t me?” aliandika Lady Jaydee katika mtandao wa Twitter.
KUMBUKUMBU
Kumbukumbu inaonesha, miongoni mwa maneno ambayo yanadaiwa kuwa yaliuchafua uongozi wa Clouds ni yale ambayo Lady Jaydee aliyaandika kupitia blogu yake hivi karibuni, akitoa waraka aliouita wosia kwa Rugen a Kusaga ikitokea yeye akitangulia kufa kabla yao.
Katika wosia huo, Jise alisema kuwa Rugen a Kusaga ni watu wabaya, wanaomuua kimuziki, akatamka kwamba siku akifa redio yao isipige nyimbo zake wala kutoa ripoti yoyote ya msiba, wao wenyewe wasisogee kumzika na watu wakitokea, watakaokuwepo wawapige mawe.
RUGE HAKUKAA KIMYA
Hata hivyo, siku chache baada ya Lady Jaydee kuandika wosia huo mzito, Mkurugenzi wa Vipindi na Utafiti wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba alitumia Kipindi cha Power Breakfast kuzipangua hoja moja baada ya nyingine na mwishoni kumalizia kwa kusema Jide anapaswa kusoma alama za nyakati kwani umri unakwenda na muziki anapaswa kujipanga vizuri ili uweze kujimudu pindi zamu ya kushuka kwenye gemu inapofika.
Kuhusu wito wa mahakamani, Jide ‘ali-tweet’: “Nimepata taarifa zisizo rasmi kuwa nimefunguliwa kesi mahakamani, natumaini sitaitwa kizimbani tar. 31 May ambayo ndiyo siku ya show.”
Baadaye aliongeza: “Ratiba ya usiku wa leo (Ijumaa iliyopita) ni Machozi Band kama kawaida, ila ratiba ya Jumatatu (leo) natakiwa Mahakama ya Kinondoni. Taarifa zaidi zitafuata nikijua kinachoendelea. Ila kwa leo mje tuburudike Nyumbani Lounge mpaka asubuhi.”
Ukweli kamili kuhusu bomu lililotupwa kanisani Arusha
Kama tulikuwa tunasubiri dalili kubwa zaidi zijitokeze ndipo tutambue kwamba hali ya nchi inatisha, tukio la bomu kutupwa kanisani, likasababisha vifo na majeruhi, lipimwe kama ishara ya juu kabisa.

Pamoja na kila kinachosemwa kuzunguka tukio hilo, ukweli ni kwamba serikali ina kazi kubwa ya kufanya kutuliza mdudu hatari wa ubaguzi ambaye anaelekea kufanikiwa kuwagawa Watanzania kutokana na matukio ya aina hiyo.
Kudhihirisha hali ilivyo mbaya, maneno ya chuki ya kidini yalitawala jijini Arusha na katika mitandao ya kijamii kuzunguka nchi nzima, baadhi ya wakosoaji wakiwashutumu watu wa dini fulani kuhusika.




NI UGAIDI TU
Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasit, Arusha, lililipuliwa na bomu la mkono, Jumapili iliyopita, saa 4:30 asubuhi.
Iliripotiwa juzi (Jumapili) kuwa mmoja wa watuhumiwa wa tukio hilo, anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, mtu huyo alikamatwa muda mfupi baada ya msako dhidi ya washukiwa kuanza.
Kuhusu chanzo au sababu ya wahusika kufanya ulipuaji huo, bado ni siri nzito lakini Watanzania wameshauriwa kuwa watulivu, kwani hilo ni moja ya matukio ya kigaidi ambayo yanapenyezwa nchini kwa sasa.
“Sisi Watanzania tunajuana, hakuna Muislamu anayeweza kufanya shambulio dhidi ya Wakristo, kadhalika hakuna Mkristo anayeweza kufanya shambulio dhidi ya Waislamu, walipuaji ni magaidi, wakamatwe na washtakiwe kama magaidi.
“Haya maneno ya kusema watu wa dini moja wamewashambulia wa dini nyingine ni uchochezi mbaya na maneno ya aina hiyo yakiendelea yatatugawa Watanzania,” alisema Aminieli Moba, juzi, akiwa eneo la tukio, muda mfupi baada ya mlipuko.
Maneno ya Moba, hayapishani na ya Tito Hebrew, aliyeandika kwenye ukurasa wake wa Facebook: “Jamani hakuna udini, kuna chokochoko nyingi zinaibuliwa hapa. Watu walishataka kutugombanisha kwa njia za kisiasa wakashindwa.
“Kuna kipindi walijitahidi kutugombanisha kwa misingi ya ukabila ikawa ngumu, sasa hivi wanaamua kutumia njia za udini. Watanzania tunatakiwa tuutegue huu mtego, vinginevyo tutaingia kwenye vita ya sisi kwa sisi.”
TUKIO LENYEWE
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, akiwemo mtoto mdogo (wote tunawahifadhi), mwanaume aliyevalia koti kubwa lenye kofia, akiwa amejifunika usoni, alitokea upande wa kushoto wa kanisa hilo kwa mbele na kutupa bomu hilo.
“Nilikuwa nimesimama ghorofani, nikamwona mtu akiwa na koti la mvua akisogea mbele ya kanisa na kurusha kitu kilichotoa mlio mkubwa na baadaye watu walianza kulia kwa sauti ndiyo nikajua lilikuwa ni bomu,” alisema shuhuda mmoja.
Shuhuda mwingine alisema: “Yule mlipuaji alikuwa na mwenzake na walifika pale kanisani wakiwa na gari. Baada ya kurusha bomu, alirudi kwenye gari kisha wakakimbia.”
Hata hivyo, shuhuda huyo ambaye ni mtoto mdogo, hakuweza kufafanua gari hilo ni aina gani wala namba zake za usajili.
VIFO
Kwa mujibu taarifa za vifo mpaka sasa, watu watatu wamesharipotiwa kufariki dunia kutokana na tukio hilo.
Watu 70 walijeruhiwa katika shambulio hilo na wote walifikishwa kwenye Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru.
Waliojeruhiwa katika tukio hilo, wengi wao walionekana wakivuja damu nyingi, zilizolowanisha kabisa nguo zao.
Wengi wa waliojeruhiwa, walikatika viungo na wengine wamechanwachanwa, hivyo kuacha taharuki isiyomithilika.
MWAKILISHI WA PAPA CHUPUCHUPU
Mwakilishi wa Papa Francis I hapa nchini, Balozi Francisco Padilla, alinusurika kifo katika shambulio hilo.
Balozi Padilla aliyekuwa mgeni rasmi wa uzinduzi wa kanisa hilo, alikoswa na bomu, kwani lililipuliwa wakati akikamilisha ratiba za kubariki kanisa kabla ya kukata utepe, kuashiria mwanzo wa utoaji wa huduma za kikanisa.
Kanisa hilo ni jipya na ujenzi wake ulikamilika hivi karibuni, hivyo kugeuka gumzo kutokana, likitajwa kuwa moja ya makanisa yaliyojengwa kisasa kabisa ukanda wa Afrika Mashariki.
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu, pamoja na mapadri zaidi ya 200, walihudhuria hafla hiyo ya uzinduzi wa kanisa hilo lakini wote wamenusurika.
NI MAAFA KATIKATI YA SHEREHE
Msemaji wa Kanisa Katoliki Parokia ya Olasit, Father Festus Mwangwangi, alisema kuwa sherehe za uzinduzi zilianza vizuri lakini mambo yaliharibika baadaye.
Alisema, kabla ya tukio hilo waumini wa kanisa hilo walianza maandamano kuanzia Kanisa Katoliki la Burka ambalo ni kanisa mama, wakiongozwa na Askofu Lebulu, na ilipofika saa 3.30 asubuhi, walifika katika kanisa hilo la Mtakatifu Joseph.
“Maandamano yalipokamilika, balozi wa Vatican (mwakilishi wa Papa), aliwasili katika msafara wake na mwenyeji wake ambaye ni Askofu Lebulu, kisha akamtembeza kulikagua kanisa hilo.
“Baada ya kulikagua kanisa, lilifuata tendo la kubariki maji ambayo yangechanganywa na chumvi kisha kutumika kulibariki kanisa lakini tukiwa kwenye hatua ya kubariki maji ndipo mlipuko mkubwa ulisikika,” alisema Father Mwangwangi.
UVUMI KUHUSU SIASA
Kwa upande mwingine, yapo madai yaliyopo mkoani Arusha kwamba bomu hilo pengine ni njama za wanasiasa.
Inadaiwa kuwa kuelekea uzinduzi wa kanisa hilo, kuna mmoja wa mawaziri wakuu wastaafu, alitajwa sana kuwa angekuwa mgeni rasmi.
“Pengine watu wabaya dhidi ya huyo mheshimiwa, waliamini huo uvumi, sasa wakaona hiyo ndiyo sehemu ya kutekeleza njama zao,” alisema mkazi mmoja wa Arusha, Philipo Abdiel.
LEMA AKOSOLEWA
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, alifika eneo la tukio muda mfupi baada ya bomu kulipuka na kutoa matamshi makali dhidi ya serikali na udini.
Hata hivyo, wananchi wa Arusha waliozungumza na ripota wetu, walisema kuwa wanamheshimu sana Lema na wanampenda kama mbunge wao lakini anakosea kuweka siasa katika tukio zito kama hilo la ugaidi.
“Kuna mambo akichanganya na siasa itakuwa sawa lakini siyo hili. Lema anatakiwa kushirikiana na serikali katika vita dhidi ya ugaidi ambao unapenyezwa nchini,” alisema Rosemina Kiwia, mkazi wa Ngarenaro, Arusha.
POLISI WANENA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema: “Uchunguzi makini utafanyika. Hapa tutawaleta wataalamu wa mabomu na baada ya uchunguzi ndipo tutatoa taarifa rasmi ya jeshi la polisi.”
MKUU WA MKOA
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, aliwataka wananchi kuwa watulivu wakati vyombo vya dola vikiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
“Polisi kutoka makao makuu ya jeshi pamoja na wataalamu wa mabomu kutoka makao makuu wanatarajiwa kufika katika eneo la tukio ili kuongeza nguvu,” alisema Mulongo.
KAULI KALI YA WAZIRI NCHIMBI
Jana, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema kuwa watu wanaoeneza chuki za kidini hawatavumiliwa, watachukuliwa hatua kali sana.
“Tunaendelea na uchunguzi wetu lakini kuanzia sasa, serikali haitawavumilia watu wanaoeneza chuki za kidini, tutawachukulia hatua kali ili iwe fundisho,” alisema Nchimbi.
JK ASITISHA SAFARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete, alikuwa kwenye ndege safarini kwenda Kuwait, wakati shambulio hilo la bomu lilipofanyika na lakini alipofika na kujulishwa kilichotokea, alisitisha ziara yake na kurudi nchini.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, alisema kuwa baada ya kupata taarifa hiyo, aliwasiliana na viongozi mbalimbali nchini kwa ajili ya kupata picha halisi ya tukio.
“Sasa hivi (jana mchana), yupo njiani, atafika Dar es Salaam halafu kesho (leo) asubuhi atakwenda Arusha,” alisema Rweyemamu.
WALIOKAMATWA
Mpaka sasa, watu wanane walishakamatwa, mmojawapo akiwa mtuhumiwa nambari moja, anayefahamika kwa jina la Victor Ambrose, 20.
Inaelezwa kuwa Ambrose, aliwataja wenzake watatu ambao nao walikamatwa.
Vilevile, raia wanne wa Saudi Arabia, walikamatwasiku ya tukio wakiwa safarini kuelekea Kenya, wakipitia mpaka wa Namanga.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ametoa taarifa bungeni leo kuwa raia wa Saudi Arabia, waliokamatwa ni kwa ajili ya upelelezi kama kweli wanaweza kuwa wanahusika au la!
“Mpaka kesho, itakuwa imeshajulikana kama kweli wale wanahusika au la,” alisema Pinda.
Aunt Ezekiel, mumewe wakutana Sauzi
Mwigizaji Aunt Ezekiel ameonekana Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, akikwea pipa kumfuata mumewe, Dimonte Almousa, pande za Afrika Kusini.

Ripota wetu alimshuhudia staa huyo akikwea pipa mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya mumewe aishiye Dubai kumpa taarifa kwamba atakuwa Afrika Kusini kikazi hivyo wakutane kwa muda.

“Nakwenda Sauzi kwa muda wa wiki moja kwa ajili ya kukutana na mume wangu, sitakaa sana nitarudi Bongo kisha nitajiandaa kumfuata nyumbani kwetu Dubai,” alisema Aunt.
Hivi karibuni Aunt aliweka bayana kuwa hata iweje, kamwe hawezi kutengana na mumewe huyo.
Mashambulizi ya Jaydee kwa Ruge, Kusaga yaibua msukosuko
Mwanamuziki mkongwe wa Bongo Fleva, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ ameendelea kuwakaba koo wakurugenzi wa Redio Clouds FM, Joseph Kusaga na Ruge Mutahaba.
Jide, ameibua msukosuko wa aina yake nchini kufuatia tamko lake alilotoa jana, akibainisha kwamba Kusaga na Ruge si watu wema na hata akifa, redio yao isitangaze kifo chake wala kupiga nyimbo zake, vilevile na wao hawatakiwi kuhudhuria.

Hili ndiyo tamko lenyewe…
WOSIA WANGU KAMA IKITOKEA NIMETANGULIA KUFA KABLA YA RUGE AU JOE KUSAGA
Watu wanashtuka mtu akiongelea kifo, Utafikiri hawafahamu fika kuwa kila nafsi itakionja, Kwenye maisha yangu nimepitia mambo mengi, magumu na mepesi na bado naendelea ku-experience mambo magumu zaidi kadri ninavyozidi kuwa mkubwa.
Siku za karibuni nimekuwa nikipigwa vita sana na watu wenye uwezo mkubwa kifedha , ki umri na hata wenye ukubwa wa connection katika hii industry ya muziki. Wanaomiliki chombo cha habari.
Nasimama na kusema kuwa sitokata tamaa, kwani lengo lao kubwa ni kuona na kuhakikisha nimeanguka kabisa na sipo katika ramani ya muziki.

Watu hao ambao vita yao ilikuwa baridi miaka kumi iliopita, sasa inazidi kuwa moto baada ya kutambua kuwa mimi ni mtu mwenye maamuzi yangu na misimamo yangu bila kuburuzwa.
Wanapita kila mahali kuhakikisha kila mrija unaoniingizia chochote unakatika, na hiyo ni kutaka kuuthibitishia umma wa Tanzania kuwa hakuna msanii anaeweza ku survive bila wao. Mimi ni msanii tofauti na hao mnaofikiria.
Nadhani mnafahamu tangu niachane na Tuzo zenu mnazo influence nani apate nani asipate, na tangu niachane na Fiesta nilipolipwa laki 8 mara ya mwisho na kuamua kuunda Band ili nijiajiri na kupata shows zangu mwenyewe, ikafanikiwa sana jambo ambalo limewauma na kuamua kufanya kitu cha kuiangusha Band yangu. Nita survive kwa njia zozote MUNGU alizonipangia.

Wakati bado wote tunapumua na kwakuwa watu hao hawanipendi kabisa, Naamini fika hawataweza kunipenda hata siku nitakapokuwa nimekufa. Na huu ndio wosia wangu kwa watu hao.
Natambua wanaweza kutumia redio yao kutangaza sana kifo changu na kusema marehemu alikuwa mtu mzuri na pengine kupiga nyimbo zangu kuanzia asubuhi mpaka jioni.
Ila naomba nitamke hivi, siku nikifa CLOUDS FM isipige nyimbo zangu, wala isiongelee lolote kuhusiana na kifo changu. Ruge Mutahaba na Joseph Kusaga wasihudhurie msiba wangu, na mkiwaona muwapige mawa enyi mtakaokuwa hai baada yangu.
Kama wamenifitini, na hawajanipenda nikiwa hai hakuna haja ya kujifanya kunipenda nikiwa marehemu. Sina haja wanipende pia kwakuwa mimi sio ndugu yao, Ila ubaya wanaoundeleza mioyoni mwao wanaujua na nina hakika nafsi zao zinawasuta pia.
Niliamua kujiepusha nao miaka mingi na kufanya biashara zangu, nimekaa kimya watu wanafikiri nabebwa lakini sijabebwa chochote sikutaka ugomvi haya mambo yalianza baada ya Album yangu ya pili ya Binti mwaka 2003 nilipojitoa Smooth Vibes chini ya Ruge.
Nilivumilia fitna nikiamini ipo siku yatakwisha lakini naona moto ndio unazidi kuwaka. Na hii ni kwasababu wanaogopa msanii akiwa mkubwa watashindwa kumuamrisha, Hamuwezi kumiliki dunia..
Kama mnasema mlinibeba mbona hamkuwabeba dada zenu wa tumbo moja waimbe ili hela irudi nyumbani??. kama kweli wewe Kusaga unajua kubeba basi beba jiwe liimbe liwe star..
Kwa roho zenu mbaya mnaweza kumbeba mpita njia nyie? Talent haibebwi, hujibeba kama mnabisha si mna watoto wabebeni basi wawe kama kina Diamond ndio nitaamini kweli nyie mnaweza kubeba watu.
Mnawatishia wasanii kuwa yoyote atakaefanya nyimbo na mimi hazitapigwa, vikao vinne mmeshakaa kunijadili. Mnadhani je! nitapungukiwa nini endapo wasanii wengine wakiacha kufanya kazi na mimi?? nyimbo hazitakuwa nzuri.
Basi sawa ngoja tuone MUNGU ni nani, Binadamu nani? Kwahiyo mtaamrisha watu pia wasikae na mimi? Ilikuwa niseme majina matatu huyo mmoja nimemsamehe baada ya kugundua sio hiyari yake ila yuko under influence ya hawa jamaa wawili.
Kila siku mnamsingizia Ruge peke yake Kusaga ni mfitini kuliko hata huyo Ruge, watu hamjui tu.
Mtu hela zote hizo bado shillingi mbili ya Jide inakuuma? Roho gani hiyo??
Naishia hapo na sitabatilisha kauli yangu
Mbwa ndiye faraja pekee ya Wema kwa sasa
Miss Tanzania 2006-2007, Wema Sepetu amefunguka kuwa hakuna kitu kinachompa faraja kubwa kwa sasa kama mbwa wake, Ivan na Gucci.
Wema alisema hawezi kukaa zaidi ya siku tatu bila kuwaona mbwa wake hao kwani amewazoea kwa kuwa humuondolea ‘stress’ za hapa na pale.

“Juzikati nilikwenda Arusha mara moja tu siku hiyohiyo nikawa nawakumbuka Ivan na Gucci mpaka nikawa natamani kurudi kwa ajili yao, kusema kweli hawa ndiyo kila kitu kwangu,” alisema Wema na kuongeza:
“Nimewazoea lakini wao pia ndiyo zaidi, hawataki kubanduka pindi ninaporudi kutoka katika kazi zangu, mtu akiwachukua tu umewakorofisha.”
Mastaa wa Bongo, pete nyingi ndoa sifuri
Katika ulimwengu huu kuna mambo mengi yanayofurahisha. Yapo pia yanayosikitisha na utapeli katika uhusiano wa kimapenzi umetamalaki.
Utangulizi huo una maana kuwa katika jamii inayotuzunguka inabidi mtu uwe makini la ivyo utajikuta kwenye wakati mgumu hasa kwa wasichana wanaohitaji kuolewa.
Kumekuwa na tabia ya baadhi ya wanaume kuwarubuni wanawake wakiwadanganya kuwa watawaoa, ahadi ambazo hazitimii kwani mapenzi yao huwa yanaishia njiani kabla hawajatimiza lengo na kuwaacha wenzao katika maumivu makali.
Katika ulimwengu wa mastaa wa Kibongo, ishu hiyo ndipo nyumbani kwao ambapo leo katika makala haya tutaona orodha ya wasanii ambao wamevishwa pete za uchumba lakini suala la ndoa limeishia ndotoni.
Ni kama wanaota lakini wakiamka hujikuta wakijuta kuwa walikosea wapi. Kinachoonekana kwa sasa ni kwamba pete ya uchumba ni ndoano ya kumnasa mwanamke na baada ya kukidhi matwakwa humwacha bila kutimiza ahadi ya ndoa.
FLORA FESTO MVUNGI
Ni mwigizaji wa filamu za Kibongo anayeishi kinyumba na mwanamuzki wa Kizazi Kipya, Hamis Ramadhan Baba ‘H. Baba’.
Tangu Flora avishwe pete ya uchumba na H. Baba pamoja na kutolewa mahari, siku zimesonga bila kuona suala la ndoa likiendelea.
Wasanii hawa kila wakiulizwa kuhusu suala la ndoa huwa wanajibu hivi karibuni ambapo kwa sasa kuna madai kuwa tayari Flora ana ‘kibendi’.
ROSE DONATUS NDAUKA
Ni staa mkubwa wa filamu za Kibongo ambaye alichumbiwa kwa muda mrefu na jamaa aliyekuwa mmoja wa kundi la kitambo la Bongo Fleva kutoka Tanga la TNG, Malick Bandawe.

Rose amekuwa akiahidi kila kukicha kuwa harusi yake iko mbioni lakini umepita muda mrefu hakuna ndoa wala nini na badala yake wamebaki kuishi pamoja kama mume na mke.
OTILIA BONIFACE
Ni mkata mayenu kiraka wa Bendi ya Extra Bongo ‘Wazee wa Kizigo Staili’. Alivishwa pete ya uchumba miaka miwili iliyopita na mume wa mtu anayejulikana kwa jina moja la Ally lakini mpaka sasa ndoa imebaki ndotoni.
Otilia na mchumba wake huyo wanaishi pamoja kama mume na mke na suala la ndoa bado wanajiandaa.
SUZAN CHUBWA ‘QUEEN SUZY’
Ni mnenguaji bei mbaya wa Bendi ya FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’. Alivishwa pete ya uchumba zaidi ya miaka miwili iliyopita na aliyekuwa rapa wa bendi hiyo, Aimerichard Mwamba ‘G-Seven’ ambaye kwa sasa amehamishia makazi yake Nairobi, Kenya na kumwacha Suzy Bongo.

G-Seven alimposa Suzy pamoja na kumvisha pete ambapo uchumba wao ulidumu kwa muda mrefu kabla ya hivi karibuni bishosti huyo kuweka wazi kuwa ameamua kuachana naye kwa sababu aligundua kuwa siyo mwaminifu.
ISABELA MPANDA
Ni Miss Ruvuma 2006. Anasaka mkate wa siku kupitia filamu na muziki wa Bongo Fleva. Alivishwa pete ya uchumba kitambo na kutolewa mahari na mwanaume jina kapuni lakini aliishia kupewa mimba na kuzaa.
Baada ya kuzaa Isabela mpaka sasa hajaolewa na amejaliwa kuwa na watoto wawili kila mmoja na baba yake huku ikifahamika kuwa yupo kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwanamuziki Luteni Kalama.
MIRIAMU GERALD
Ni Miss Tanzania 2009 aliyevishwa pete ya uchumba na msanii wa filamu za Kibongo, Kennedy Victor ‘Kenny’. Walipanga kufunga pingu za maisha mwezi Juni, mwaka jana lakini hadi unaposoma hapa hakuna chochote zaidi kujaliwa mtoto mmoja wa kiume.
WEMA SEPETU
Ni mwanadada mrembo kutoka kiwanda cha filamu za Kibongo. alivishwa pete ya uchumba na mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nasib Abdul ‘Diamond Platnumz’ lakini mapenzi yao hayakufika mbali, waliishia kuachana na mambo ya ndoa yakaishia hapo huku bidada akiendelea kujikusanyia pete za uchumba kabatini kwake baada ya ile ya Yusuf Jumbe.
SHAMSA FORD
Ni staa wa filamu za Kibongo ambaye kwa muda mrefu amechumbiwa na jamaa mmoja aitwaye Dick. Uchumba wao una zaidi ya miaka miwili lakini ndoa imekuwa ni kitendawili huku wakijaliwa mtoto mmoja wa kiume aitwaye Terry.

SALMA JABU ‘NISHA’
Ni staa wa filamu za Kibongo ambaye aliwahi kudaiwa kuvishwa pete ya uchumba na mwigizaji mwenzake aitwaye Godfrey Kusila kabla ya uchumba kuvunjika na penzi kuhamia kwa mwanamuziki Elibariki Emmanuel ‘Ney wa Mitego’. Hata hivyo, kwa Ney wa Mitego napo uchumba uliota mbawa pamoja na kuwa na mbwembwe nyingi.

Nani fisadi yupi siyo, Usalama wa Taifa wakiamka nchi itanyooka
Idara ya Usalama wa Taifa ni nyeti. Hali ya ufisadi ilivyofikia sasa hivi, haiwezi kumalizwa na wanasiasa peke yao. Programu ya dharura inapaswa kuchukua nafasi na watekelezaji wake wanatakiwa wawe wazalendo kweli. Wenye tamaa wakae mbali, maana ndiyo wametufikisha hapa.
Pamoja na uwepo wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Usalama wa Taifa wanaweza kuwa msingi wa vita dhidi ya ufisadi. Kama wamelala katika eneo hili, wanapaswa kuamshwa, watambue kwamba maisha ya Watanzania yanahitaji nguvu na maarifa yao.

Watumishi wengi wa umma wanaishi maisha ya bandia. Wanafanya mambo makubwa tofauti kabisa na mishahara pamoja na marupurupu yao. Wanajenga majengo ya kutisha na kuendesha magari ya kufuru. Ajabu ni kwamba watu hao hawaguswi. Usalama wa Taifa mpo wapi?
Kama aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, aliandamwa kwa kununua nyumba ya shilingi milioni 650, ni kwa nini maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, hawafuatiliwi na hawachunguzwi? Kwa maana wanayoyafanya ni mazito.
Akaunti yake ina mabilioni ya shilingi, amezipataje? Amejenga nyumba yenye thamani ya shilingi bilioni tatu, amepata wapi fedha za kufanya hivyo? Anamiliki magari ya kifahari, ukijumlisha idadi yake na kuyapigia hesabu, yanaweza kugharimu zaidi ya shilingi bilioni moja.
Anatembea na wapambe siyo chini ya 10, anakutana nao kwenye hoteli zenye hadhi ya nyota tano, anawanunulia chakula, wanakula mpaka wanasaza, anawanywesha pombe hadi wanalewa tilalila. Kwa siku moja anaweza kutumia shilingi 2,000,000, kwa siku 10, milioni 20 zinakatika.
Mshahara wake na marupurupu vimekaaje? Maana pamoja na matumizi hayo, anawalipia kodi za nyumba wapambe ambao kazi yao kubwa ni kumtafutia tu wanawake. Hawana kazi, kwa hiyo anawapa mpaka fedha za matumizi ya kuendesha familia zao na starehe ndogondogo.
Hao wanawake, wenye bahati wanajengewa nyumba, wapo wanaonunuliwa zikiwa zimekamilika. Wengine wanapangiwa, vilevile kuna wanaoishia kupewa fedha. Kuhonga magari ndiyo usiseme, utadhani anayatengeneza yeye. Turudi kwenye swali la msingi, anapata wapi pesa?
Ofisa wa TRA, hata akiwa kamishna hana ubavu wa kufanya vurugu hizo. Lazima tu atakuwa anaiba. Wizi wenyewe ni uhuni wa ulipaji kodi. Wanakula na wakwepaji, na kwa sababu fedha zinakuwa za haramu, haoni hata woga wa kuzichezea, ndiyo maana anazitumia kama fimbo.
Tunawaona, wakali wa vita za kugombea wanawake. Wanashindana kuhonga vitu vya thamani ili kupata mapenzi (ngono). Siku zote mwizi akili yake huwa inalala, ukomo wa mawazo yake huishia katika kuiba na kutumia. Anaiba nyingi, anafanyaje sasa? Hii ndiyo sababu ya kufanya vurugu nyingi mitaani.
Nidhamu ya utumishi wa umma ni jambo ambalo linapaswa kusukwa upya. Wengi wanajiangalia wao peke yao. Usalama wa Taifa wakiamua, wanaweza kuchunguza aina ya watu ambao wanafaa kuwatumikia wananchi. Wezi, wenye tamaa, watapanya pesa hawatakiwi.
Inashindikana nini kwa Usalama wa Taifa kuchunguza mishahara ya watumishi wa umma lafu wakaoanisha na matumizi yao, kujua nani fisadi yupi siyo? Ni hesabu ndogo, tena ni kazi ambayo haihitaji hata siku 30. Wakifuatiliwa, ndani ya wiki moja watakuwa wameshabainika.
Inawezekana Usalama wa Taifa wanafuatilia mambo mengi kwa ajili ya kuhakikisha nchi ipo salama, hili la ufisadi katika kipengele cha mapato ya watumishi wa umma dhidi ya matumizi, wanawaachia Takukuru. Hapo ndipo wanapofanya makosa makubwa.
Takukuru wanafanya kazi kwa mtindo wa mazoea. Pale walipo, hawashughuliki na mtu mpaka wapewe taarifa kwamba mhusika amepokea au yupo kwenye harakati za kula/kutoa rushwa. Akifuatiliwa bila taarifa, hiyo ni janja ya maofisa fulani na wakishapozwa hunyamazwa kimya.
Tunataka watu wanaothubutu. Wale watakaosimama leo na kusema ufisadi ufike mwisho. Wenye uchungu na jasho la walalahoi. Walio na nia thabiti ya kumkomboa Mtanzania na hili janga la ugumu wa maisha. Usalala wa Taifa amkeni leo, tuanze mapambano ya mapato dhidi ya matumizi kwa watumishi wa umma, tutawanasa mafisadi wengi sana.
Jina la Biggie latumika kunadi mjengo
Mjengo wa kifahari uliopo eneo la Clinton Hill, Brooklyn, New York, Marekani, unauzwa kwa thamani ya dola za 750,000, sawa na shilingi 1.2.
Mchawi wa Freestyle, Christopher Wallace ‘Notorious B.I.G’, aliishi kwenye mjengo huo wakati akiwa mdogo.

Kwa vile B.I.G a.k.a Biggie aliishi hapo enzi hizo, wamiliki wa jengo hilo, wameamua kutumia jina lake kwa ajili ya kulinadi, kwa imani kwamba litapata wateja kwa urahisi.
Matangazo mengi mtandaoni, yanasomeka: “Nyumba aliyoishi Biggie inauzwa.”



Familia ya Biggie ambaye alifariki dunia miaka 16 iliyopita, haijatoa tamko kama inaona sawa au kuchukizwa na matumizi ya jina la mkali huyo wa Hip Hop katika mauzo ya mnada wa jengo hilo.
Barthez njiapanda Taifa Stars
KOCHA Mkuu Taifa Stars, Kim Poulsen ametangaza kikosi cha pili cha timu ya taifa, Taifa Stars, ambacho atakitumia kuangalia wachezaji anaoweza kuwaita kwenye kikosi cha kwanza huku jina la kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’ likiwemo na mchezaji kutoka England.
Akizungumza kabla ya kutaja kikosi hicho jana, Kim alisema hiyo ni sehemu ya Mpango wa Maendeleo wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) uliozinduliwa Aprili 4, 2013.
Amesema timu hiyo inajumuisha wachezaji ambao wamepita umri wa kuchezea timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, lakini hawajapata nafasi ya kucheza Taifa Stars.
“Leo (jana) ninatangaza timu ya pili ya Stars ambayo inaundwa na wachezaji wengi vijana wa umri chini ya miaka 20 na wachache ambao hawajapata nafasi ya kuichezea ile ya kikosi cha kwanza.
“Tofauti na vijana hao, pia nimeita wakongwe kama Barthez, Barnabas (Vicent) na David Mwantika kwa ajili ya kuwaangalia uwezo wao zaidi na kama nikiona wanafaa nitawapandisha kwenye timu ya kwanza,” alisema Kim.

Wachezaji walioitwa wataingia kambini Mei 2 hadi 6, mwaka huu. Walioitwa ni; Aishi Manula (Azam), Hussein Shariff (Mtibwa Sugar) ambao ni makipa. Mabeki ni Kessy Hassan (Mtibwa Sugar), Kennan Ngoma (Barnsley FC, Uingereza), Himid Mao (Azam), Ismail Gambo (Azam), David Mwantika (Azam), Miraji Adam (Simba), Mohamed Hussein (Kagera Sugar), Waziri Salum (Azam), Samih Nuhu (Azam) na Emily Mgeta (Simba).
Viungo ni; Haruna Chanongo, William Lucian, Jonas Mkude, Edward Christopher, Abdallah Seseme, Ramadhan Singano (wote Simba), Mudathiri Yahya (Azam), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Jimmy Shoji (JKT Ruvu), Farid Mussa (Azam) na Vicent Barnabas (Mtibwa Sugar).
Washambuliaji ni; Hussein Javu (Mtibwa Sugar), Jerome Lambele (Ashanti United), Zahoro Pazi (JKT Ruvu), Twaha Hussein (Coastal Union), Abdallah Karihe (Azam) na Juma Luizio (Mtibwa Sugar) na Barthez.
Miss Utalii sasa kimeeleweka
Baada ya Kambi ya Miss Utalii Tanzania 2012/13 ambayo imeanza upya kwa kasi ya ajabu ambapo wadau mbali mbali ikiwa ni asasi za Serikali, Taasisi mbalimbali, Makampuni pamoja na watu mbalimbali wamejitokeza kudhamini Fainali Hizo za Miss Utalii Tanzania Taifa Ambazo zitafanyika Mwanzoni mwa Mwezi Ujao.
Walio jitokeza Kudhamini ni pamoja na. TANAPA, Ngorongoro Crater, Tanzania Tourist Board, Mtwana Catering, Ikondolelo Lodge Hotel, Sahara Media Group, Mbasha Entertainment, Sophia Records,Nyinda Hotel, Tanga Beach Resort, Retco, Tanzania School of Journalism and Mass Communication, Oriental Berau De Change, Clouds Media Group, Times FM, Global Publishers, Tone Multimedia Group, Dar es salaam City College, Eden Hill College, Maweni Hotel.
Bado kuna wadau wengine mbalimbali ambao wanaendelea kujitokeza kwa ajili ya Kudhamini Fainali Hizo za Miss Utalii Tanzania 2012/13.
Mpaka sasa Kambi mpya ya Miss Utalii Tanzania 2012/13 ipo na inaendelea Vizuri, Warembo zaidi ya 30 wamejiandaa vizuri kwa ajili ya Fainali Hizo zitakazo fanyika Mwanzoni mwa mwezi Ujao ikiwa ni pamoja na Kutoka Mikoa yote Tanzania, Kanda Maalum ya Zanzibar na Vyuo vikuu Tanzania.
Washindi wa 1-5 wa Fainali za Taifa ,watawakilisha Tanzania katika mashindano mbalimbali ya Dunia yakiwemo ya International Miss Tourism World, Miss Tourism United Nation, Miss Heritage World, Miss Tourism University World, Miss Globe International n.k
Miss Utalii Tanzania ,hadi sasa tunashikilia Jumla ya mataji 5 ya Dunia na kimataifa, yakiwemo ya Miss Tourism World 2005-Africa,Miss Tourism World 2006-SADC,Miss Tourism World 2007-Africa, Miss Tourism Model Of The World 2008-Personality n.k